MASOKO ya hisa huuza na kununua hisa za makampuni yaliyoorodheshwa kwenye masoko ya mitaji ambapo hisa husika zinaweza kuwa ni za kawaida au za upendeleo.
Hisa zinatofautiana kutokana na vigezo mbalimbali ambapo hisa za kawaida humwezesha mwekezaji kurudishiwa mtaji wake akiwa mdau wa mwisho baada ya wadau wengine wote kulipwa kutokana na mauzo ya rasilimali za kampuni ambapo hii hutokea kampuni inapofilisiwa.
Pia kiwango cha gawio kinacholipwa hakijulikani tangu awali ambapo hisa za upendeleo zina kiwango maalumu cha gawio ambacho hulipwa kutokana na faida ya kampuni ambapo wenye hisa za kawaida hubeba uwezekano mkubwa wa hasara kuliko wenye hisa za upendeleo.
Hisa za kawaida zinawakilisha sehemu ya umiliki wa kampuni, kama kampuni ina hisa milioni moja na mwekezaji ana hisa 10,000, basi mwekezaji huyo atakuwa anamiliki asilimia moja ya kampuni hiyo.
Hivi karibuni wanahisa wa benki ya CRDB walikutana jijini Arusha kwa siku mbili ambapo siku ya kwanza ilikuwa maalum kwa ajili ya kutoa elimu kwa wahisa ili kukuza uelewa wa masuala mbalimbali ya fedha na uwekezaji katika masoko ya mitaji. .
Aidha siku inayofuata walifanya mkutano wao mkuu wa 27 ambapo kwa kauli moja wanahisa wa Benki ya CRDB wakapitisha kwa kauli moja mapendekezo ya Bodi ya Wakurugenzi kuhusu malipo ya gawio la Shilingi 36 kwa kila hisa.
Mwenyekiti wa Bodi ya Benki hiyo Dkt. Ally Laay akafafanua kuwa gawio lililoidhinishwa kwa kila hisa ni ongezeko la asilimia 64 ikilinganishwa na Shilingi 22 kwa kila hisa iliyotolewa mwaka jana.
Amesema kuwa hiyo inaashiria ukuaji wa mapato kwa kila hisa ambapo katika kipindi cha mwaka 2021 yalikuwa Shilingi 102.7.
Laay amesema kuwa kampuni tanzu za Benki hiyo ziliendelea kuchangia vyema katika biashara ya kundi huku kampuni tanzu ya Burundi pekee ikichangia faida ya jumla ya Shilingi bilioni 12.8 huku kampuni tanzu ya bima ikichangia faida ya shilingi milioni 859 ambapo jumla ya mchango wa kampuni tanzu kwenye faida ya kundi ilikuwa asilimia tano.
" Nafurahi kuripoti kwenu kwamba tumepata maendeleo makubwa katika kupata leseni na vibali vinavyohitajika kutoka kwa mamlaka za nyumbani pamoja na DRC. Tunatarajia kuanza uendeshaji ndani ya nusu ya pili ya mwaka wa fedha wa 2022.,” alibainisha alipokuwa akiwasasisha wanahisa kuhusu upanuzi wa kimkakati wa Benki hadi DRC.
Akizungumzia utendaji wa mwaka uliopita, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela amesema mapato ya uendeshaji ya Kampuni yaliongezeka kwa asilimia 14.3 sawa na Shilingi bilioni 924.0 kutoka Shilingi bilioni 808.7 mwaka 2020.
Anasema kuwa ukuaji huo ulitokana na ongezeko la asilimia 11.3 ya mapato ya jumla ya riba, yaliyotokana na ukuaji mzuri wa mikopo kwa wateja wadogo na wakati. Pamoja na ukuaji wa mikopo Benki hiyo lilifunga mwaka na uwiano wa mikopo chechefu wa wa asilimia 3.3 kulinganisha na kiwango cha udhibiti cha soko cha asilimia tano
Nsekela anasema Benki ya CRDB pia ilirekodi ukuaji mkubwa wa mizania wa mwaka hadi mwaka wa asilimia 23 kutoka Shilingi trilioni 7.2 mwaka 2020 hadi Shilingi trilioni 8.8. Ukuaji huo ulisababishwa na ukuaji wa asilimia 19.4 wa amana za wateja hadi Shilingi trilioni 6.5 kutoka Shilingi trilioni 5.4 zilizoripotiwa mwaka 2020, na ukuaji wa 20.6% wa fedha za wanahisa.
"Kutokana na mtazamo wetu makini katika mwaka huo, Benki yetu iliendelea kukamata masoko kwa bidhaa na huduma bunifu, hivyo kupelekea ukuaji endelevu katika mapato na faida yetu. Tuliendelea kufanyia kazi changamoto za wateja ili kuboresha utoaji wetu wa huduma na kuhakikisha tunawapa uzoefu uliobora zaidi pindi watumiapo huduma zetu,” anafafanua zaidi Nsekela.
Akizungumzia kuhusu mipango ya mbeleni, Mkurugenzi Mtendaji huyo anasema kuwa kipaumbele cha Benki hiyo ni kuimarisha vichocheo vya ukuaji, na kujenga misingi imara ya uendelevu ambapo aliutangaza mwaka wa fedha wa 2022 kuwa mwaka wa mwisho wa mkakati wa muda wa kati wa Benki ya CRDB ambao ulikuwa na jukumu muhimu katika kuimarisha utendaji, na umeipa msingi mzuri benki hiyo kukabiliana na siku zijazo.
Akizungumzia malipo ya gawio hilo, aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu Mtendaji wa Benki hiyo na Mbunge wa Vunjo, Dkt. Charles Kimei, ameeleza kufurahishwa kwake na kuendelea kuongezeka kwa gawio huku akibainisha kuwa ukuaji huo ni mkubwa kupata kutokea.
Dkt. Kimei alisema kuwa hisa za benki hiyo zimebakia kuwa chachu ya wawekezaji kwasababu benki hiyo haijawahi kushindwa kutoa gawio kwa Wanahisa wake.
“Kabla ya kununua hisa ni lazima ujue unawekeza kwenye kampuni gani kwa sababu si kila kampuni inaweza kupata faida. Lakini benki ya CRDB yenye uzoefu wa miaka zaidi ya 27 kwenye biashara una uhakika zaidi wa kupata gawio," anasema Dkt Kimei na kuongeza.
..Gawio linazidi kuongezeka mwaka hadi mwaka, kama mwaka huu limekuwa kubwa sana nimewaambia gawio langu sichukui, waniongezee kwenye hisa zangu nizidi kunufaika, hivyo watu wasiogope kuja kununua hisa huku tunapata faida,”
“Benki hii ina misingi mizuri , ina mtaji mkubwa, mtandao mkubwa kuweza kufikia watu maeneo mengi ndani na nje ya nchi hivyo mahali kwa uhakika kununua hisa ni CRDB,”.
Mwana hisa mwingine, Dkt Festo Kilawe anasema kuwa yeye ni miongoni mwa wanahisa wa mwanzo ambapo alianza kwa kununua hisa za milioni moja wakati huo benki ndiyo imeanza.
“ Miaka miwili ya mwanzo benki iliyumba sana DANIDA ( Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Denmark) wakaweka nguvu ya ziada huku wakitushauri wanahisa tusichukue gawio badala yake tuongeze hisa,” anaeleza Dkt Kilawe na kuongeza.
…Alipokuja Dk Kimei mambo yalianza kubadilika faida ikaanza kuonekana tukaambiwa tunaongezewa hisa mfano aliyekuwa na hisa moja akaongezewa zikawa tatu na hisa ilikuwa shilingi 10,000,”
“Baada ya hapo hisa zikawa zinapanda kila mwaka, tukawa tunaongezewa kwenye hisa zetu wakiita bakshishi. Hisa nilizonunua kwa shilingi milioni moja wakati benki inaanza nikauza shilingi milioni 100 kwenye mwaka 2016 na 2017 na bado nikabaki na hisa za shilingi laki moja,”.
“Nilinunua benki na sasa najivunia kwani bado napata gawio kwa sababu benki inajiendesha kwa mifumo ya kisasa wananchi wengi akielewa umuhimu wa hisa naamini wangekuja kununua,”
Mwanahisa mwingine Giatar Beder ambapo alinunua hisa za CRDB kwenye benki hiyo mwaka 1996 ambapo alieleza kuwa anaridhishwa na utendaji wa menejimenti na bodi ya benki hiyo unayoifanya kuwa moja ya benki zinazoaminiwa ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.
Katika hatua nyingine, wanahisa waliidhinisha Ernst & Young kama Wakaguzi wa Nje wa Benki kwa mwaka wa fedha wa 2022, kuashiria imani yao katika sheria ya kiakili ya kampuni na kuendelea kwa Benki kuzingatia itifaki za utawala bora.


No comments:
Post a Comment