Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, amesema kuwa mifarakano ndani ya chama hicho ni jambo la kawaida katika siasa, akisisitiza kuwa chama chochote cha siasa kisichokuwa na changamoto kama hizo ni chama mfu.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Mbowe alisema:
“Mara nyingine viongozi ndani ya chama wanatofautiana kauli, na kuna wakati wanakwenda mbali zaidi, lakini kama chama tuna taratibu za kuyamaliza ndani kwa ndani. Hili ni jambo la kawaida, hasa kwa chama hai kama CHADEMA.”
Kauli hiyo ya Mbowe imekuja siku chache baada ya Makamu Mwenyekiti wa chama hicho (Bara), Tundu Lissu, kuibua masuala tata, akilalamikia kile alichokiita rushwa, mikanganyo ya uchaguzi wa serikali za mitaa, na maridhiano ya uongo kati ya CHADEMA na serikali.
Tundu Lissu Kuanza Kampeni
Mbowe aliongeza kuwa licha ya changamoto zilizopo, Tundu Lissu ataendelea na majukumu yake ya kisiasa na anatarajiwa kuanza kampeni za uchaguzi wa serikali za mitaa kesho katika Wilaya ya Ikungi kabla ya kuelekea Tarime.
“CHADEMA ni chama cha demokrasia, na hata pale tunapokosana tunajua namna ya kurekebisha mambo. Ndio maana, licha ya kauli tata za baadhi ya viongozi, kampeni zinaendelea kama kawaida,” alieleza Mbowe.
Hoja za Lissu Zajibiwa
Siku chache zilizopita, CHADEMA kilitoa taarifa rasmi kikijibu hoja zilizotolewa na Tundu Lissu bila kumtaja moja kwa moja. Katika taarifa hiyo, chama hicho kilisema hakijawahi kupokea maelezo yoyote kuhusu madai ya kugawana majimbo au nafasi za madaraka kati ya chama na serikali.
Msimamo wa CHADEMA Kuhusu Uchaguzi
Mbowe pia alizungumzia maandalizi ya uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024, akibainisha kuwa chama hicho kimepitisha asilimia 33.2 ya wagombea wa nafasi mbalimbali. Hata hivyo, aliendelea kusisitiza msimamo wa chama wa kushiriki uchaguzi huo licha ya changamoto zilizopo.
“Wagombea wetu wamepata changamoto nyingi, lakini hatujajiengua. Tunaamini katika kupigania nafasi hizi kwa njia ya kidemokrasia, hata kama mazingira siyo rafiki,” alisema Mbowe.
Mnyika Akanusha Kauli ya TAMISEMI
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika, alikanusha madai yaliyotolewa na Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa, aliyedai kuwa vyama vyote vya siasa vilikubaliana hatua zote za uchaguzi huo.
“Hakuna makubaliano ya pamoja kuhusu hatua za uchaguzi huu kama inavyodaiwa. Tunapinga taarifa hiyo na kusimamia ukweli,” alisema Mnyika.
Uchaguzi wa serikali za mitaa nchini Tanzania unatarajiwa kufanyika katika mazingira yanayofanana na yale ya mwaka 2019, ambapo chama tawala CCM kilipata ushindi mkubwa, huku wagombea wa upinzani wakikumbana na changamoto nyingi.
No comments:
Post a Comment