Na Kassim Nyaki, NCAA.
Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya eneo la Ngorongoro (NCAA) Dkt. Elirehema Doriye ametembelea timu za NCAA zinazoshiriki mashindano ya SHIMMUTA Jijini Tanga na kusisitiza wachezaji kuzingatia nidhamu katika michezo yote wanayoshiriki.
Akizungumza na wachezaji wa NCAA wanaoshiriki michezo mbalimbali katika mashindano hayo, Dkt Doriye amebainisha kuwa, watumishi wa NCAA kushiriki michezo hiyo inachangia kuimarisha afya zao , kujikinga na magonjwa mbalimbali, kupanua mtandao wa ushirikiano na taasisi zingine na kuisaidia NCAA kutangaza utalii wa ndani kupitia vivutio vya utalii vilivyopo Ngorongoro kupitia washiriki wa michezo hiyo.
"Nawapongeza kwa jinsi mnavyoendelea kujitoa katika michezo mnayoshiriki, nimemabiwa baadhi ya timu kama Kamba (wanawake na wanaume) pamoja na timu ya mpira wa miguu za NCAA tayari zimefuzu kwenda hatua ya robo fainali huku michezo mingine ikiwa inaendelea, endeleeni kujitoa katika michezo hii lakini mhakikishe mnazingatia nidhamu kwa kila mchezo" amesisitiza Dkt. Doriye.
Michezo ya Shirikisho ya mashirika ya Umma na ya Sekta binafsi (SHIMMUTA) iliyofunguliwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Dotto Biteko ilianza tarehe 11 Novemba na itahitimishwa tarehe 22 Novemba, 2024 jijini Tanga.
0 Comments:
Post a Comment