SAMIA AKEMEA NIDHAMU YA WOGA SERIKALINI, ILISHAMIRI AWAMU YA TANO


RAIS, Samia Suluhu Hassan amewataka viongozi na watumishi wa umma kuwa na heshima ya kweli kutoka ndani ya mioyo yao na kila mtu kutimiza majukumu yake kwa maadili na weledi mkubwa kwa maslahi mapana ya taifa.

Aidha amesema heshima iliyokuzwa awamu ya tano ni ya woga kwa sababu kulikuwa na Simba wa Yuda ambaye akiguswa sharubu anararua.

Rais Samia ameyasema hayo leo Aprili 2,2022 jijini Dodoma wakati akiwaapisha viongozi mbalimbali wakiwemo mawaziri watatu aliowabadilisha wizara siku chache zilizopita.

Amesema  kuwa licha ya serikali ya awamu ya tano kusifiwa kwa kukuza heshima kwa watumishi wa umma, lakini heshima hiyo ilikuwa ya woga, na hivyo akawataka watumishi kuwa na nidhamu kutoka ndani ya mioyo yao.


“Tunasifiwa kuwa awamu ya tano tulikuza heshima kwa watumishi wa umma, heshima iliyokuzwa ni heshima ya woga kwa sababu alikuwepo simba wa Yuda, ambaye ukimgusa sharubu anakurarua, heshima inayotakiwa iwe ya moyoni” ,amesisitiza  Rais Samia.


Amesema heshima hiyo ya woga imechangia baadhi ya mambo kutofanyika kwa kiwango kinachotakiwa.

Rais Samia amesema kuwa ataendelea kufanya kazi kwa kalamu, na kamwe hawezi kuwafokea watendaji walio chini.


“Mimi ni mtumishi wa serikali majukumu yangu ni haya sitakiwi kuvuka laini hii sitakiwi kuvuka huku, kila mmoja aheshimu laini ya mwenzake hicho tunakosa serikalini,”amesema Rais Samia na kuongeza.


...Unaangalia kila siku unasika Waziri kaparurana na katibu wake, katibu kaparurana na waziri wake naibu hamueshimu nani hakuna hiyo kitu nadhani kuna kitu tunakosa mahali,”.


Machi 31, 2022 Rais Samia alifanya mabadiliko madogo ya baraza la mawaziro ambapo aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria, George Simbachawene alihamishwa kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Bunge, Sera na Uratibu huku nafasi yake ikichukuliwa na Damas Ndumbaro.

Waziri Ndumbaro yeye alihamishwa kutoka kuwa Wizara ya Mali asili na utalii nafasi ambayo sasa imechukuliwa Pindi Chana ambaye kabla ya hapo alikuwa Waziri wa Bunge, Sera na Uratibu.



0 Comments:

Post a Comment