Kiongozi wa Hamas, Ismail Haniyeh, aliuawa mjini Tehran, Iran, siku ya Jumatano, kwa mujibu wa taarifa kutoka Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi la Iran. Hamas imelaumu Israel kwa shambulio hilo la kuua.
Kwa mujibu wa taarifa, Haniyeh aliuawa baada ya kushiriki katika hafla ya kuapishwa kwa rais mpya wa Iran.
Israel imekataa kutoa maelezo kuhusu kifo hicho, huku ikijua kwamba mara nyingi haithibitishi au kukataa ripoti zinazohusiana na mauaji yanayotekelezwa na shirika lake la kijasusi, Mossad.
Hamas ilithibitisha kifo cha Haniyeh na kusema kuwa kiongozi huyo alikufa kama shahidi kwa ajili ya Palestina.
Katika taarifa yake, Hamas imemnukuu Haniyeh akisema kuwa kadhia ya Palestina ina "gharama" na kwamba wanajiandaa kwa gharama hiyo, ikiwa ni pamoja na kuuwawa kama shahidi kwa ajili ya Palestina na Mwenyezi Mungu.
IRAN KUCHUNGUZA KIFO CHA HANIYEH
Jeshi la Ulinzi la Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC) limetoa rambirambi zake kufuatia kifo cha Ismail Haniyeh mjini Tehran.
Taarifa iliyotolewa na chombo chake cha habari cha Sepah news ilisema inachunguza "sababu na ukubwa wa tukio" na itatangaza ilichobaini baadaye.
Iliongeza kuwa Haniyeh na mmoja wa walinzi wake "waliuawa".
IRGC ni kikosi kikubwa cha kijeshi, kisiasa na kiuchumi nchini Iran, chenye uhusiano wa karibu na kiongozi mkuu, Ayatollah Ali Khamenei.
HANIYEH NI NANI
Haniyeh, 62, alikuwa mwanachama mashuhuri wa vuguvugu la Hamas mwishoni mwa miaka ya 1980.
Israel ilimfunga Haniyeh kwa miaka mitatu mwaka 1989 huku ikikabiliana na uasi wa kwanza wa Wapalestina.
Kisha alihamishwa mwaka 1992 hadi ardhi isiyomilikiwa na nchi yoyote kati ya Israel na Lebanon, pamoja na baadhi ya viongozi wa Hamas.
Haniyeh aliteuliwa kuwa waziri mkuu wa Palestina mwaka 2006 na Rais Mahmoud Abbas baada ya Hamas kushinda viti vingi zaidi katika uchaguzi wa kitaifa, lakini alifutwa mwaka mmoja baadaye baada ya kundi hilo kukiondoa chama cha Fatah cha Bw Abbas kutoka Ukanda wa Gaza katika wiki moja ya ghasia .
Haniyeh alikataa kuondolewa kwake kama "kinyume cha katiba", akisisitiza kwamba serikali yake "haitaacha majukumu yake ya kitaifa kwa watu wa Palestina", na kuendelea kutawala huko Gaza.
Alichaguliwa kuwa mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Hamas mnamo 2017.
Mnamo 2018, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilimtaja Haniyeh kuwa gaidi . Amekuwa akiishi Qatar kwa miaka kadhaa iliyopita.
0 Comments:
Post a Comment