BOT Yatangaza Kuondoa Noti za Zamani kwenye Mzunguko




Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imetoa taarifa rasmi kwa umma juu ya kuondolewa kwenye mzunguko kwa noti za shilingi za zamani zenye thamani ya shilingi ishirini (20), mia mbili (200), mia tano (500), elfu moja (1000), elfu mbili (2000), elfu tano (5000) na elfu kumi (10000) zilizotolewa kati ya mwaka 1985 hadi mwaka 2003. Pia, hatua hiyo inajumuisha noti ya shilingi mia tano (500) iliyotolewa mwaka 2010, ambazo zitaondolewa rasmi kulingana na Tangazo la Serikali Na. 858 lililotolewa Oktoba 11, 2024.



Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Gavana wa Benki Kuu, Emmanuel M. Tutuba, ubadilishaji wa noti hizo utaanza Januari 6, 2025 hadi Aprili 5, 2025. 


"Tunaomba wananchi wanaomiliki noti hizi za zamani wajitokeze kwa ajili ya kubadilisha au kuweka akiba katika benki yoyote ndani ya muda uliopangwa," alieleza Gavana Tutuba, akisisitiza umuhimu wa kutekeleza zoezi hilo kwa wakati.


Kuhusu utaratibu wa ubadilishaji, Gavana Tutuba alieleza kuwa wananchi wataweza kubadilisha noti hizo kupitia ofisi zote za Benki Kuu na katika benki za kibiashara kote nchini. 


"Tunataka wananchi wapatiwe malipo yenye thamani sawa na kiasi cha noti wanazowasilisha," aliongeza.


BoT imeonya kuwa kuanzia Aprili 6, 2025, noti hizi za zamani hazitakubalika tena kama fedha halali, na mtu yeyote au taasisi yoyote itakayomiliki fedha hizo haitaruhusiwa kuzitumia kwa malipo mahali popote duniani. 


Aidha, benki zote zitaacha kupokea au kulipa fedha hizo kama amana. 


Gavana Tutuba alihitimisha kwa kusema, "Wananchi ambao bado wanamiliki noti hizi wanashauriwa kuzibadilisha haraka iwezekanavyo."




0 Comments:

Post a Comment