Mwanasheria Mkuu Mstaafu, Jaji Werema Afariki Dunia

 


Rais Samia Suluhu Hassan ametangaza kwa masikitiko makubwa kifo cha Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mstaafu, Mheshimiwa Jaji Mstaafu Frederick Werema, kilichotokea tarehe 30 Desemba 2024 katika Hospitali ya Muhimbili. Rais Samia alieleza hisia zake kupitia mtandao wa X, akitoa pole kwa familia ya mpendwa, Mheshimiwa Jaji Mkuu, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, majaji, ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu.

Rais Samia Suluhu alisema:
"Nimepokea kwa masikitiko taarifa ya kifo cha Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mstaafu, Mheshimiwa Jaji Mstaafu Frederick Werema. Ninatoa pole kwa familia, Mheshimiwa Jaji Mkuu, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Majaji, ndugu, jamaa na marafiki."

Awali, ujumbe ulioandikwa na Salome Ntaro, Katibu wa HW-Parokia ya Mt. Martha, ulisambaa kwenye mitandao ya kijamii akieleza kusikitishwa kwake na msiba huu mzito. Salome alisema:

"Kwa Masikitiko makubwa nimepokea taarifa ya kifo cha Mwenyekiti wetu wa Parokia ya Mt. Martha, Judge na Mwanasheria Mkuu Mstaafu, Mzee wetu Frederick Werema, kilichotokea mchana wa leo tarehe 30/12/2024 katika Hospital ya Muhimbili.
Tujumuike na familia yake katika sala na maombolezo kwa msiba huu mzito. Bwana ametoa na Bwana ametwaa, jina la Bwana lihimidiwe.
Taratibu Nyingine zinapangwa, tutaendelea kuwajulisha."

Salome pia aliendelea kutoa pole kwa familia ya Werema, akisema:

"Nawaombea kwa Mwenyezi Mungu awajalie subra na imani katika kipindi hiki cha kuomboleza msiba huu, na ailaze roho ya mpendwa wetu huyu mahali pema peponi."

Frederick Mwita Werema alizaliwa tarehe 10 Oktoba 1955, na aliwahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa Tanzania kuanzia mwaka 2009 hadi alipojiuzulu mwaka 2014. Kabla ya uteuzi wake kuwa Mwanasheria Mkuu, Werema alikuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania katika Divisheni ya Biashara.

0 Comments:

Post a Comment