Sunday, November 10, 2024

TIRA YATOA ELIMU YA BIMA KWA VYAMA VYA USHIRIKA ARUSHA

 


Happy Lazaro ,Arusha 


Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) kanda ya kaskazini imetoa elimu kwa viongozi wa vyama vya ushirika mkoa wa Arusha kuhusu maswala ya bima na shughuli zinazotekelezwa  na Mamlaka hiyo.



Akizungumza wakati akitoa  elimu hiyo katika shule ya Arusha , Afisa Bima  kutoka TIRA kanda ya kaskazini, Caroline Makiluli amesema kuwa, utoaji wa elimu ni miongoni mwa majukumu ya Taasisi hiyo katika kuwafikia wananchi wa Makundi mbalimbali ili waweze kutambua umuhimu wa matumizi ya bidhaa za bima.



Viongozi hao wamepatiwa elimu kuhusu shughuli za Mamlaka hiyo, mafanikio katika sekta ndogo ya bima, maana ya bima, aina za bima, bidhaa mbalimbali za bimana fursa zilizopo katika sekta ndogo ya bima.


"Tumeweza  kutoa elimu juu ya umuhimu wa bima na baadhi ya bidhaa za bima zilizopo sokoni, fursa zilizopo  kwenye sekta ndogo ya bima, makundi ya watoa huduma za bima wanaosajiliwa na Mamlaka, namna ya kuhakiki uwepo wa bima na masuala mengineyo "amesema Caroline.


Aidha, amefafanua zaidi kuwa, wamefikia hatua ya kuwasilisha mada kuhusu umuhimu wa bima kwani vyama vya ushirika vingi vina sera ya mikopo, hivyo matumizi ya bima ya mkopo ni muhimu sana kwa ajili yao.


"Kuna faida kubwa sana ya kuwa na bima ya mkopo kwani kama mkopaji  amefariki kabla ya kukamilisha marejesho, basi Kampuni ya Bima  itarudisha kiasi cha mkopo wa fedha kilichobaki. Fursa hiyo ni muhimu sana kwa wanachama hao kuweza kutumia na kuweza kutoa elimu kwa wanachama wenzao" amesema Caroline. 



Aidha ameongeza kuwa, zoezi hilo la utoaji elimu kwa makundi mbalimbali ni endelevu kwani ni moja ya majukumu ya Mamlaka hii  ili waweze kufahamu kazi zinazotekelzwa na TIRA na kuweza kuwa mabalozi wazuri katika maeneo yao ."amesema Caroline



Kwa upande wa washiriki waliokuwa kwenye semina hiyo, Meneja wa Nanenane Women Saccos, Leticia Ng'hoboko amesema kuwa, wamefurahi kupata elimu hiyo kwani watanzania wengi hawana tabia ya kukata bima za majengo, hivyo elimu hiyo itawasaidia kwa kiwango kikubwa sana kukata bima ya jengo huku akiomba Mamlaka hiyo kuendelea kutoa elimu kwa wananchi zaidi. 



Naye Meneja wa Braeburn staff Saccos Kisongo  na Njiro, Peter Maqway  amesema kuwa, waweza kupata elimu kutoka TIRA kuhusu  Mamlaka hiyo na kazi wanazofanya ambapo  wameweza kupata elimu mbalimbali kuhusu maswala ya bima ambayo wengi wao hawakuwa na elimu ya kutosha kuhusu maswala hayo.



No comments:

Post a Comment