Mwenyekiti wa Halmashauri ya Arusha, Dkt. Ujungu Salekwa, amewataka wananchi wa halmashauri hiyo kuwa na amani huku akiwahakikishia kuwa zaidi ya shilingi milioni 600 zilizokuwa zimepotea zimesharudi zote.
Akiongea na waandishi wa habari Agosti 7, 2024, baada ya kumalizika kwa kikao cha baraza la madiwani, Dkt. Salekwa alieleza kuwa fedha hizo zilipotea kwenye baadhi ya taasisi za kifedha na watumishi wawili wa halmashauri, lakini baada ya uchunguzi, taasisi hizo zilijiridhisha na kurejesha fedha zote.
"Mimi kama mwenyekiti wa halmashauri niseme kuwa fedha hizo zilipotea kwenye baadhi ya taasisi za kifedha na watumishi wawili wa halmashauri na taasisi hizo baada ya kujiridhisha kuna makosa yalifanyika kwa upande wao walisharudisha fedha hizo zote zimesharudi na moja kwa moja zitaenda kwenye vituo vya afya na zahanati ambazo upotevu huo ulitokea," alisema Dkt. Salekwa.
Kwenye kikao hicho, madiwani walijadili pia suala la taarifa zilizokuwa zikizagaa kuwa halmashauri hiyo ilikuwa na bakaa ya shilingi bilioni 8.5. Akifafanua kuhusu suala hilo, Dkt. Salekwa alisema, "Taarifa sahihi mpaka tunafika mwisho wa mwaka Juni 2024, fedha ambazo zilikuwa hazijatumika ni kama bilioni 2.7 ambazo zilikuwa na maelezo kwani zilikuwa ni za miradi mikubwa iliyokuwa inaendelea na haijakamilika kama Olturmet wenye zaidi ya shilingi milioni 900 na shule kama Engalaon."
Aidha, Dkt. Salekwa aliwapongeza madiwani kwa kuendelea kutekeleza wajibu wao wa kusimamia fedha zinazoletwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo kama ujenzi wa nyumba za walimu na madarasa
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Emmanuela Kaganda, akiongea na madiwani hao, aliwakumbusha kuwa uchaguzi wa serikali za mitaa unakaribia, hivyo wanapaswa kutoa elimu kwa wananchi ili wajitokeze kwa wingi wakati wa kujiandikisha na kupiga kura kuchagua wenyeviti wa vijiji.
Kaganda aliendelea kwa kusema, "Rais wa awamu ya sita, Samia Suluhu Hassan, ametuma fedha nyingi za miradi ya maendeleo, hivyo ni jukumu la madiwani kuzisimamia kwa umakini zaidi ili miradi hiyo itekelezwe kwa ubora na ikamilike kwa wakati."
Kuhusu usimamizi wa miradi, Kaganda aliwaasa madiwani kwenda kwa wananchi na kuwaeleza miradi inayotekelezwa na serikali. "Ni wajibu wa madiwani kwenda kwa wananchi kuwaeleza miradi inayotekelezwa na serikali na wao kama wenyeviti wa kamati za maendeleo ya kata wakasimamie kuhakikisha watendaji na wenyeviti wa vijiji na vitongoji waeleze wananchi miradi inayotekelezwa ili ikamilike kwa ukamifu na kwa wakati," alisisitiza.
No comments:
Post a Comment