Mtoto Mwenye Ualbino Apatikana Amefariki Katika Tukio la Kusikitisha Muleba

 Mtoto Mwenye Ualbino Apatikana Amefariki Katika Tukio la Kusikitisha Muleba



Mtoto mwenye ualbino, Asimwe Novath, aliyekuwa na miaka miwili na miezi sita, mkazi wa Kitongoji cha Mbale, Kijiji cha Bulamula, kata ya Kamachumu wilaya ya Muleba mkoani Kagera, amekutwa amefariki huku mwili wake ukiwa umefungwa kwenye mfuko (Sandarusi) na kukosa baadhi ya viungo.



Akizungumza kuhusu tukio hilo, Katibu Tawala wa Wilaya ya Muleba, Benjamin Mwikasyege, amesema kuwa mwili wa mtoto huyo umekutwa umetelekezwa kwenye karavati lenye maji katika barabara ya Makongora, Kijiji cha Malele. 



Aidha, Mwikasyege ameongeza kuwa mwili wa marehemu umechukuliwa kwa ajili ya uchunguzi zaidi na ameomba wananchi kutoa ushirikiano ili kubaini waliohusika na tukio hili la kikatili.



Asimwe Novath aliibwa nyumbani kwao Mei 30 mwaka huu, baada ya mama yake kukabwa na watu wasiojulikana usiku wa saa 2:30 na kisha mtoto huyo kuchukuliwa. 


Mtoto huyo amekuwa akitafutwa kwa siku kadhaa hadi mwili wake ulipopatikana leo Juni 17, 2024, katika Kijiji cha Malele, kata ya Ruhanga, wilaya ya Muleba, mkoani Kagera.

0 Comments:

Post a Comment