SAMIA AZIAGIZA HALMASHAURI ZENYE MFUMO WA M-MAMA KUTENGA FEDHA ZAIDI HUDUMA YA MAMA NA MTOTO

 
Rais , Samia Suluhu Hassan akisikiliza jambo kutoka kwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye wakati wa uzinduzi wa Mfumo wa usafirishaji wa dharura kwa wajawazito na watoto wachanga (M-MAMA) katika hafla iliyofanyika viwanja vya Chinangali Park Jijini Dodoma.

RAIS  Samia Suluhu Hassan ameagiza Wakuu wa Mikoa katika Halmashauri ambazo mfumo wa M-MAMA utatekelezwa, kutenga fedha zitakazoongeza nguvu kwenye huduma ya mama na mtoto mchanga.



Amesema hayo leo April 7, 2022 wakati akizindua mfumo wa usafirishaji wa dharura wa wajawazito na watoto wachanga (M-MAMA) iliyoratibiwa na kampuni ya simu ya Vodacom katika viwanja vya Chinangali jijini Dodoma.



Rais Samia amesema, lengo la mfumo huo ni kuhakikisha kuwa wakina mama zaidi ya milioni moja ambao ni walengwa wanafikiwa na kunufaika na huduma hii katika kipindi cha miaka mitano.



Amesema tangu kuanza kwa majaribio ya mfumo wa M-MAMA katika Wilaya ya Sengerema na mkoani Shinyanga mwaka 2013, wanawake na watoto 12,000 wameshahudumiwa na hivyo kusaidia kupunguza vifo vya kina mama vinavyotokana na ukosefu wa usafiri.



Rais Samia ameitaka Kampuni ya Vodacom kuufanya mfumo huo uwe endelevu na uwafikie wananchi wengi na kutoa wito kwa kampuni zingine zilizopo nchini kuwekeza katika sekta mbalimbali.


Amesema, pamoja na jitihada zilizofanywa na Serikali, bado zipo changamoto ambazo husababisha vifo vya mama na mtoto kabla au baada ya kujifungua kutokana na kukosekana kwa mawasiliano ya haraka na usafiri wa uhakika wa kumwahisha mama mjamzito kufika katika kituo cha afya.



Rais Samia ameiagiza Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kulinda taarifa binafsi za watumiaji wa M-MAMA ili zikusanywe, kuchakatwa na kuhifadhiwa kwa mujibu wa Sheria na Kanuni zinazokubalika Kimataifa

0 Comments:

Post a Comment