Sunday, December 29, 2024

Ajali ya Ndege ya Jeju Air Kusini yaacha Vifo 179, Wafanyakazi Wawili Wanusurika

 


Ajali ya ndege iliyotokea katika mji wa Muan, Korea Kusini, imesababisha vifo vya abiria 179 na wafanyakazi wanne wa ndege. 


Watu wawili, ambao ni wafanyakazi wa ndege, walinusurika na walikolewa kutoka kwa mabaki ya ndege na kupelekwa hospitalini kwa matibabu.



Kulingana na taarifa rasmi, ajali hiyo ilihusisha ndege aina ya Boeing 737-800 ya kampuni ya Jeju Air. 


Wote 175 wa abiria waliokuwa kwenye ndege walipoteza maisha, pamoja na wafanyakazi wanne wa ndege hiyo, ambao walikuwa sehemu ya wahanga wa ajali hii. 



Familia za waliokufa zimejumuika kwenye uwanja wa ndege kwa ajili ya kutoa heshima za mwisho huku shughuli za uokoaji zikiendelea.



Picha za ajali zimekuwa zikisambaa kutoka eneo la tukio, ambapo wafanyakazi wa uokoaji wanajaribu kufukua mabaki ya ndege kwa matumaini ya kupata taarifa zaidi kuhusu chanzo cha ajali hiyo. 



Kaimu Rais wa Korea Kusini, Choi Sang-mok, alifika kwenye eneo la ajali akiongoza juhudi za kutoa msaada wa haraka, ikiwa ni pamoja na huduma za afya na vifaa vya kusaidia wahanga. 


Ofisi ya rais imesema kuwa serikali itahakikisha familia zilizofiwa zinapata msaada wa kutosha.


Ajali hii ni moja ya ajali mbaya zaidi katika historia ya Korea Kusini, nchi inayojivunia rekodi nzuri ya usalama wa ndege katika miaka ya hivi karibuni. 


Jeju Air, kampuni ya ndege ya bei nafuu iliyoanzishwa mwaka 2005, ni moja ya mashirika makubwa ya ndege nchini humo. 


Ajali hii ni ya kwanza katika historia ya Jeju Air, huku kampuni hiyo ikitoa rambirambi kwa waathiriwa wa ajali na kuahidi kuchukua hatua za dharura ili kusaidia familia zilizopoteza wapendwa wao.



Mkurugenzi Mtendaji wa Jeju Air, Kim E-bae, aliomba radhi hadharani kwa waathiriwa wa ajali hiyo akisema kuwa kampuni yake inashirikiana na mamlaka za uokoaji ili kukabiliana na madhara yaliyosababishwa na ajali hiyo. 


Alisisitiza kuwa msaada kwa waathiriwa na familia zao ndiyo kipaumbele cha kampuni kwa sasa.


Chanzo cha ajali hiyo bado hakijathibitishwa, ingawa vyombo vya habari nchini Korea Kusini vimeripoti kuwa huenda ilitokana na hitilafu kwenye mfumo wa ndege. 


Hata hivyo, uchunguzi wa kina unaendelea ili kubaini sababu kamili ya ajali



Ajali hii inahusisha ndege aina ya Boeing 737-800, ndege maarufu inayotumika sana na mashirika ya ndege duniani. 


Boeing imejibu kwa kutoa rambirambi kwa waathiriwa na kusema kuwa inawasiliana na Jeju Air ili kutoa msaada wa kiufundi na kujua zaidi kuhusu kilichosababisha ajali hiyo.


Kwa sasa, hii inabakia kuwa ajali ya ndege mbaya zaidi ya aina yake katika ardhi ya Korea Kusini, na inatoa changamoto kubwa kwa Jeju Air, ambayo imekuwa na sifa nzuri ya usalama hadi sasa. Huu pia ni mtihani mkubwa kwa sekta ya usafiri wa anga katika nchi hiyo.

No comments:

Post a Comment