Wednesday, August 7, 2024

KITANDULA ASISITIZA KASI ZAIDI KWA TANAPA KATIKA KUVUTIA WAWEKEZAJI

Na Edmund Salaho,Dodoma



Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, M Dunstan Kitandula (Mb) amelitaka Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kuongeza kasi zaidi katika kutangaza maeneo ya uwekezaji yanayopatikana katika Hifadhi za Taifa.


Kitandula ameyasema hayo leo alipotembelea banda la TANAPA lililopo ndani  ya banda la Wizara ya Maliasili na Utalii katika Maonesho ya NaneNane yanayoendelea katika viwanja vya Nzuguni jijini, Dodoma.


“Niwapongeze TANAPA mnafanya kazi kubwa katika kutunza na kutangaza vivutio vilivyopo katika Hifadhi, niwatake muongeze kasi katika kuvutia wawekezaji kupitia maonesho mbalimbali pamoja na kubainisha vigezo vinavyohitajika katika kila aina ya uwekezaji ili kuweza kuvutia wawekezaji zaidi katika maeneo hayo “ alisema Kitandula


Naye, Afisa Uhifadhi Mkuu, Alex Choya Choya kutoka Ofisi ya TANAPA Dodoma alibainisha mikakati inayofanywa na Shirika katika kuvutia wawekezaji katika maeneo ya Hifadhi za Taifa kwa kufanya kampeni kubwa za ndani na nje ya nchi zenye lengo la  kutangaza fursa za uwekezaji kupitia maonesho ya Kitaifa na Kimataifa pamoja na vyombo mbalimbali vya habari.


TANAPA imeendelea  kutoa elimu ya Uhifadhi, Utalii pamoja na kutangaza fursa za Uwekezaji zinazopatika katika maeneo ya Hifadhi za Taifa kupitia maonesho ya Nane Nane yanayoendelea jijini, Dodoma.

No comments:

Post a Comment