Sunday, April 3, 2022

KIFUSI CHAUA WATATU KIGAMBONI


WATU watatu wamefariki dunia na wawili kunusurika baada ya kufukiwa na kifusi wakati wakiwa kwenye shughuli za machimbo ya mawe katika eneo la machimbo ya Kikikaka, Mji Mwema Kigamboni, Dar es salaam.



Ajali hiyo imetokea mapema leo Aprili 3, 2022 saa tatu asubuhi wakati watu hao  wakipakia kokoto katika gari kwenye  machimbo hayo ambayo awali yalikuwa yakitumiwa na wachimba kokoto wadogo kabla ya Serikali kuyafunga mwaka 2018.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Mjimwema, Mohamed Gharib Mohamed amethibitisha na kusema majeruhi wamekimbizwa hospitali. 

Waliofariki dunia ni Ally Abdallah Fundi (18), Mohammed Maganga na Kashinde Msigalo hats hivyo majina ya manusura hayakuweza kupatikana mara moja.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Fatma Nyangasa amesema baada ya taarifa za tukio, jitihada za uokoaji zilianza.

"Mwanzoni tulikuwa hatuna idadi kamili kwa sababu hakuna mtu aliyekuwa na uwezo wa kuthibitisha kuna watu wangapi huko chini, lakini tulipoongea na viongozi wa maeneo haya walituambia kuwa siku za mwisho wa wiki huwa hazina watu wengi," amesema Nyangasa na kuongeza.

...Jitihada zimefanyika za uokoaji na tumefanikiwa kutoa kifusi hadi kugusa mwamba na kutoa miili mitatu ya jinsia ya kiume na miili yao imehifadhiwa katika hospitali ya Vijibweni.”.

Hata hivyo aliwaomba wananchi wa maeneo hayo kuwa yeyote ambaye atakuwa na taarifa au kutomuona ndugu yake na anafanya kazi katika machimbo hayo atoe taarifa ili hatua nyingine za ufuatiliaji zichukuliwe.


"Lakini niwaombe wananchi wa eneo hili kutoendelea na shughuli za ugongaji kokoto, eneo hili limeshafungwa tangu 2018,” Nyangaza aliwasihi wananchi hao.


No comments:

Post a Comment