Kesi ya Kumuondoa Naibu Rais Gachagua Yapangiwa Kusikilizwa na Jopo la Majaji

 


Jaji Lawrence Mugambi ameagiza kesi ya kupinga kutimuliwa kwa Naibu Rais Rigathi Gachagua kupelekwa kwa Jaji Mkuu Martha Koome ili kuunda jopo la majaji litakalosikiliza na kuamua suala hilo. 


Katika uamuzi wake wa Ijumaa asubuhi, Jaji Mugambi alisema kuwa ombi hilo linagusa masuala mazito ya kikatiba, hivyo inahitajika jopo kusikiliza na kutoa uamuzi wake.


Huku hayo yakitokea, ratiba iliyotolewa na Karani wa Seneti imeonyesha kuwa Naibu Rais Gachagua anatarajiwa kuwasilisha ushahidi wake Alhamisi, Oktoba 17. 


Atakuwa na saa nne kuanzia saa tatu asubuhi hadi saa saba mchana kuwasilisha utetezi wake dhidi ya mashtaka yanayomkabili. Kikao cha pili kimepangwa kufanyika alasiri ambapo Gachagua atahojiwa na maseneta.


Mawakili wa Naibu Rais wataweza kuwaita mashahidi kadhaa watakaosaidia katika utetezi wake. Hata hivyo, timu ya mawakili wa Gachagua haikufichua majina ya mashahidi hao. 


Baada ya ushahidi kuwasilishwa, maseneta watapata fursa ya kuuliza maswali na kupata ufafanuzi kutoka kwa Gachagua kabla ya kupewa muda wa saa moja kutoa mawasilisho yao ya mwisho.


Kwa upande mwingine, timu ya Bunge la Kitaifa, inayoongozwa na Mbunge wa Kibwezi Magharibi Mwengi Mutuse, itakuwa na muda sawa wa kuwasilisha kesi yao siku ya Jumatano, ambapo mashahidi kadhaa watakuwa wakiitwa kutetea hoja ya kumwondoa Naibu Rais madarakani.


Miongoni mwa mashahidi wa upande wa Bunge wanaotarajiwa kutoa ushahidi ni Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja, Katibu wa Baraza la Mawaziri Mercy Wanjau, na aliyekuwa Kaimu Afisa Mkuu Mtendaji wa KEMSA, Andrew Mulwa. 


Kikao cha kupiga kura kuamua hatma ya Gachagua kinatarajiwa kuanza saa moja unusu jioni siku ya Alhamisi.

0 Comments:

Post a Comment