Utoro wa Mawaziri wasababisha Bunge la Afrika Mashariki Kuahirishwa
Bunge la Afrika Mashariki limeshindwa kuendelea na kikao chake baada ya mawaziri wanaohusika na Jumuiya kutoka nchi wanachama kutohudhuria bungeni.
Hali hiyo ilisababisha wabunge kuomba muongozo wa Spika juu ya kutokuwepo kwa mawaziri hao wakati bunge lilitakiwa kujadili Taarifa ya Kamati ya Madhumuni ya Jumla ya Makadirio ya Ziada ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha wa 2023/2024.
Mbunge wa EALA kutoka Uganda, Rose Akol, alimuomba Spika kwa nafasi hiyo ili alete suala la kikanuni, akisema, "Mchana huu tulipaswa kujadili bajeti ya ziada na kisha tuendelee na kupanga bajeti. Lakini kama tunavyoona hapa, hatuna mtu yeyote kwenye benchi la mbele ili kusimamia na kutekeleza majukumu yao kuhusu bajeti tunazozijadili."
Mbunge wa EALA kutoka Tanzania, Abdullah Makame, aliongeza kuwa, "Hali hii ni mbaya zaidi kwani hata CTC hayupo. Katika nyakati zingine, CTC angekuwa hapa lakini sasa hata yeye hayupo."
Baada ya kusikiliza hoja hizo, Spika Joseph Ntakirutimana aliahirisha bunge kwa dakika 15 ili kutoa nafasi endapo mawaziri hao wanaweza kufika bungeni. Hata hivyo, baada ya bunge kurejea, Spika alisema, "Benchi la mbele bado liko wazi. Hakuna mtu na ni vigumu kuendelea na shughuli zetu leo. Kamati inahitaji muda zaidi kuzungumza na baraza, wanachama wa baraza na idara. Kwa sababu hii, naahirisha bunge hili hadi kesho saa 8:30 mchana."
Awali, Mbunge Dr. Abdullah Makame alisema, "Tuna kipengele kinachosubiri kujadiliwa kwa mwaka wa fedha 2023/2024. Mpaka tukamilishe kipengele hicho, hatuwezi kuendelea na mambo ya mwaka wa fedha 2024/2025. Napendekeza tusiingilie mambo ya 2024/2025 mpaka tumalize masuala ya 2023/2024."
Kwa hivyo, bunge lililazimika kuahirishwa hadi kesho ili kutoa muda kwa mawaziri husika kuhudhuria na kushiriki katika mijadala muhimu ya bajeti.
No comments:
Post a Comment