MHADHIRI wa Chuo Kikuu cha Mzumbe Kampasi ya Dar es Salaam ,Profesa, Honest Ngowi,(55) na dereva wake Innocent Gerson (33) mkazi wa Dar es Salaam wamefariki dunia leo Jumatatu Machi 28, 2022 baada ya gari walilokuwa wakisafiria kikazi kuelekeza Morogoro kudondokewa na kontena.
Kamanda wa Polisi mkoani Pwani, Pius Lutumo ameeleza ajali hiyo ilitokea saa 12.20 asubuhi na kusababisha vifo hivyo ambapo miili ya marehemu ilipelekwa kuhifadhiwa kituo cha afya Mlandizi.
Ajali hiyo ilihusisha magari matatu Scania , Noah na Toyota Land Cruiser na kwamba watu wawili pia walijeruhiwa ambao ni dereva wa lori, Raymond Kimaro (39) na dereva wa Noah, Abdalah Mohamed (33) na kusababisha uharibifu wa magari hayo.
RPC, Lutumo ameongeza kuwa chanzo cha ajali hiyo bado hakijajulikama ingawa uchunguzi wa awali unaonyesha ni uzembe wa dereva wa Scania anayedaiwa kuhama upande wake wa barabara na kugonga gari aina ya Noah na kupelekea kontena kuchomoka na kuliangukia Land Cruizer.
"Ni kweli ajali imetokea leo saa 12 alfajiri ikihusisha magari matatu aina ya Noah, Land Cruiser alilokuwa anasafiria yeye (Profesa Ngowi) na lori ambalo ndio chanzo cha ajali lilihama njia na kuiangukia Noah ubavuni kisha kuilalia gari ya Ngowi," amesema RPC, Lutumo.
Amesema hadi wanamtoa eneo la tukio alikuwa bado mzima ambapo alifariki akiwa njiani akiwahishwa Hospitali ya Rufaa ya Tumbi Mkoa wa Pwani.
Watu mbalimbali wamejitokeza kutoa salamu za rambirambi kwa njia mbalimbali ikiwemo wale walitumia mitandao ya kijamii wakimueleza kuwa alikuwa mtu muungwana na anayetoa ushirikiano kwa watu wote.
Vyombo mbalimbali vya habari vimemnukuu mdogo wa marehemu, Juvenalis Ngowi akiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Tumbi mkoani Pwani akisema walipokea taarifa ya kifo cha ndugu yake huyo asubuhi Machi 28 na kwenda kuangalia mwili wa marehemu ambao umehifadhiwa katika hospitali hiyo.
"Tumekuja hapa tumeingia mochwari tumeuona na kuutambua mwili wake, ni kweli amefariki. Basi tunapokea yale ambayo hatuwezi kuyabadilisha, tunamshukuru Mungu kwa kila jambo,” amesema Juvenalis.
Kuhusu taratibu zingine, amesema wanasubiri ndugu akiwemo mtoto wa marehemu aliyepo Nairobi, mke wa marehemu kutoka Iringa pamoja na ndugu wengine waliopo nje ya nchi ili waweze kuendelea na taratibu nyingine ambapo msiba wa Mhadhiri huyo uko nyumbani kwake Mbezi Makabe jijini Dar es Salaam.



No comments:
Post a Comment