Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko, amesema kuwa aliyewahi kuwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Mstaafu David Bugozi Musuguri, alijitolea kwa moyo wake wote kuhakikisha Tanzania inabaki kuwa na amani, usalama na mshikamano.
Pia, alifundisha jamii umuhimu wa kuipenda na kuilinda nchi kwa dhati.
Dkt. Biteko aliyasema hayo leo, Novemba 4, 2024, huko Butiama mkoani Mara, alipokuwa akiwasilisha salamu za Serikali kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, wakati wa mazishi ya Jenerali Mstaafu Musuguri.
"Katika uhai wa kila mmoja wetu, ni jambo gani mtu atakumbukwa nalo? Baba huyu ameacha alama ya uzalendo, kujitoa kwake, na kuipenda nchi," alisema Dkt. Biteko.
"Musuguri alikuwa mstari wa mbele kuliokoa Taifa lake.
Tujiulize sisi tuliobaki tutaacha alama gani? Yeye aliacha alama ya kulikomboa Taifa letu," aliongeza.
Dkt. Biteko pia alieleza kuwa Jenerali Musuguri alikuwa kiongozi aliyetamani amani na aliamini katika nguvu ya mshikamano.
"Hakuna vita iliyo nzuri. Alisisitiza mshikamano, na katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi, tushikamane na tuendelee kufanya amani iwe tunu ya Taifa letu," alisema Dkt. Biteko.
Aidha, Dkt. Biteko alisisitiza kuwa Serikali itaheshimu na kuenzi mchango wa Jenerali Musuguri kwa daima, na kutaja kuwa alitunukiwa medali kadhaa, ikiwemo ya Vita ya Kagera.
Aliahidi kuwa Serikali itaendelea kusimamia ujasiri, uzalendo, na kuthamini amani aliyopigania.
Pia, Dkt. Biteko aliihimiza familia ya Jenerali Musuguri kuendeleza umoja na mshikamano miongoni mwao.
Alitoa shukrani kwa madaktari wote waliomhudumia wakati wa kuugua kwake.
Kwa upande wake, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Stergomena Tax, alisema, "Taifa limepoteza hazina kubwa.
Kamwe, Jenerali Musuguri hatasahaulika kwa mema yake yote, na Jeshi litaenzi mchango wake."
Naye, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi wa Wananchi wa Tanzania, Jenerali Jacob Mkunda, alisema kuwa kifo cha Jenerali Musuguri ni pigo kubwa si tu kwa Jeshi bali kwa Tanzania nzima.
"Alishiriki Vita vya Pili vya Dunia ambavyo vilimjenga, kumkomaza, na kumpa uzoefu mkubwa. Aliporejea nchini, alitumia uzoefu huo kujenga Taifa lake na kuandaa mipango mbalimbali ya kivita, ikiwa ni pamoja na vita vya mvamizi Iddi Amini na vya ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika," alisema Jenerali Mkunda.
Askofu wa Jimbo la Kanisa Katoliki Musoma, Michael Msonganzila, wakati wa misa ya mazishi, alisema kuwa watu wamekusanyika kwa wingi kumuaga Jenerali Mstaafu Musuguri.
"Kilichotukutanisha ni misa ya kumuombea Musuguri aende kwa safari ya amani kwa aliyetuumba," alisema Askofu Msonganzila.
Aliongeza kuwa, "Kumuombea Jenerali huyu ni tendo la kiimani, tunaamini Yesu alikufa, akazikwa, na kufufuka, na tunaamini Mungu atawakutanisha waliokwisha fariki na Yesu Kristo."
Chifu wa Kabila la Zanaki, Japheti Wanzagi, alimsifu Jenerali Musuguri kwa unyenyekevu wake na moyo wa kusaidia kila mtu.
"Mzee huyu hakuwa na ukwasi wa mali bali utajiri wa utu wema. Wengi wetu tulipenda kukaa naye na kuzungumza naye mara kwa mara.
Kwa ujumla tunamshukuru Mzee kwa ukarimu na moyo wake wa kusaidia wahitaji," alisema Chifu Wanzagi.
Jenerali Mstaafu David Bugozi Musuguri alizaliwa Januari 4, 1920, kijijini Butiama na kufariki Oktoba 29, 2024, katika Hospitali ya Rufaa Bugando iliyopo Mwanza.
Alitumikia Jeshi kwa miaka 43, akihitimu kozi mbalimbali za kijeshi hadi kufikia cheo cha Jenerali mwaka 1985. Mazishi yake yaliambatana na upigwaji wa mizinga ya heshima 17.
No comments:
Post a Comment