RUSHWA ya ngono kwenye vyuo vikuu limekuwa ni tatizo sugu linalolalamikiwa kwa muda mrefu likidaiwa kuchangia kuwaathiri zaidi vijana wa kike ukilinganisha na wa kiume.
Aidha mbali ya athari za moja kwa moja kuonekana kwa mtoto wa kike lakini imeelezwa kuwa Taifa linaathirika zaidi kwa kupata wataalam wasio na uwezo unaotakiwa kwani mhitimu wa rushwa ya ngono kichwani hana ujuzi unaoonekana kwenye vyeti vyake hivyo ni mzigo kwa Taifa.
Imedaiwa kuwa kiini cha tatizo la rushwa ya ngono vyuo vikuu ni mmomonyoko wa maadili kwenye jamii ambayo tiba yake inaweza kupatikana kwa somo la maadili kufundishwa kuanzia shule za awali.
Mwaka 2020 Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini, (TAKUKURU) ilifanya utafiti wake kwenye vyuo vikuu viwili vya umma kile cha Dar es Salaam, (UDSM) na Dodoma, (UDOM).
Utafiti huo ulibaini chanzo cha rushwa ya ngono vyuoni ni ukosefu wa maadili, ushawishi wa walio kwenye mamlaka, mfumo wa utoaji taarifa kutokuwa rafiki, mfumo dhaifu wa kushughulikia rushwa ya ngono na mamlaka ya kutoa alama za mitihani kuachwa chini ya waalimu pekee.
Kwa kuona ukubwa wa tatizo hilo wiki iliyopita Shirika la Usaidizi wa Ustawi wa Wanawake na watoto, (WOCWELS) limezinduzi wa kampeni ya kuzuia na kupambana na rushwa ya ngono na kijinsia kwenye taasisi za elimu ya juu mkoani Arusha.
Mkurugenzi wa shirika hilo, Mary Mushi anasema kuwa lengo la kampeni hiyo ni kukuza uelewa na kujengea uwezo wa wanafunzi wa taasisi ya elimu ya juu kuhusu kukabiliana, kufuatilia na kuripoti taarifa za ukatili wa kijinsia ikiwemo rushwa ya ngono.
Anasema kuwa kampeni hiyo itafanyika kwenye vyuo vyote mkoani Arusha ambapo kwenye uzinduzi huo walihusisha wanachuo 50 kutoka vyuo vitatu vya Radio Habari Maalum,(HMC) Chuo cha Waandishi wa Habari cha Fanikiwa na Chuo cha Maendeleo ya Jamii Tengeru, (TICD) ambao wamewezeshwa kuanzisha, uendeshaji na ufuatuliaji wa dawati la jinsia.
“ Tunachotaka kukifanya kama tukijua tatizo rushwa ya ngono vyuoni linapoanzia na viashiria vyake tutaenda kuachana na hizo tabia lakini tutaenda kuwaelimisha na wale ambao hawapo hapa ndani naamini mtaenda kuwa mabalozi kufikisha ujumbe huu tuwafunze na njia tutakayoitumia kufikisha taarifa hizi kupitia mitandao ya jamii,” anasema Mushi.
Uzinduzi huo uliofanyika kwenye chuo cha HMC kilichopo Ngaramtoni wilayani Arumeru pia ulishirikisha wataalam kutoa ofisi za Mwanasheria Mkuu wa Serikali, (AG), Mkurugenzi wa Mashitaka nchini, (DPP), wanasheria wa kujitegemea, wanahakati wa haki za binadamu na waandishi wa habari.
Mambo mengi yaliibuka wakati wa mdahalo wa wazi juu ya suala la rushwa ya ngono namna inavyodaiwa kushamiri kwenye vyuo vikuu hapa nchini huku chanzo kikuu kikionekana ni mmomonyoko wa maadili kwenye jamii ambayo tiba yake inaweza kupatikana kwa somo la maadili kufundishwa kuanzia shule za awali.
Kwenye mdahao washiriki walidai kuwa japo kumekuwa na ugumu wa kukusanya ushahidi wa rushwa ya ngono lakini pia rushwa ya fedha inasababisha kukwamisha mchakato wa uchunguzi na kushitaki.
Hivyo walitaka kuwe na sheria ya kuwabana polisi, mawakili na mahakimu ambao wanapokea rushwa ili kusababisha haki isipatikane kwani polisi akipokea rushwa asikusanye ushahidi, wakili wa serikali akipokea rushwa akaacha kumtetea ipasavyo mhanga wa unyanyasaji wa kingono au hakimu anayeamua kwa uonevu , hivyo suluhisho ni kuwe na sheria mbadala ya kumtetea muathirika.
Domina Mboya ambaye ni Muadili (dean) wa TIDC anashauria suala la maadili liwekewe kwenye mtaala wa kufundishia kwa kuwa watoto wanaka muda mrefu shuleni kuliko wanapokuwa nyumbani
“Watoto hata tukiwaambia kitu nyumbani anakwambia mwalimu wake hajamwambia hivyo ni vema watoto wakafundishwa maadili shule tokea wakiwa na umri mdogo,” anasema Mboya na kuongeza.
“Kila mtu akisimama kwenye nafasi yake tunaweza kupambana rushwa ya ngono binti anavaa nguo fupi akishikwa na mhadhiri analalamika, mwanafunzi hasomi hafanyi majaribio halafu mwenzako anakushauri uende kwa mwalimu peke yako unategemea nini?,”.
“Ukifanyiwa vitendo vya unyanyasaji utamlaumu nani watoto wa kike timizeni wajibu wenu someni, fanyeni kazi mnazopewa darasani vizuri kupunguza haya matukio ya rushwa za ngono,”
“Mimi ni mwalimu wa saikolojia kila kitu kinaanza na namna unavyofikiri. Watu wasimame wawe imara tujengeane ujasiri sisi kwa sisi kujua nini sahihi kufanya na kipi si sahihi kufanya,”.
Irene Mzirai kutoka HMC anataka ubuniwe mfumo rafiki wa kutoa taarifa wa vitendo vya ukatili wa kijinsia na rushwa ya ngono vyuoni.
Anasema pia kuwe na wataalam wa saikolojia vyuoni watakaotoa ushauri nasaha kuwasaidia na kuwalinda wahanga wanaofanyiwa vitendo vya ukatili na wanaoombwa rushwa ya ngono.
Hata hivyo mwanachuo, Ombeni Patric alionyesha mashaka yake juu ya wale watakaosimamia madawati ya jinsia akihoji utatumika utaratibu gani kuhakikisha wanapatikana watu sahihi.
“Madawati ya jinsia wamepimwa vipi kuwa wanaweza kulinda haki za wanaotendewa ukatili wa kijinsia. Mzee Juma anapewa nafasi kusimamia hili dawati kijijini kwa kuwa ni mkimya kumbe huko nyuma ana tabia ya kunyanyasa wanawake,” anatoa angalizo Ombeni na kuongeza
“ Mzee Juma na yeye anampendekeza mzee John kusaidiana naye kumbe naye anatabia za kutesa familia yake hakuna nayejua sasa inapotokea mhanga anapeleka malalamiko kwenye hili dawati atasaidika kweli,”
Mkufunzi kutoka HNC, Kelfas anaonyesha mashaka yake kuwa kwa sheria ya ushahidi ilivyo inaweza kumsababisha mwanachuo anayekusanya ushahidi akajikuta amenasa kwenye mtego wa kutoa rushwa ya ngono
“Tujiulize viashiria vinaweza kumtia hatiani muhusika kisheria? badala ya kusubiri kutokea kwa tukio kwa sababu mtu mwingine anaweza kujikuta amejiingiza kwenye tatizo ili kupata ushahidi,” Mkufunzi huyo anatoa angalizo.
Anasema kesi nyingi za ukatili wa kijinsia ikiwemo za rushwa ya ngono zinashindwa kuendelea baada ya familia au mtendewa kumalizana nje ya mahakama au polisi, mawakili wa serikali au mahakimu kupokea rushwa hivyo mhanga anashindwa kupata haki.
“Kuwe na sheria ya kuwabana polisi, mawakili na mahakimu ambao wanapokea rushwa halafu wanasababisha haki isipatikane.Polisi akipokea rushwa asikusanye ushahidi, wakili wa serikali akipokea rushwa akaacha kumtetea ipasavyo mhanga wa unyanyasaji wa kingono au hakimu anayeamua kwa uonevu,” anashauri Kelfas.
Mkufunzi kutoka TICD, Rose Mtei, akitoa mada ya hali ya ukatili wa kijinsia vyuoni amesema kuwa mfumo wa elimu utengeneze mitaala ambayo mtoto akiwa chekechea ajue namna gani ya kuishi badala ya kusubiri siku moja kwa wiki ya kwenda kanisani au msikitini.
Anasema inakuwa ngumu mafunzo ya siku moja kupindua yale aliyoyasilikiza kwa wiki nzima huku akawatolea uvivu washiriki wa mdahalo huo kuwa kuna anaowaona wanachangia lakini ndiyo haohao wanaogombana nao lwa luliuka maadili chuoni.
“Kuongea hapa ni rahisi lakini tunaenda kutenda tofauti kwa sababu hatujajengwa vizuri kimaadili. Ni vema mitaala yetu ikatangenezwa iwafundishe watoto namna ya kuishi kwa maadili mazuri watu wawe na ujasiri wa kusema kile kinachotakiwa na ambacho hakitakiwi,” anasisitiza Mtei na kuongeza.
…Hata mifumo ya kisheria inaumiza watu yaani mtu kaumizwa lakini suala la kukosekana ushahidi unaochukuliwa kwa mujibu wa sheria linamfanya akose haki,”.
Mtei anasema anayefaulu mtihani kwa ngono hataishia hapo ataendelea kutumia ngono kuingia kazini na ukipata kazi kwa rushwa ya ngono hata ukiingia kazini bado utaendea kutumia ngono kubaki kazi hivyo Taifa litakosa watu sahihi kwa kuwa kuna watu wanaendekeza rushwa kufanikisha malengo binafsi.
“Tunatakiwa tuzungumze kuhusu maadili. Mtoto wa kike anapolelewa kama mnyonge na wa kiume ni simba hata kulia unaambiwa wewe wa kiume unaliaje hii si sahihi tubadilike tuwape haki sawa tokea wakiwa wadogo,” anaonya Mtei na kuongeza.
…Ukiwaacha na mtazamo huo hata akifika kule juu hata mtu akimshika kwa kumdhalilisha mtoto wa kike ataona ni sawa kwa kuwa amezoa kuonyeshwa yeye ni mnyonge jambo ambalo si sahihi,”.
“ Mtoto wa kike ni sawa na wa kiume tofauti ni jinsi mmoja anakuwa na maziwa na mwingine ndevu ila wote wana haki sawa mbele ya jamii. Hivyo tukikufundisha hapa ukitoka nenda kafundishe kwenye jamii na familia tumalize tatizo la ukatili wa kijinsia na rushwa za ngono vyuoni,”.
Mtei anasema kuwa tatizo la rushwa ya ngono vyuoni hata yeye kama mkufunzi kuna wakati lilimweka kwenye hali wakati mgumu baada ya mwanachuo aliyeripoti kuombwa rushwa ya ngono kuamua kubadilika na kudai hakutoa taarifa hiyo.
“Kubadili tabia ni shida mtu amekuzwa akiona kumnyanyasa mwanamke ni sawa.
Kuna wakati nikiwa matroni akaja mwanafunzi analalamika kuwa kuna mwalimu anamfanyia vitendo vya kinyanyasaji anataka kuacha chuo.”
“Tukamsihi asiache chuo, tukaanza kushughulikia suala hilo, bahati tulimsikiliza nikiwa na mwalimu mwenzangu tukamuita mwalimu aliyehusika kuomba rushwa ngono tukaongea naye ,” tukamuhoji.
“ Lakini baada ya wiki mwanafunzi akabadilika akadai kuwa sisi ndiyo tunamuwekea maneno mdomoni,Kuanzia hapo ikanifanya nibadilike haya matukio nayashughilikia kwa tahadhari sana kwa sababu mwisho wa siku yanaweza kukufanya uonekane mbaya kwa waalimu wenzako na jumuiya nzima ya chuo,”.
Mwanachuo, Samuel Saitoti kutoka, HMC anasema rushwa ya ngono inarudisha nyuma maendeleo ya mwanafunzi kwani atashindwa kufahamu kilichompeleka shule hivyo atashindwa kuwajibika kwenye kujifunza na mwalimu atakuwa anaendekeza tabia hiyo inayojenga mazingira ya ngono baina yao kuendelea.
Martha Mzirai anasema rushwa ya ngono inaleta mmomonyoko wa maadili kielimu na kijamii hiyo itakuwa ni kitu endelevu kwani baada ya kumaliza shule kuingia kazini utataka uendelee kutumia ngoni kupata ajira na ukiingia kazini pia ataendelea kukutumia kubaki kazini.
Joyce Magesa mtangazaji Radio Habari Maalum anasema wanawake wapatiwe haki zao wasiwe wanyonge wakiona hawapatiwi huku akiwaasa wanachuo wa kike kuwa “thamani yako inashuka kwa kuwa unakuwa umetumika sana kuanzia shule na kazini,”.
Hata hivyo Mkuu wa chuo HMC, Nestory Ihano mbali na kuunga mkono kupinga rushwa ya ngono vyuoni lakini watoto wa kike lazima wabadilike huku akieleza kuwa akiwa kwenye mafunzo yake ya ualimu chuo kikuu kuna wakati akaenda kufanya mafunzo kwa vitendo Bwiru sekondari akawa anasimamia mitihani.
"Nilishangaa kuona msichana anapandisha sketi yake juu, vile nina Roho wa Mungu (kicheko) sikuingia majaribuni hivyo hii kampeni ni yakutetea wanafunzi wa kike lakini hata waalimu wanahitaji kutetewa," alisema Ihamo.
Mwanachuo, Zulfa Musa kutoka chuo cha TDC anasema washiriki wasijikite tu kuzungumzia rushwa ya ngoni vyuoni bali wajadili na ukatili mwingine ambao watoto wa kike wanakabiliana nao vyuoni.
“Tunazungumzia rushwa ya ngono lakini kuna tatizo la vijana wanapokuwa kwenye mahusiano vijana wa kiume wanawapiga na kuwanyanyasa wanawake.
Hivyo elimu kwa jamii ni muhimu kuanzia ngazi ya familia mpaka shule.
Mwakilishi kutoka ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka nchini, (DPP), Akisa Mhando anasema licha ya kuwepo kwa malalamiko juu ya uwepo matukio ya rushwa ya ngono kwenye elimu ya juu lakini mwamko wa wahanga kujitokeza kwenye vyombo vya kiuchunguzi ili wahusika waweze kuchukuliwa hatua ni mdogo.
Wakili huyo wa Serikali Mwandamizi anasema kuwa kuwa licha ya kuwa kuna tatizo kubwa la rushwa ya ngono vyuoni lakini hakuna malalamiko wanayopokea kwa ajili ya kupelekwa mahakamani.
"Masuala ya rushwa watu hawaji kulalamika, hakuna hata siku moja katika maisha yangu ya uwakili wa serikali kuna mtu aliwahi kuja kulalamika. Sijawahi kuona mtu anayelalamikia kuombwa rushwa ya ngono vyuoni, wangekuwepo watu wa TAKUKURU hapa wanaohusika na uchunguzi wa masuala ya rushwa wangesema," anasema Mhando.
Akijibu maswali ya washiriki waliotaka kujua inakuwaje ofisi ya DPP inafuta kesi ambazo tukio lilitokea kweli na kila mtu aliona Mhando anasema kuwa hiyo inasababishwa na udhaifu wa ushahidi uliokusanywa wakati wa upelelezi au muathirika kuingia makubaliano na mshitakiwa hivyo kutotokea mahakamani.
Hata hivyo anasema kuwa ni mara chache sana kusikia ofisi ya DPP kufuta kesi za ukatili wa kijinsia kwani wanajitahidi kuhakikisha zinaenda mpaka mwisho.
"Jinsi unavyojitahidi kuweka ushahidi haunyooki, au unakuta mashahidi na muathirika wamekubaliana nje ya mahakama ukiwaita mashahidi mahakamani hawaji. Unaona bora uitoe hiyo kesi mahakamani kwa kifungu cha 91 cha CPA kinakupa nguvu ya kuitoa lakini inakuwezesha kuirejesha mahakamani," anasema Mhando na kuongeza.
... Ukishaitoa kesi hiyo unaweza kwenda kuwakamata mashahidi hapo unawaza kulirudisha shauri mahakamani kesi inaendelea,".
Mwakilishi wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wakili wa serikali, Mkama Msalama anasema kuwa kuna muongozo wa serikali unaotaka kila taasisi ya elimu iwe na dawati anaamini kupitia kampeni hii hilo litafanikiwa kwa mkoa wa Arusha.
“Tumekuwa tukisikia haya matukio kwenye baadhi ya vyuo, leo nimeona kumbe yapo vyuo vingi wangesema vyuo wote waje nafasi ingepungua lakini wachache tuliopata hii elimu tukawe waalimu,” amesema Msalama na kuongeza.
…Changamoto ya ukatili wa kijinsia inaanza tokea tukiwa wadogo inakuwa ngumu kubadilika tukiwa wakubwa kuna wazazi na walezi hapa. Kila Taifa, kila bara yana tamaduni zake yale mazuri tuyaige yale mabaya tusiyaige,”.
“Tuwe chachu ya kuhimiza ndugu na jamaa kubadilika, watoto wakasome tuwe na hofu ya Mungu tuyafate yale yanayoandikwa kwenye maandiko Matakatifu yote haya mabaya ya rushwa ya ngono hayatatokea,”.
Msalama anamalizia kwa kuwahimiza washiriki wa mdahalo huo kuwa andapo wakiwa vyuoni wakiona wenzao wanaenda kinyume na utaratibu wawakumbushe kutimiza wajibu wao.
“Kwa hapa Arusha kuna changamoto ya masula ya jinai, masuala ya unyanyasaji wa kijinsia wanakuwa wanamalizia nyumbani matatizo ambayo yanapaswa kumalizika mbele ya mahakamani,” anasema Msalama
“Ili ushinde kesi ni ushahidi kama hautaki kutoa ushahidi hauwezi kushinda.
Makosa ya jinai hayana kipengelea cha kufanya makubliano nje ya mahakama inatakiwa iishie ndani ya mahakama kesi za madai ndiyo wanaweza kukubaliana nje ya mahakama,”
“Wanaotoa na wanaodai rushwa ya ngono wakipatikana wakashitakiwa na kuadhibiwa na mahakama inasaidia jamii kubadilika kwani watajua wakifanya vitendo vya unyanyasaji wa kingono watachukuliwa hatua,”
“Kesi ni ushahidi sasa mhanga akigoma kutoa ushahidi huwezi kushinda kesi.
Kwenye sheria inatambua kuwa na nia unaweza kurekodi endapo utaona viashiria japo haviwezi kumtia mtu hatiani mpaka kitendo cha kuvunja sheria kifanyike,”.
“Tuna shida sana kwenye jamii hasa elimu ya juu, zamani mtu wa chuo kikuu alikuwa akiheshimika hata akitaka kuongea kila mtu anataka kumsikiliza lakini kwa sasa hata mtoto wa darasa la saba anamzidi hekima,”.
“Maadili mema ndiyo muarubaini wa tatizo la rushwa ya ngono vyuoni hili vijana wana mavazi yasiyo mazuri binti wa chuo kikuu amevaa nguo fupi kupita kiasi hivi jamii inajifunza nini kwake,”.
Msalama anasema kuwa zamani kulikuwa hakuna makanisa mengi na hakukuwa na hizi changamoto lakini sasa makanisa yako kila kona na haya matendo yasiyo na maadili yanaongezeka.
Kwa upande wake, , Makamu Mkuu wa Chuo cha Habari Maalum, (HMC) AstereTaluka, aliwataka wanachuo kuyaweka kwenye utekelezaji yale waliyojifunza kwenye uzinduzi huo kupitia mjadala wa wazi, majadiliano ya vikundi na mada zilizowasilishwa ili mazingira ya chuo yawe salama kwa ajili ya kujifunza bila kuwepo na tatizo la rushwa ya ngono











No comments:
Post a Comment