Lissu Atangaza Kugombea Urais 2025, Hakuna Mvutano na Mbowe




Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Tanzania Bara, Tundu Lissu, amesema atagombea nafasi ya Rais wa Tanzania katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka 2025, huku akibainisha kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ndiye anayeweza kuwa mpinzani wake mkuu.


Lissu alisisitiza kwamba hana tofauti zozote na Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, na kuongeza kuwa hana dhamira yoyote ya kuwania nafasi ya Mwenyekiti wa chama hicho Taifa katika uchaguzi wa ndani unaoendelea.


Akizungumza na wanahabari Ijumaa, Julai 26, 2024, katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA), muda mfupi baada ya kuwasili nchini akitokea mapumzikoni nje ya nchi, Lissu alisema ana dhamira ya kurejea kwenye kinyang'anyiro hicho baada ya kugombea kwa mara ya kwanza kwenye uchaguzi mkuu uliopita wa mwaka 2020, ambapo mpinzani wake mkuu alikuwa Hayati Dkt. John Pombe Magufuli (CCM).


Kuhusu joto la kisiasa kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu (2024) na uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, Lissu alieleza utayari wa CHADEMA kusimamisha wagombea na kuwaombea ridhaa kwa wananchi wakati utakapowadia. Hata hivyo, alitoa tahadhari kwa mamlaka mbalimbali zinazosimamia chaguzi hizo kutambua kuwa chama hicho hakitakubali kushuhudia vitendo vya ukiukwaji wa taratibu vilivyotokea kwenye chaguzi zilizopita.


Kuhusiana na madai ya mvutano ndani ya CHADEMA yanayomhusisha yeye na Freeman Mbowe, Lissu alisema hakuna mvutano au mgogoro wowote kati yao na amewahi kufafanua mara kadhaa kuwa hana dhamira ya kuwania nafasi ya Mwenyekiti wa chama hicho Taifa.


Pia, Lissu alizungumzia tuhuma zinazotolewa na aliyekuwa kada wa chama hicho aliyehamia CCM hivi karibuni, Mchungaji Peter Msigwa, kuhusu matumizi ya raslimali fedha na utawala bora ndani ya CHADEMA. Lissu alisema ni jambo la kawaida kwa kiongozi mwandamizi anapohama kutoa tuhuma, lakini alikiri kuwa ni vyema ofisi ya Katibu Mkuu wa CHADEMA kutoa majibu ya kila hoja ili kuondoa sintofahamu miongoni mwa wanachama na Watanzania kwa ujumla.

0 Comments:

Post a Comment