Sakata la kupotea kwa mfanyabiashara Daisle Simon Ulomi, mwenye umri wa miaka 43, limefikia tamati ya kusikitisha baada ya kubainika kuwa alifariki dunia kwa ajali ya pikipiki.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Ulomi aliondoka ofisini kwake Sinza Kijiweni mnamo tarehe 11 Desemba 2024, majira ya saa 6:00 mchana, akielekea Temeke, Bandari Kavu kukagua makontena ya bidhaa zake.
Hata hivyo, hakurejea nyumbani, na juhudi za familia kumtafuta hazikuzaa matunda hadi walipopeleka taarifa ya kupotea kwake katika Kituo cha Polisi Chang’ombe mnamo tarehe 12 Desemba 2024.
Awali, taarifa za kupotea kwake zilianza kusambaa mitandaoni kupitia ukurasa wa Boniface Jacob kwenye mtandao wa X, ambapo alichapisha ujumbe ulioeleza:
“AMEPOTEA AMEPOTEA AMEPOTEA! Hakurudi nyumbani kwake tangu alipoondoka kazini tarehe 11 Desemba, 2024.”Jina: DAISLE SIMON ULOMIUmri: 43 miakaKazi: Mfanyabiashara
Polisi walifuatilia simu ya Ulomi na kubaini kuwa mara ya mwisho ilionekana eneo la Chang’ombe, lakini taarifa mpya zimeibuka zikionesha kuwa alihusika katika ajali ya pikipiki mnamo mchana wa tarehe 11 Desemba 2024.
Taarifa ya Jeshi la Polisi ilisema:
“Mwili wa marehemu ulifikishwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Mwananyamala kama mtu asiyefahamika, akisubiri kutambuliwa na ndugu zake.”
“Jeshi la Polisi linaendelea kufuatilia tukio hili kwa kina ili kubaini undani wa ajali hiyo, na taarifa zaidi zitatolewa pindi uchunguzi utakapokamilika.”
Aidha, pikipiki ya marehemu iliyoharibika vibaya imetambuliwa na polisi, na familia imeshaarifiwa kuhusu kifo chake.
Kwa mujibu wa taarifa yao ya tarehe 14 Desemba 2024, TRA ilieleza:
“Kwa mujibu wa kumbukumbu zetu, Bw. Daisle Simon Ulomi alichagua kampuni ya wakala wa forodha ya TWENDE Freight Forwarders Limited kushughulikia uondoshaji wa mizigo yake. TRA haijawahi kumuita wala kushirikiana naye moja kwa moja kwa jambo lolote.”
Hali hii inafunga ukurasa kwa masikitiko katika sakata lililozua maswali mengi, huku familia ya marehemu ikiomboleza msiba wa ghafla wa mpendwa wao.
No comments:
Post a Comment