TAASISI ya Fire Kinder ya nchini Ujerumani imesaidia ujenzi wa jengo lenye vyumba vinne vya upasuaji kwenye hospitali ya Nkoaranga iliyopo Arumeru mkoani Arusha.
Aidha, wamefunga vifaa vya kisasa vya kidigitali kwa ajili ya kufanyia upasuaji ambapo vyote vimegharimu zaidi ya shilingi milioni 750 (Euro 300,000).
Pia, watoto matatizo ya kupinda mifupa na makovu ya kuungua moto yaliyowasababisha baadhi ya viungo kushindwa kufanya kazi wanafanyiwa upasuaji bure na madaktari wa hospitali hiyo wakishirikiana na madaktari na wauguzi 10 kutoka nchini Ujerumani.
Hayo yamesemwa April 5, 2022 na Mkuu wa Fire Kinder, Annemarrie Schraml na Mkurugenzi wa hospitali ya Nkoaranga, Dkt Samuel Kiwesa ambapo jengo hilo limezinduliwa rasmi April 1, mwaka huu na Askofu Elias Kitoi Nassari wa KKKT Daiyosisi ya Meru.
Kiongozi wa taasisi ya Fire Kinder, Annemarrie amesema wamefanikisha ujenzi wa jengo hilo kupitia mradi wao kusaidia Tanzania ambapo walianza ujenzi huo mwaka 2019.
"Chumba cha upasuaji (cha awali) hakikuwa kizuri, huduma haikuwa nzuri tukaamua kugharamia kusomesha madaktari watatu hapa Dkt Kiwisa ni mtaalam wa mifupa alisomea KCMC, pia Dkt Molel na Mungure," amesema Dkt Annemarie na kuongeza
...Dkt Kiwesa anafanya vizuri sana anafanyia upasuaji vijana wadogo wanaopata ajali za pikipiki ambao hupata shida kwenye mifupa,".
Akieleza namna alivyoweza kufanikisha ujenzi wa jengo hilo, Dkt Annemarie alisema kuwa ailiwaomba washirika wao nchini Ujerumani, marafiki na kampuni ya A heart for children wakawasaidia fedha zaidi kwa ajili ya ujenzi wa jengo hilo la upasuaji.
Amesema walianzisha taasisi ya Fire Kinder nchini Ujerumani baada ya kuona watoto wanapoungua na moto namna wanaweka mikono au miguu wakipona jeraha viungo hivyo vinakuwa vimeshikana na maeneo mengine ya mwili hivyo yanashindwa kurejea kama ilivyo awali hivyo wakaona wawasaidie watoto hawa kwa kuwafanyia upasuaji na kuwarejesha katika hali yao ya kawaida waweze kutumia viungo vyao kama kawaida.
Dkt Annemarie amesema kuwa wanatarajia kujenga jengo la wazazi kwani lililopo sasa ni la zamani hivyo haliko kwenye hali nzuri kwani wakati wa mvua linakuwa na changamoto zaidi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa hospitali ya Nkoaranga, Dkt Kiwesa aliishukuru taasisi ya Fire Kinder aliyosema imekuwa msaada mkubwa kwao tokea waanze urafiki mwaka 2000 ambapo wamekuwa wakipokea madaktari na wauguzi wanaojitolea kila mwaka.
Amesema kuwa kwa kipindi hicho kwa kushirikiana wameshafanyia upasuaji zaidi ya wagonjwa 2000 na wamefanya kazi nyingi za maendeleo katika hospitali ikiwemo kuwafungia mashine mpya ya x ray ya kidigitali, wamejenga jengo la X Ray, pamoja hilo jipya kwa ajili ya kufanya upasuaji
"Jengo lenyewe limejengwa kwa mtindo wa gorofa ingawa kwa hatua ya sasa wameanza na jengo la chini. Hili jengo lina vyumba vya upasuaji ni la kisasa sana pamoja na vifaa vyake na kila chumba kina vifaa vyake ikiwemo mashine ya nusu kaputi," amesema Dkt Kiwesa na kuongeza.
...Sasa hivi tuna vifaa vinavyotufanya tufanye upasuaji kwa kasi kubwa zaidi zamani kwa siku kwenye idara yangu ya mifupa tulikuwa tunaweza kufanya upasuaji sita au saba lakini kwa sasa kwa sababu tuna vifaa zaidi tunaweza kufanya upasuaji 10 au 12.
....Awali tulikuwa tuna vyumba viwili tu vya upasuaji lakini sasa tuna vyumba sita hivyo utaona kwa siku tunaweza kufanya upasuaji wagonjwa zaidi ya 18 mpaka 20,".
Dkt Kiwesa amesema kuwa hospitali ya Nkoaranga ina hadhi kama hospitali ya wilaya ila idadi ya upasuaji wanaofanya nying si hospitali zote zinaweza kufanya operesheni nyingi namna hiyo.
"Tunawashukuru sana wamekuwa marafiki wa kweli wa muda mrefu na wamekuwa na nia ya kuwasaidia watoto wenye matatizo hasa wenye vifundo vya miguu na ulemavu mwingine," amesema Dkt Kiwesa na kuongeza
...Dkt Annemarie amekuja (Nkiaranga) hii ni mara ya 35 tokea mwaka 2000 unaweza kufikiria mapenzi yake kwa hospitali yetu na watu wa Tanzania na hasa watoto wanaotoka maeneo yote ya Tanzania na wanawahudumia bure,".
Mkurugenzi huyo wa hospitali ya Nkoaranga amesema kuwa Fire Kinder pia imesaidia kusomesha baadhi ya madaktari wao jambo alilodai kuwa ujuzi huo umewajenga kwa maana ya wananchi kupata huduma kwa sababu unapomsomesha daktari au unapojenga jengo la upasuaji lengo ni wananchi wapate huduma bora na kwa urahisi zaidi.
Amesema kuwa wataalam wa hospitali ya Nkoaranga wameweza kupata mafunzo kwa vitendo nchini Ujerumani kabla ya mlipuko wa UVIKO 19 ambapo tayari makundi mawili yalishaenda kabla ya mpango huo kusitishwa.
Hata hivyo mwezi Mei mwaka huu wanatarajia kukutana mjini Moshi na taasisi za Ujerumani zinazofadhili sekta ya afya hasa mahospitali kuona changamoto zinazotukabili hasa kipindi hiki cha UVIKO 19 zitakavyoshughulikiwa ikiwemo kutejeshwa kwa safari hizo za mafunzo.
Naye muuguzi Msaidizi kutoka Ujerumani, Paula Scharrer alisema kuwa mazingira ya kazi yako tofauti na kwao hivyo wamekuja na vifaa tiba vingine ili kuwawezesha kufanya shughuli hizo kwa ufanisi zaidi.
“Vitu kama nguo za kuingia kwenye chupa cha upasuaji zinazotumiaka hapo hospitali ya Nkoaranga ni za kufua hivyo wao wameleta za kutumia na kutupa mara baada ya upasuaji wa mgonjwa mmoja unapokamilika,” amesema Paula.
Mtaalam wa sindano ya usingizi, (nusu kaputi) kutoaka hospitali ya Nkoaranga, Emmanuel Zablon alisema kuwa jengo hilo la kisasa pia lina vifaa na mashine za kisasa kwa ajili ya kufanya upasuaji ikiwemo TV inayoonyesha eneo la mwili wa mgonjwa wanalolifanyia upasuaji.
Mtaalam wa nusu kaputi kutoka Denmark ambaye yupo hospitali hapo kwa ajili ya kujitolea kwa wiki sita, Cathrine Garver alisema kuwa amepata ujuzi akiwa hospitalini hapo kwani yeye ni mwanafunzi hivyo amejifunza mengi hospitalini hapo.
Naye Muuguzi Msaidizi Mstaafu wa hospitali ya Nkoaranga, Adelina Nko amekuwa akijitolea kila kundi hilo la madaktari na wauguzi kutoka ujerumani wanapofika kufanyia watoto upasuaji wa mifupa.
![]() |
| Eneo la mapokezi ya wagonjwa kwenye jengo hilo la upasuaji |
“jengo hili la upasuaji ni zuri mno ukilinganisha na la awali hili lina mwanga na nafsi ya kutosha hata madaktari wanaweza kuwahudumia mgonjwa vizuri zaidi ,” amesema Nko ambaye alistaafu tokea mwaka 2015 ila amekuwa akishirikiana na madaktari na wauguzi hao kutoka Ujerumani kuwahudumia watoto kila wanapokuja nchini.






No comments:
Post a Comment