Jeshi la Polisi nchini linamshikilia askari wa Magereza kwa tuhuma za kusababisha kifo cha George Juma (41), mgombea wa kitongoji cha Stendi, kata ya Mkwese, jimbo la Manyoni Mashariki kupitia chama cha upinzani Chadema.
Tukio hili limetokea wakati wa purukushani zilizojitokeza katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaoendelea nchini.
Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi, marehemu George Juma alijeruhiwa kwa risasi katika vurugu zilizoanza baada ya wafuasi wa Chadema kudaiwa kuwavamia wafuasi wa CCM waliokuwa katika kikao cha ndani.
Polisi walisema kuwa askari wa Magereza kutoka kituo cha karibu waliitwa na walipofika eneo la tukio, walishambuliwa kwa mawe.
"Askari walipiga risasi hewani ili kuwazuia wafuasi wa Chadema, lakini kwa bahati mbaya risasi moja ilimpata marehemu George Juma," ilisema taarifa ya Polisi.
Hata hivyo, Chadema imekanusha madai hayo, ikitoa taarifa inayokinzana na ile ya Polisi. Chama hicho kilieleza kuwa George Juma alivamiwa nyumbani kwake na watu waliotajwa kuwa makada wa CCM, jambo lililoibua mzozo.
"Polisi walifika nyumbani kwa George Juma, wakampiga risasi na kusababisha kifo chake," ilisomeka sehemu ya taarifa ya Chadema.
Tukio Lingine la Mauaji
Katika tukio jingine, mwanachama na kiongozi wa Chadema, Steven Chalamila, ameripotiwa kuuawa kwa kushambuliwa na mapanga katika mji wa Tunduma usiku wa kuamkia Novemba 27, 2024.
Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari mbalimbali, Chadema imesema kuwa mauaji hayo yalitokea nyumbani kwa Chalamila, lakini Jeshi la Polisi bado halijatoa taarifa rasmi kuhusu tukio hilo.
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Chini ya Utata
Matukio haya ya vurugu na vifo yanajiri wakati ambapo Tanzania imeanza uchaguzi wa serikali za mitaa.
Uchaguzi huu una lengo la kuwachagua viongozi wa vijiji na mitaa , lakini vurugu zilizoripotiwa zimeleta hali ya taharuki.
Huku uchaguzi ukiendelea, wadau mbalimbali wanatoa wito wa amani na utulivu ili kuhakikisha demokrasia inachukua mkondo wake bila madhara kwa maisha ya watu.
No comments:
Post a Comment