Ushindi wa Keir Starmer na Changamoto za Kuongoza Chama cha Labour
Keir Starmer aliliongoza Chama cha Labour kwenye ushindi mkubwa, akilivusha chama hicho "katika enzi mpya za kujiamini na matumaini." Hata hivyo, kulikuwa na changamoto njiani.
Mwaka 2021, Conservative walichukua kiti cha jimbo la Hartlepool kutoka Labour, mji wa kaskazini-mashariki mwa Uingereza ambao haujawahi kuwa na Mbunge wa Conservative.
Tukio hilo lilikuwa pigo kubwa kwa juhudi za Starmer za kupata uungwaji mkono katika ngome za muda mrefu za chama cha Labour.
Matokeo yalikuwa mabaya kiasi kwamba, kiongozi huyo aliwaambia wafanyakazi wake kuwa anajiuzulu kwa sababu kilichotokea kilionyesha chama kinarudi nyuma na alijiona yeye ndiye anayekataliwa.
Hakujiuzulu, lakini kilichotokea kilimsukuma kufikiria tena kuhusu sera na kupanga upya timu yake ya uongozi.
Lengo lilikuwa ni kuwarudishia wapiga kura wa chama cha Labour waliokwenda kwa mhafidhina Boris Johnson katika ngome za zamani za Labour - zinazojulikana kama Red Wall.
Marekebisho ya ndani yalifanyika. Starmer alimsimamisha kazi mtangulizi wake, Jeremy Corbyn, wakati uchunguzi kuhusu chuki dhidi ya Wayahudi ndani ya chama ulipofanyika.
Hilo lilimaanisha Corbyn hakuweza kusimama kama mgombeaji wa Ubunge wa chama cha Labour katika uchaguzi huu, lakini alisimama kama mgombea huru na akashinda.
Wanasiasa wengine wa chama cha Labour pia wanasema wamezuiwa kugombea na kumtuhumu Starmer kujaribu kuwaondoa watu wa mrengo wa kushoto katika chama. Vilevile, wanamtuhumu kushirikiana na mwanachama wa muda mrefu wa chama cha Labour, Waziri Mkuu wa zamani Tony Blair.
Starmer alijaribu kuziondoa hofu za Waingereza kwa kusema Labour haitaingia kwenye matumizi yasiyo ya lazima. Mwezi Februari, aliitupilia mbali moja ya ahadi zake kubwa kuhusu matumizi ya pauni bilioni 28 (dola bilioni 35) kwa mwaka katika sera rafiki na mazingira.
Hilo limechangia kuwa na mvuto kwa wapiga kura wengi, lakini pia wapiga kura wengine wanamuona kama mwanasiasa asiye madhubuti.
Siku zijazo, Uingereza itajifunza mambo mengine kuhusu mwanasiasa huyu wa chama cha Labour atakapohamia 10 Downing Street, ofisi ya Waziri Mkuu wa Uingereza.
No comments:
Post a Comment