Yanga SC Yaachana na Kocha Wake Miguel Gamondi

 





Klabu ya Yanga SC imetangaza rasmi kuachana na Kocha wake mkuu, Miguel Gamondi, pamoja na msaidizi wake, Moussa Ndaw, hii leo Ijumaa, 15 Novemba, 2024kupitia taarifa iliyotolewa kwenye ukurasa wa Instagram wa klabu hiyo.



Gamondi, raia wa Argentina, alijiunga na Yanga SC mwezi Juni 2023 akichukua nafasi ya Mtunisia Nesreddine Nabi, ambaye alihamia AS FAR Rabat ya Morocco. Kocha huyo alisifika kwa mbinu zake za kufundisha mpira wa kushambulia na wenye burudani, akileta mtindo wa soka lenye ladha ya Amerika Kusini. Chini ya uongozi wake, Yanga iliweza kushinda Kombe la Shirikisho Tanzania, Kombe la Ligi Kuu Tanzania Bara, na kufika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.


Hata hivyo, sababu zinazosemekana kupelekea Gamondi kuachishwa kazi ni kushindwa kudhibiti nidhamu ya wachezaji, kupoteza uwezo wa kushawishi wachezaji katika vyumba vya kubadilishia nguo, na kushuka kwa viwango vya wachezaji katika kikosi chake. Hali hii ilidhihirishwa zaidi baada ya Yanga SC kupoteza michezo miwili mfululizo katika Ligi Kuu dhidi ya Azam FC kwa goli 1-0 na Tabora United kwa 3-1, kabla ya mapumziko ya michezo ya kufuzu michuano ya AFCON 2025.


Habari zisizo rasmi zinadai kuwa klabu hiyo ipo mbioni kumpa nafasi kocha mpya, Sead Ramović, ambaye hivi karibuni aliifundisha TS Galaxy ya Afrika Kusini. Ujio wa Ramović umeongeza uzito kwenye tetesi za kuachishwa kazi kwa Gamondi.


Gamondi ataacha kumbukumbu muhimu, akiwa ndiye kocha pekee aliyeweza kuiongoza Yanga kushinda michezo minne mfululizo dhidi ya Simba SC katika Dabi ya Kariakoo, rekodi ambayo haijawahi kufikiwa na kocha mwingine.


Klabu ya Yanga inajiandaa kuanza upya chini ya uongozi mpya kwa lengo la kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Kombe la Shirikisho Tanzania, na kufanya vizuri katika Ligi ya Mabingwa Afrika. Mechi yao ijayo baada ya mapumziko ya michezo ya timu za taifa itakuwa dhidi ya Al-Hilal Omdurman, tarehe 26 Novemba.


0 Comments:

Post a Comment