Muleba, Kagera - Tukio la kusikitisha na la kulaaniwa lilitokea Mei 30, 2024 majira ya saa mbili usiku katika kijiji cha Bulamula Wilaya ya Muleba mkoani Kagera, ambapo mtoto mwenye umri wa miaka miwili na nusu mwenye ualbino, aitwaye Asimwe Novart, aliporwa na watu wasiojulikana kutoka kwa mama yake mzazi.
Mtoto huyo alipatikana akiwa ameuawa kikatili mnamo Juni 17, 2024 majira ya saa sita mchana, kwa kukatwa baadhi ya viungo vyake na kufungwa kwenye mfuko kisha kutupwa kwenye kalavati linalopitisha maji katika barabara itokayo Luhanga kwenda kijiji cha Makongora.
Baada ya tukio hilo, Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na raia wema wanaochukia vitendo vya kinyama, walianza msako mkali kuanzia Mei 31, 2024 hadi usiku wa kuamkia Juni 19, 2024. Katika msako huo, watuhumiwa tisa walikamatwa wakiwa na viungo vinavyodhaniwa ni vya mtoto Asimwe Novart, wakiwa wamehifadhi katika vifungashio vya plastiki wakitafuta mteja.
Watuhumiwa waliokamatwa walieleza jinsi walivyoshiriki katika tukio hili na ni pamoja na baba mzazi wa mtoto huyo, Novart Venant; Desideli Evarist ambaye ni mganga wa jadi mkazi wa Nyakahama; na Elipidius Rwegoshora, Paroko Msaidizi wa Parokia ya Bugandika. Inadaiwa kuwa Paroko huyo alimshawishi baba mzazi wa mtoto ili wafanye biashara ya viungo vya binadamu, na pia ndiye aliyemtafuta mganga wa jadi na kulipia gharama zote za uganga.
Watuhumiwa wengine ni Dastan Kaiza, mkazi wa Bushagara; Faswiru Athuman, mkazi wa Nyakahama; Gozibert Aikadi, mkazi wa Nyakahama Kamachumu; Rwenyagira Burkadi, mkazi wa Nyakahama Kamachumu; Ramadhani Selestine, mkazi wa Kamachumu; na Nurduni Hamada, mkazi wa Kamachumu.
Msemaji wa Jeshi la Polisi, David A. Misime - DCP, alisema, "Jeshi la Polisi linatoa onyo kali kwa watu wanaoendekeza imani za kishirikina, ikiwa ni pamoja na kupiga ramli chonganishi wakiaminishana kwamba wanaweza kupata utajiri kwa njia za kishirikina. Wanapaswa kuacha tabia hizo mara moja kwani hakuna utajiri unaopatikana kwa kumiliki viungo vya binadamu mwenye ualbino. Familia zenye watoto au ndugu wenye ualbino zingeweza kuwa tajiri sana kama ingekuwa hivyo, lakini badala yake wanaishi maisha ya kawaida kama sisi wengine."
Aliendelea kusema, "Vitendo hivi ni uhalifu uliopitiliza na ushamba katika karne hii ya maendeleo ya sayansi na teknolojia. Yeyote anayeshiriki katika uhalifu wa aina hiyo lazima atakamatwa, kwani vitendo hivyo havina baraka za Mwenyezi Mungu wala za sheria za nchi. Watu wenye mawazo hayo wanapaswa kuacha na kufanya kazi halali, kutafuta mafanikio kwa njia sahihi na kuacha kuendekeza ushirikina."
0 Comments:
Post a Comment