PROF NDAKIDEMI AKAGUA MRADI WA UJENZI WA OFISI YA TARAFA YA HAI MASHARIKI NA KUONGEA NA WANANCHI.

  

Na Gift Mongi,Moshi


Ndio!ndio! Uwakilishi ni vitendo yaani vikiambatana na kusikiliza wale ambao unawawajibisha!hapa nina maana kubwa unatakiwa kujishusha na kujua unaowaongoza wapo katika hali ipi



Katika hili huenda likawa ni jambo la kawaida kwake  kwa mbunge wa jimbo La Moshi Vijijini Mkoani Kilimanjaro, Prof Patrick Ndakidemi ambaye  amefanya ziara ya kukagua mradi wa ujenzi wa ofisi ya Tarafa ya Hai Mashariki iliyopo katika  Kata ya Kimochi na kuongea na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya shule ya msingi Kisaseni.



Ofisi hiyo ya Tarafa ya Hai Mashariki imegharimu Shilingi milioni 90 na iko katika hatua za mwisho kukamilika.



Katika ziara hiyo Mbunge aliongozana na Katibu wa CCM wilaya  Ramadhani Mahanyu, Katibu wa Wazazi wilaya Cde Andrew Mwandu,  Ally Badi (Diwani wa Kata), Mwakilishi wa Mamlaka ya maji safi na maji taka (MUWSA), Flora Nguma, Mkurugenzi wa Chuo cha Afya cha Kumbukumbu ya Zawadi Mama Mrema na viongozi wa CCM na Serikali Kata ya Kimochi.



Akiongea katika mkutano wa hadhara, Diwani wa Kata hiyo Ally Badi alimshukuru sana Mbunge kwa ushirikiano mkubwa uliopo baina yao, jambo ambalo limewezesha Kata ya Kimochi kupata miradi ya maendeleo yenye thamani kubwa ya pesa.




Katika mkutano wa hadhara, Mbunge aliwasilisha utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi kwa kipindi cha miaka minne tokea aingie madarakani. 


Alieleza wananchi kuwa serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hasani imetoa shilingi bilioni 3,985,321,600.00 kutekeleza miradi ya maendeleo hapo Kimochi katika maeneo ya Elimu, Miundombinu ya Barabara, Maendeleo ya Jamii, Maji, Afya, Kilimo, Ujenzi wa Ofisi Mpya za Halmashauri ya Moshi  na ile ya Tarafa ya Hai Mashariki.


 Kati ya miradi mikubwa ya kielelezo ilinayotekelezwa ni ile ya ujenzi wa Jengo jipya na Halmashauri ya Moshi na ule wa maji unaohudumia wananchi wa vijiji vyote sita vya Kata ya Kimochi.



Katika mkutano huo, wananchi walipata fursa ya kumweleza Mbunge kero zao. Kero kubwa  ilikuwa ni Ubovu wa Barabara zote za Kata ya Kimochi na ukarabati wa barabara kwa kiwango cha chini kwani zimetumika changarawe zenye kiwango duni.



 Walilalamika kuwa TARURA wanatekeleza miradi bila kuwashirikisha wananchi. Kero ya pili ikiyolalamikiwa na wananchi wengi ni ukosefu wa maji katika vijiji vingi vya Kata ya Kimochi. 


Mbunge kwa kushirikiana na Diwani, walijibu kero zote  na kuchukua kero ambazo hazikuwa na majibu. Waliwahakikishia wananchi kuwa watazipeleka kwenye mamlaka husika ili zipate ufumbuzi. Mwisho wa mkutano Mbunge aligawa miche bora ya migomba.


Katibu wa CCM wilaya  Ramadhani Mahanyu aliwashukuru Rais Samia Suluhu Hassan, Mbunge na Diwani  kwa kazi kubwa waliyofanya ya kuwapa wananchi wa Kimochi  maendeleo katika nyanja mbalimbali. 


Aliwaomba watu wa Kimochi waendelee kuwaunga mkono Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mbunge Ndakidemi na Diwani Ally Badi kwani kazi walizofanya ni kubwa na zenye tija kwa Wananchi.  Cde Mahanyu aliwaasa vijana kuachana na tabia ya ulevi uliokithiri katika jamii.



0 Comments:

Post a Comment