Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amewahakikishia wananchi wa Tarafa ya Ngorongoro, Wilaya ya Ngorongoro kuwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba 2024 pamoja na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 utaendelea kama ilivyopangwa, huku mipaka ya vijiji na vitongoji ikizingatiwa kama ilivyokuwa awali.
Akizungumza kwa niaba ya Rais katika mkutano wa hadhara uliofanyika kijiji cha Oloirobi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), William Lukuvi, amewataka wananchi wa eneo hilo kuondoa hofu na kuendelea kuishi kwa amani. Alisisitiza kuwa Tanzania ni nchi ya amani inayoheshimu haki za binadamu na usawa.
Pia, Lukuvi alisema Rais Samia amesikiliza kero na malalamiko ya viongozi na vyombo vya habari kuhusu changamoto wanazokabiliana nazo wananchi wa eneo hilo, na amewaagiza askari wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kuacha unyanyasaji dhidi ya wananchi na kuheshimu mamlaka za serikali za vijiji na vitongoji.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Christian Makonda, aliwapongeza wananchi kwa uvumilivu na kuwaahidi kuwa serikali itahakikisha huduma za kijamii, hususan katika sekta ya afya na elimu, zinarejea katika hali bora na kwa viwango vinavyotakiwa.
Ziara hiyo iliwahusisha pia viongozi waandamizi akiwemo Waziri wa Katiba na Sheria, Prof. Palamagamba Kabudi, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Dunstan Kitandula, pamoja na Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Awadh Juma Haji.
No comments:
Post a Comment