Ajali ya Magari Mawili Yagongana Yasababisha Vifo vya Watu Tisa

 


Rombo, Kilimanjaro – Tarehe 26/12/2024, majira ya saa tisa na dakika arobaini jioni, ajali mbaya ya barabarani ilitokea huko Kijiji cha Kibaoni, Tarafa ya Tarakea, Wilaya ya Rombo, Mkoa wa Kilimanjaro, baada ya magari mawili kugongana kwenye barabara kuu ya Moshi – Tarakea.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa, ajali hiyo ilihusisha gari la abiria la aina ya Toyota Noah lenye namba za usajili T959 CKU, lililotoka Tarakea kuelekea Moshi, kugongana na basi la abiria la aina ya Yutong lenye namba za usajili T620 DZQ, lililotoka Dodoma kuelekea Tarakea. Gari la Noah lilikuwa limejaa abiria, na lilipogongana na basi hilo, watu tisa (9) waliokuwa kwenye gari la Toyota Noah walipoteza maisha.

Watu waliokufa ni pamoja na:

  • Mamasita Lowasa (27), mkazi wa Kamwanga
  • Damarisi Kanini Mwikau (22), mkazi wa Elast, Kenya
  • Peter Alex Urio (38)
  • Monica Joyce Mumbua (64), Mkenya
  • Eligatanasi Kanje (30), mkazi wa Tarakea
  • Hilda Francis Leberatus (24), mkazi wa Kikelelwa

Mili mingine ya watu watatu haijatambuliwa hadi sasa.

Aidha, mtembea kwa miguu mmoja ambaye alijeruhiwa katika ajali hiyo amepelekwa katika Hospitali ya Huruma, Wilaya ya Rombo kwa matibabu. Hali yake bado haijafahamika.

Uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa ajali ilitokana na uzembe wa dereva wa gari dogo la abiria (Toyota Noah), ambaye alijaribu kuyapita magari mengine bila kuchukua tahadhari ya kutosha.

Mili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Huruma, Wilaya ya Rombo, kwa ajili ya uchunguzi wa kimatibabu na taratibu zingine.

Kamanda Simon Maigwa ametoa wito kwa madereva kuwa waangalifu na kuchukua tahadhari zaidi ili kuepuka ajali zinazosababisha vifo na majeruhi.

0 Comments:

Post a Comment