MFANYABIASHARA maarufu jijini Arusha ambaye amewahi kuwa mgombea ubunge kwenye jimbo la Arusha Mjini kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi, (CCM) ,Dkt Philemoni Mollel maarufu kama Monaban ameamua kujikita kwenye masuala ya dini baada ya baada ya kutawazwa kuwa mchungaji wa kanisa jipya la Kilutheri Afrika Mashariki, (KKAM).
Monaban ambaye mwaka 2025 alichuana vikali na Godbless Lema wa Chadema kwenye ubunge wa jimbo la Arusha mjini kisha mwaka 2020 alichuana vikali na mbunge wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo kwenye kura za ndani ya chama hicho, Mei 15, 2022 alitawazwa kuwa mchungaji pamoja na waumini wengine wanne kwenye kanisa hilo Ngaramtoni wilayani Arumeru.
Kabla ya kujiunga na kanisa hilo, Monaban alikuwa muumini wa kawaida wa kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Daiyosisi ya Kaskazini Kati usharika wa Sokon II ambapo mbali ya kuwa muumini lakini amekuwa ajitolea kusaidia shughuli mbalimbali kanisani hapo.
Akiongea mara baada ya kuvishwa taji la uchungaji, Monaban alisema kuwa ndoto yake kubwa ilikuwa ni kumtumikia Mungu kupitia uinjilishaji hivyo kupata wadhifa huo, kumekamilisha ndoto yake.
Hata hivyo aliweka wazi kuingia kwenye uchungaji hakumwondolei harakati za kuendesha siasa bali atapangilia namna ya kutekeleza majukumu yake ya kichungaji na ya kisiasa.
"Kazi ya utumishi wa Mungu nilianza muda mrefu lakini leo nafurahi kanisa hili limetambua mchango wangu na kunivisha taji la uchungaji. Kwenye siasa wapo wachungaji na kila jambo lina wakati wake, "alisema Monaban.
Awali askofu mkuu wa kanisa hilo, Oscar Olotu aliwatahadhalisha baadhi ya waumini kuhusu utitiri wa makanisa ambayo baadhi yao yamekuwa yakipotosha waumini wake na hivyo kwenda kinyume na amri za Mungu na sheria za nchi.
Aliwataka watu kabla ya kujiunga na makanisa hayo wachunguze yanahubiri nini na yanamtangaza nini kwa sababu yameibuka makanisa mengi ya uongo na upotoshaji na kuishauri serikali kuchunguza kinachohubiriwa.
Kwa upande wake, katibu wa kanisa hilo, Hericky Mkwizu alisema kuwa kubarikiwa na kuingizwa kazini kwa wachungaji nane wa kanisa hilo ni mwanzo mzuri wa kukubalika kwa kanisa hilo ambalo limeanza kuenea katika maeneo mbalimbali nchini.
"Baada ya kukamilika kwa zoezi la kuwaingiza kazini wachungaji nane, Mei 28 mwaka huu tutakuwa na ibada maalumu ya kumsimika askofu mkuu na askofu msaidizi wa kanisa hili jimbo la Arusha Mashariki, "alisema Mkwizu.
Kanisa la KKAM limeenra maeneo mbalimbali dkwenye mikoa ya Kilimanjaro, Dar es Salaam, Arusha, Tabora, Manyara, Tanga, Singida na sasa linaelekea katika mikoa ya Shinyanga ,Mwanza na Sumbawanga.
.jpeg)
0 Comments:
Post a Comment