Leo, jamii ya Wamasai wa Ngorongoro walikusanyika kwenye barabara kuu ya Ngorongoro-Serengeti kwa maandamano ya amani, wakidai heshima kwa haki zao za msingi ambazo wanadai zimepuuziliwa mbali na Serikali ya Tanzania kwa kipindi cha miaka minne iliyopita.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na wanajamii hao kwa vyombo vya habari leo, Agosti 18, 2024, wametaja kuwa wamekumbwa na vikwazo vya huduma za kijamii, unyanyasaji kutoka kwa serikali, ukiukwaji wa haki za ardhi, kunyimwa haki ya kujiandikisha kama wapiga kura, na kuhitajika kuwa na kadi za vibali kwenye ardhi yao wenyewe.
Walisema kuwa walilazimika kuchukua hatua hii baada ya majaribio mengi ya kuwasiliana na mamlaka kukosa mwitikio.
"Hatufungi barabara hii kwa hiari, tunafanya hivi kwa lazima," alisema mmoja wa washiriki wa maandamano asubuhi hii. "Kwa muda mrefu, sauti zetu zimepuuziliwa mbali, na haki zetu zimekanyagwa," aliongeza mwandamanaji mwingine.
"Hii ni hatua yetu ya mwisho kuvuta hisia kuhusu mateso yetu na kudai heshima na utu tunaostahili," alisisitiza mwandamanaji mwingine.
Jamii ya Wamasai inatoa wito kwa mamlaka kushiriki katika mazungumzo ya maana ili kushughulikia wasiwasi wao. Wanatoa pia wito kwa umma kuelewa hali ya Wamasai na kuunga mkono mapambano yao ya haki.
Wananchi hao wanadai kuwa katika kipindi cha miaka minne iliyopita, Serikali ya Tanzania imezuiya huduma zote za kijamii kama afya na elimu katika eneo la Ngorongoro kama njia ya kuwahamisha Wamasai.
Wamasai wanasisitiza kuwa maandamano yao ni ya amani na wanatumaini kwamba hatua ya leo italeta mabadiliko ya kimkakati kutoka kwa serikali.
Mwanazuoni maarufu, Profesa Issa Shivji, ametoa maoni kupitia ukurasa wake wa kijamii wa X, akisema, "Jamii ya Maasai waishio Ngorongoro inaelekea wanathibitiwa kwa kutokupewa huduma za kijamii na kuadhibiwa kwa kukosa majina yao katika daftari la kudumu la wapigakura. Hii kwa Kiingereza inaitwa disenfranchisement. Kitabu kilichoandikwa na Issa Shivji na Wilbert Kapinga mnamo 1996 kilionyesha kwamba Wamaasai waishio Ngorongoro hawana haki ya kuwa na serikali yao ya Mtaa na kuwa na uwakilishi katika vyombo vya utawala ngazi ya Wilaya kwa kuwa wanatawaliwa na Mamlaka ya Ngorongoro."
Profesa Shivji aliendelea kusema, "Sakata la Maasai wa Ngorongoro limekuwa mbaya zaidi na kuna hatari ya wao kukosa ardhi na makazi yao katika eneo la Ngorongoro, ardhi ambayo ni mali yao ya kiasili na mahali ambapo babu zao wamezikwa. Tukikubali upanuzi wa hifadhi kufanyikwa kwa nguvu na kwa gharama ya kumeza maliasili ya wote, tutakuwa tunakwenda kubaya. Tupaze sauti. Maliasili ni ya wote. Yasibinafsishwe kwa kisingizio chochote kile."
Kwa upande wake, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) imeeleza kwa umma kuwa shughuli za utalii katika hifadhi hiyo zinaendelea vizuri licha ya maandamano ya wananchi. Taarifa iliyosainiwa na Kaimu Meneja wa Kitengo cha Uhusiano kwa Umma, Hamis Dambaya, imefafanua kwamba watalii kutoka ndani na nje ya nchi wanaendelea na safari zao na Serikali inaendelea kuhakikisha usalama wao.
"Maandamano yaliyoripotiwa kupitia baadhi ya mitandao ya kijamii yanaidhihirishia dunia na jumuiya za kimataifa kwamba ndani ya Hifadhi hiyo hakuna ukiukwaji wa haki za binadamu na unyanyasaji wa wananchi. Mamlaka inawahakikishia watalii wote waliopanga safari za kuja Ngorongoro kuwa Serikali itaendelea kusimamia usalama wao wakati wote watakapokuwa ndani ya hifadhi," imeeleza taarifa hiyo.
No comments:
Post a Comment