WCWELS YAZINDUA KAMPENI KUPIGA VITA RUSHWA YA NGONO VYUONI


 LICHA ya kuwepo kwa malalamiko juu ya uwepo matukio ya rushwa ya ngono kwenye elimu ya juu lakini mwamko wa wahanga kujitokeza kwenye vyombo vya kiuchunguzi ili wahusika waweze kuchukuliwa hatua ni mdogo.



Hayo yalisemwa leo Mei 13, 2022 na Mwakilishi kutoka ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka nchini, (DPP), Akisa Mhando kwenye uzinduzi wa kampeni ya kuzuia na kupambana na rushwa ya ngono na kijinsia kwenye taasisi za elimu ya juu mkoani Arusha.

Wakili huyo wa Serikali Mwandamizi amesema kuwa kuwa licha ya kuwa  kuna tatizo kubwa la rushwa ya ngono vyuoni lakini hakuna malalamiko wanayopokea kwa ajili ya kupelekwa mahakamani.

"Masuala ya rushwa watu hawaji kulalamika, hakuna hata siku moja katika maisha yangu ya uwakili wa serikali kuna mtu aliwahi kuja kulalamika. Sijawahi kuona mtu anayelalamikia kuombwa rushwa ya ngono vyuoni, wangekuwepo watu wa TAKUKURU hapa wanaohusika na uchunguzi wa masuala ya rushwa wangesema," amesema Mhando.


Akijibu maswali ya washiriki waliotaka kujua inakuwaje ofisi ya DPP inafuta kesi ambazo tukio lilitokea kweli na kila mtu aliona Mhando amesema kuwa hiyo inasababishwa na udhaifu wa ushahidi uliokusanywa wakati wa upelelezi au muathirika kuingia makubaliano na mshitakiwa hivyo kutotokea mahakamani. 


Hata hivyo amesema kuwa ni mara chache sana kusikia ofisi ya DPP kufuta kesi za ukatili wa kijinsia kwani wanajitahidi kuhakikisha zinaenda mpaka mwisho.

"Jinsi unavyojitahidi kuweka ushahidi haunyooki, au unakuta mashahidi na muathirika wamekubaliana nje ya mahakama ukiwaita mashahidi mahakamani hawaji. Unaona bora uitoe hiyo kesi mahakamani kwa kifungu cha 91 cha CPA kinakupa nguvu ya kuitoa lakini inakuwezesha kuirejesha mahakamani," amesema Mhando na kuongeza.

... Ukishaitoa kesi hiyo unaweza kwenda kuwakamata mashahidi  hapo  unawaza kulirudisha shauri mahakamani kesi inaendelea,".


Kwa upande wake, Mkurugenzi wa shirika la Usaidizi wa Ustawi wa Wanawake na watoto, (WOCWELS), Mary Mushi amesema kuwa lengo la kampeni hiyo ni kukuza na Kukuza uelewa na kujengea uwezo wa wanafunzi wa taasisi ya elimu ya juu kuhusu kukabiliana, kufuatilia na kuripoti taarifa za ukatili wa kijinsia ikiwemo rushwa ya ngono.



Amesema kuwa kampeni hiyo itafanyika kwenye vyuo vyote mkoani Arusha ambapo kwenye uzinduzi huo wameshirikisha wanavyuo 50 kutoka vyuo vya Radio Habari Maalum, Fanikiwa na Chuo cha Maendeleo ya Jamii Tengeru, (TICD) ambapo watawawezesha kuanzisha uendeshaji na ufuatuliaji wa dawati la jinsia.


Naye, Makamu Mkuu wa Chuo cha Habari Maalum, (HMC) Astere Taluka, aliwashukuru WOCWELSkwa kuleta mafunzo hayo anayoamini yatasaidia kuwapa wanavyuo uelewa wa kutosha juu ya mambano ya rushwa ya ngono hivyo kujenga jamii nzuri.

"Niwatake kila mmoja kufungua masikio na kuweza kusikiliza na kuyaweka kwenye utekelezaji ili mazingira ya chuo yawe salama kwa ajili ya kujifunza bila kuwepo na tatizo la rushwa ya ngono," amesema Taluka.


0 Comments:

Post a Comment