Saturday, October 12, 2024

WATU ELFU MOJA WAJITOKEZA KUSHIRIKI MBIO ZA DYSLEXIA AWARENESS RUN OKTOBA 20

Happy Lazaro, Arusha .



Washiriki Elfu moja wanatarajiwa kushiriki katika mbio za "Dyslexia Awareness Run" zinazotarajiwa kufanyika oktoba 20 mwaka huu katika uwanja wa mgambo mkoani (karibu na Gymkhana) Arusha .




Hayo yamesemwa mkoani Arusha na Mwanzilishi na Mkurugenzi  wa Taasisi ya Dyslexia Tanzania , Caudence Ayoti ambao ndio waandaaji wa mbio hizo .




Amesema kuwa, lengo la mbio hizo ni kusambaza uelewa kuhusiana na Dyslexia kwani Taasisi hiyo inajihusisha na kusambaza uelewa kuhusu  changamoto za kujifunza kwa watoto. 



"Dyslexia ni changamoto ambayo inampata mtoto katika kujifunza ,kuandika, kusoma  na kuhesabu ambapo mbio hizo zitasaidia taasisi hiyo kuendelea kusambaza uelewa kuhusiana na changamoto hiyo kwenye jamii".amesema Ayoti. 



Ayoti ameongeza kuwa ,washiriki hao watakimbia mbio za kilometa 5 na 10 ambapo  washiriki kwenye mbio hizo watapata medali za kipekee kutoka Shanga Foundation ambazo zinatengenezwa  na walemavu ikiwa ni njia mojawapo ya kuwaunga mkono pia.



Aidha amesema kuwa,kiingilio katika mbio hizo ni shs 35,000 ambapo ametoa wito kwa wananchi mbalimbali kujitokeza kwa wingi kushiriki katika mbio hizo ili waweze kuiunga  taasisi hiyo mkono katika kuendelea kusaidia watoto wenye changamoto hiyo.



Kwa upande  wake  Meneja Rasilimali watu kutoka Shanga Foundation ambao ndio   wamefadhili  medali hizo,Janet Steven amesema kuwa,Taasisi hiyo ya kijamii inashughulika na watu wenye ulemavu ambao wamekuwa wakitengeneza medali  hizo wa lengo la kujipatia kipato. 



Amesema kuwa, taasisi hiyo imechukua  uamuzi wa kufadhili  mbio hizo kwa lengo la kuwasaidia walemavu hao  na pia kusambaza uelewa kuwa wanaweza  ili waweze kuungwa  mkono kwani medali hizo  ndio wametengeneza wenyewe.


Kw upande wake Mwenyekiti chama cha riadha mkoa wa Arusha ,Gerald Babu ameipongeza  taasisi hiyo kwa kuanzisha mbio hizo ambazo zinalenga  kutatua changamoto  hiyo ya Dyslexia  kwa watoto kwani ni jambo zuri sana na ni mfano wa kuigwa na jamii.


Babu ametoa wito kwa wadau na jamii mbalimbali  kujitokeza kwa wingi katika mbio hizo kwa lengo la  kuwaunga mkono kwa ajili ya kusaidia  jitihada hizo .



No comments:

Post a Comment