MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji, (EWURA), imewataka wafanyabiashara wa gesi kutumia mizani kwa ajili ya kupimia uzito wa mitungi ya gesi ili kuhakikisha ina ujazo sahihi na kuacha tabia ya kuuuza gesi bila kuipima mteja akishuhudia.
Hayo yameelezwa Mei 20, 2022 na Meneja EWURA Kanda ya Kaskazini, mhandisi, Lorivii Long'idu wakati akiongea na wauzaji wa gesi za majumbani kwenye semina iliyoandaliwa na kampuni Taifa Gas inayojihusisha na uagizaji na usambazaji wa gesi inayotumika majumbani, mahotelini, viwandani na taasisi mbalilmbali
Amesema kuwa kwa sasa bado wapo baadhi ya wafanyabiashara ambao wanauza mitungi ya gesi bila kupima jambo ambalo ni kinyume na sheria kwani uzito unatakiwa kuonekana kabla ya mtumiaji kufikisha nyumbani na kuanza matumizi.
Mhandisi Lorivii amesema kuwa wauzaji wa gesi wanawajibu wa kumuuzia mtuamiaji kilo ambazo zimeoneshwa kwenye mtungi
"Mwananchi unatakiwa kuhakikisha kuwa umeona muuzaji akiwa amepima na umejiridhisha kabisa kuwa ni kiwango hicho lakini kama ni pungufu basi pia utaona," amesisitiza mhandisi huyo.
Ameongeza kuwa wafanyabiashara wa uuzaji wa mitungi hiyo ya gesi wakifuata sheria basi changamoto hizo za ujazo hafifu zitaisha kabisa
Amewataka wafanyabiashara kuhakikisha kuwa wanakuwa waaminifu na kuachana na tabia ya kupunguza gesi kwani endapo watakamatwa sheria itawafikisha mahakamani
"Tulifanya msako Moshi (mkoani Kilimanjaro) na tumeshawafikisha mahakamani wafanyabiashara wawili. Niwaombe tu ninyi wafanyabiashara kama kuna wanaofanya hivyo waache kwani ni hatari sana ndani ya jamii," ameonya mhandisi Lorivii.
Kwa upande wake Meneja Mauzo wa kampuni ya Taifa Gas, , Joseph Nzumbi amesema bado kuna changamoto ya ujazaji wa mitungi holela mitaani hasa kwenye mikoa ya Kaskazini.
Amewataka watumiaji wa gesi nao kabla ya kuinunua wahakikishe wanaipima ili kuhakikisha uzito anaolipia unawiana na kiwango kilichoandikwa kwenye mitungi.

No comments:
Post a Comment