Friday, November 1, 2024

Makamu wa Rais: Tutamuenzi Jenerali Musuguri kwa Kujitolea Kulinda Taifa



Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango, ametoa wito kwa Watanzania wote, raia na askari, kujitolea hata kufa ikiwa inahitajika, kwa ajili ya kulinda na kutetea uhuru, heshima, na maslahi ya Taifa. 



Akizungumza wakati wa kuaga mwili wa aliyekuwa Mkuu wa Majeshi Mstaafu, Jenerali David Bugozi Musuguri, katika Hospitali Kuu ya Jeshi Lugalo jijini Dar es Salaam, Makamu wa Rais amesisitiza umuhimu wa kuenzi mchango wa Jenerali Musuguri.



Dkt. Mpango ametoa rai kwa vijana wa Tanzania kuipenda nchi yao na jeshi lao kwa moyo wa dhati na kuwa tayari kulinda Tanzania kwa gharama yoyote, akisema, "Jenerali Mstaafu Musuguri ametufundisha kujitoa kwa dhati kwa ajili ya nchi yetu."



Akitoa salamu za pole kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais alitoa pole kwa Mkuu wa Majeshi, Jeshi la Wananchi wa Tanzania, familia ya marehemu, ndugu, na Watanzania wote walioguswa na msiba huu. 



"Serikali inaiombea faraja familia ya hayati Musuguri na wote walioguswa na msiba huu. Serikali na Taifa zima tupo pamoja nao," amesema.



Dkt. Mpango amewaasa makamanda na wapiganaji waliopewa dhamana ya uongozi katika Jeshi la Wananchi wa Tanzania kuendelea kufuata mfano bora uliyoachwa na Jenerali Musuguri. 



Ameeleza kuwa Jenerali Musuguri alikuwa mwalimu na mlezi wa askari vijana, na alifanya jitihada kubwa katika kujenga na kuliimarisha Jeshi la Wananchi wa Tanzania.



"Alipokuwa akiongoza jeshi letu, alifanikiwa kuwaandikisha vijana wengi na kuimarisha Jeshi letu hadi likawa moja ya majeshi bora na imara barani Afrika. 


Ni kwa uongozi wake ndiyo maana Jeshi la Idd Amin lilipovamia ardhi ya Tanzania lilidhibitiwa na Jeshi la Wananchi likiongozwa na Jenerali Musuguri," aliongeza Dkt. Mpango.


Shughuli hiyo ya kuaga mwili wa Jenerali Musuguri ilihudhuriwa na viongozi wa serikali pamoja na wananchi mbalimbali waliokuja kumuenzi shujaa huyo wa Taifa. 


Mwili wa Jenerali Musuguri uliwasili katika viwanja vya Hospitali ya Jeshi Lugalo kwa heshima kubwa, huku Makamu wa Rais na waombolezaji wakitoa heshima za mwisho kwa kiongozi huyo aliyelitumikia Taifa kwa moyo wa uzalendo.

No comments:

Post a Comment