Rais wa Kenya, William Ruto, ameagiza mamlaka husika kuharakisha uchunguzi kuhusu miili iliyokuwa imefungwa kwenye mifuko ya plastiki na kutupwa jalalani katika mtaa wa Mukuru kwa Njenga, jijini Nairobi.
Rais Ruto ametoa ahadi kwa umma kuwa wale waliohusika na kitendo hiki cha kinyama watakamatwa na kushtakiwa haraka iwezekanavyo.
Taarifa za awali zinaonyesha kuwa miili tisa imepatikana, ingawa wakazi wa Mukuru kwa Njenga wanadai kuwa idadi hii ni kubwa zaidi, wakiarifu kwamba miili mitano zaidi ilipatikana Jumamosi asubuhi.
Kwa mujibu wa ripoti ya uchunguzi wa awali, waathiriwa wote ni wanawake na waliuawa kwa njia sawa.
Rais Ruto, akizungumza kuhusu suala hili, alisema, "Kule Nairobi, kumepatikana miili ya Wakenya, imefika karibu tisa. Karibu wote ni wasichana na tunafanya uchunguzi.
Nimeamrisha polisi na wale wote wanaohusika kwa mambo ya homicide. Nawahakikisha Wakenya, wale wote waliohusika na vifo vya Kware watachukuliwa hatua."
Eneo la tukio limefungwa wakati polisi wakiendelea na uchunguzi na kutafuta miili zaidi. Tukio hili limeleta mshtuko na huzuni kwa jamii na nchi kwa ujumla, huku umma ukisubiri kwa hamu matokeo ya uchunguzi na hatua kali kwa wahusika.
Haya yanajiri siku moja tu baada ya mkuu wa polisi nchini Kenya kujiuzulu kufuatia maandamano ya kupinga nyongeza ya kodi, ambayo yalisababisha vifo vya zaidi ya watu 40.
Hali hii inaongeza changamoto kwa serikali ya Rais Ruto katika kudhibiti usalama na kurejesha amani nchini.
No comments:
Post a Comment