![]() |
Wakili wa Utetezi Jebra Kambole akiongea na washitakiwa mara baada ya kesi kuahirishwa |
SHUGHULI za maendeleo zinakwama kwenye tarafa
ya Loliondo kutokana na zaidi ya nusu ya madiwani wanaowakilisha wananchi
kwenye baraza la madiwani wilayani Ngorongoro kushikiliwa kwa zaidi ya miezi
mitatu kwa kesi ya mauaji ya polisi, mwenye namba G 4200 Koplo Garlus Mwita huku
upelelezi wa shauri hilo ukiwa haujakamilika.
Aidha, mahakama ya hakimu Makazi Arusha
imeutaka upande wa jamhuri kuharakisha upelelezi wa shauri hilo huku ikiwataka
mawakili wa utetezi kufuata taratibu ili mshitakiwa wa 18 anayehitaji kutolewa
chuma kwenye mguu na 19 anayesumbuliwa na ugonjwa wa sukari wapatiwe matibabu.
Hayo yameelezwa leo Agosti 17, 2022 mbele ya
Hakimu Mkazi, Herieth Mhenga anayesikiliza shauri hilo la mauaji namba 11/2022
linalofika mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwa likisubiri upelelezi ukamilike
ili likasikilizwe Mahakama Kuu.
Wakili, William Ernest anayeongoza jopo la mawakili nane kuwatetea washitakiwa wote 24 aliieleza mahakama hiyo kuwa hatua ya washitakiwa hao kushikiliwa mbali ya kumkwamisha shughuli za umma lakini inawagharimu wananchi wao wanaokuja Arusha kwa ajili ya kufuatilia kesi hiyo.
Kwenye shauri hilo jumla ya madiwani 10 wa kata na viti maalum wanashikiliwa akiwemo Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi, (CCM) wilayani Ngorongoro, Ndirango SEnge Laizer.
“Tunayo rai upelelezi ukamilike kwa haraka, zaidi ya nusu ya washitakiwa hawa ni madiwani, ni wawakilishi wa wananchi hivyo kwa kipindi chote walichoshikiliwa shughuli za kimaendeleo zinakwama kwa sababu wao hawapo kwa ajili ya kuongoza shughuli za kimaendeleo,” alieleza Wakili William na kuongeza
…Wananchi ambao wanawaongoza kama unavyowaona wanatumia gharama nyingi kufika mahakamani hapa na wanakuja kwenye kesi badala ya kufanya shughuli za maendeleo,”.
Hoja hiyo iliungwa mkono na wakili wa utetezi, Yonas Masiaya ambaye alieleza kuwa zaidi ya robo tatu ya viongozi wa tarafa ya Loliondo wanashikiliwa hivyo hawashiriki vikao vinavyoamua maamuzi ya shughuli za miradi ya maendeleo
“Ili hatma ipatikane ni upelelezi kukamilika na upande jamhuri kila mara wanasema upelelezi haujakamilika licha ya mahakama yako tukufu kutoa uamuzi mdogo ikiwataka waharakishe upelelezi,” alieleza Siaya na kuongeza
… Mshitakiwa wa 16 ana chuma mguuni imefika wakati wa kutolewa ni hatari kuendelea kukaa nayo ... mshitakiwa wa 18 ana mtoto mdogo aliyemzaa kwa upasuaji na mshitakiwa wa 19 ana kisukari
Kutokana na hawa wagonjwa upande wa jamhuri wanapaswa kuharakisha upelelezi,”.
“Haki iliyocheleweshwa ni haki iliyopote wakamilishe upelelezi ili watuhumiwa waweze kusikilizwa kwa mujibu wa sheria,”.
Wakili mwingine wa Utetezi, Paul Kisabo alieleza kuwa kifungu 10 cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai kimeelezea kuhakikisha upelelezi unakamilika kwa wakati.
“Lakini pia mheshimiwa Agosti 5, 2022 mahakama hii ilitoa uamuzi mdogo ukisisitiza upande wa jamhuri kukamilisha upelelezi kwa wakati uamuzi wa mahakama unapaswa kuheshimiwa na kuna maamuzi ya mahakama za juu unaelekeza maamuzi ya mahakama kuheshimi hivyo tunaiomba mahakama iuagize upoande wa jamhuri kukamilisha upelelezi kwa wakati ili haki iweze kutendeka,” alieleza Wakili Kisabo na kuongeza.
…Lakini pia ili kuonyesha mahakama inaheshimiwa inabidi uamuzi wako uheshimiwe na utekelezwa,”.
Wakili mwingine wa utetezi, Jebra Kambole alirejea katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 Ibara ya 13 ibara ndogo 6 (b ) 1977 kama ilivyorekebishwa mara kadhaa kuwa watuhumiwa inaaminiwa hawajatenda kosa mpaka pale watakapohukumiwa na mahakama.
“Hawa watuhumiwa tunaamini/ tunadhani mpaka sasa hawajatenda kosa tunapaswa kuongozwa hivyo lakini tunaenda huu mwezi wa tatu sasa wako ndani,” alieleza wakili Kambole na kuongeza.
…Mamlaka ya mwendesha mashitaka wa serikali kwa mujibu wa sheria inamtaka kutenda haki kwa wakati na azingatie maslahi ya umma ambapo umma unatamani kuona ambaye ametenda kosa anakuwa ndani na ambaye hajatenda kosa anakuwa nje umma haupendi kuona ambaye hajatenda kosa anakuwa ndani,”.
“Mahakama nayo haipaswi kuchelesha haki bila sababu za msingi. Sababu tunaambiwa upelelezi haujakamilika ni vema tuambiwe upelelezi umefikia wapi na nini kinachelewesha ili wanaoenda mahabusu wajue nini kinachelewesha kesi yao kusikilizwa, na upelelezi ni vielelezo na mashahidi,” .
Akijibu hoja hizo wakili wa Serikali, Upendo Shemkole alieleza kuwa amesikia hoja zote za mawakili wasomi ikiwemo malalamiko ya washitakiwa 16, 19 na 18
“Nimesikia malalamiko yao ya kisheria yote ya nimeyasikia na nimeyachukua kama nilivyosema awali tunasisitiza upelelezi ufanyike kwa wakati,” alieleza Shemkole.
Kisha aliomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa kwa shauri hilo ili waone jitihada za kukamilisha upelelezi wa shauri hilo zitafikia wapi mpaka tarehe nyingine itakayopangwa.
Akiahirisha shauri hilo mpaka Agosti 30, mwaka huu litakaporudi mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwa, hakimu Mhenga aliamsisitiza mwendesha mashitaka alipeleke kwa viongozi wake suala la kuharakishwa kwa upelelezi kama ilivyoelekezwa na mahakama.
“Upelelezi wake ufanyike upesi kama ilivyoelezwa kuna washitakiwa wengine wanahitaji ‘medical attention’ wakamilishe upelelezi ili tuondoe malalmiko na sintofahamu ili hawa watu wakasikilizwe mahakama kuu,” alieleza Hakimu Mkazi Mhenga na kuongeza.
Askari Magereza huyo alieleza mahakamani hapo kuwa wana madaktari wao ambao wanawahudumia wagonjwa walio gerezani na wakiona kuna mgonjwa anahitaji matibabu zaidi hutoa kibali akatibiwe kwenye hospitali za serikali.
Baada ya maelezo hayo hakimu waliwaagiza mawakili wa utetezi kufuata taratibu za kuwezesha wagonjwa hao kupatiwa matibabu.
“Kusema huyu anahitaji hiki na hiki tu hapa mahakamani haitoshi, mtu huyo akatibiwe,” alisisitiza Hakimu Mhenga.
Washitakiwa
kwenye shauri hilo ni pamoja na Molongo Paschal, Albert Selembo, Lekayoko
Parmwati, (21) Sapati Parmwati, (30) Ingoi Olkedenyi Kanjwel, (20) Sangau
Morongeti, (Morijoi Parmati, (20) Morongeti Meeki, (Kambatai Lulu,(40) na
Moloimet Yohana,(37)?
Wengine ni
Ndirango Senge Laizer, (52) Joel Clemes Lessonu, (54) Simon Nairiam
Orosikiria, (59) Damian Rago Laiza, Mathew Eliakimu, (41) Luka Kursas,
(49) Taleng'o Twambei Leshoko, (37) Kijoolu Kakeya, (56)
Shengena Killel, (34) Kelvin Shaso Nairoti, (33) , Wilsom Tiuwa Kiling,
(32), James Mumes Taki (28), Simon Saitoti, (41), na Joseph Lukumay
Awali Julai 14, mwaka huu Wakili wa Serikali
Shemkole aliwasomea upya washitakiwa hao makosa yao ambapo alidai kuwa kuwa
kosa la kwanza ni kula njama ya mauaji ambalo linawakabili washitakiwa
wote ambapo wanadaiwa katika tarehe na sehemu isiyofahamika walipanga njama ya
kuua maafisa wa serikali na polisi waliokuwa wakishiriki kuweka mipaka
kwenye Pori Tengefu la Loliondo.
Katika shitaka la pili la mauaji wakili huyo
wa serikali alidai kuwa mnamo tarehe 10 Juni 2022 katika eneo la
Ololosokwan wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha kwa nia ovu washitakiwa hao
walisababisha kifo cha askari polisi mwenye namba G 4200 Koplo Garnus Mwita.
Washitakiwa hao wamerejeshwa mahabusu kwenye
gereza la mkoa la Kisongo kwani shauri linalowakabili halina dhamana.
0 Comments:
Post a Comment