SHAHIDI; SABAYA DIKTETA, KASABABISHA NIMEKAMATWA

Wistson Mwahomange, (kushoto) Enock Togolani na Lengai Ole Sabaya


SHAHIDI  wa saba wa utetezi, Watson Mwahomange, (27) kwenye  ya uhujumu uchumi inayomkabili, Lengai Ole Sabaya na wenzake sita, ameiomba Mahakama imuachie huru kwa kuwa kukamatwa kwake kulisababishwa na vitendo alivyofanya kiongozi huyo kwa mfanyabiashara Francis Mrosso.

Aidha ameeleza  Sabaya alikuwa dikteta na vitendo vilivyosababisha ahusishwe na kesi hiyo vilitokana na kulazimishwa na Sabaya na alitekeleza amri zake kwa kuhofia maisha yake.

Mwahomange anayejitetea mwenyewe mahakamani hapo ameyasema hayo leo Jumatano Machi 16, 2022 alipokuwa akimaliza kutoa ushahidi wake mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Patricia Kisinda anayesikiliza shauri hilo la uhujumu uchumi namba 27/2022 kwenye  Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha.


Mwahomange ameeleza kuwa Sabaya alikuwa dikteta kwake na uhusiano wao haukuwa mzuri kwa sababu alikuwa anamtaka afanye anachotaka, hali iliyomfanya kuwa na hofu wakati wote.


Fuatilia sehemu ya mahojiano hayo;


Wakili: Ni ukweli ulieleza katika ushahidi  wako wa msingi ulieleza ulipigiwa simu na Sylvester ufike Point Zone mkuu anakuhitaji?


Shahidi: Ni kweli nilieleza hivyo


Wakili: Ni ukweli neno mkuu lilimaanisha ni Lengai Ole Sabaya?


Shahidi: Ndiyo ni kweli


Wakili: Na ni ukweli umeeleza Sylvester alikuwa msaidizi binafsi wa Sabaya baada ya Lameck kuondoka?


Shahidi: Ni kweli nilieleza


Wakili: Lameck aliondoka lini kama unakumbuka?


Shahidi: Mwaka 2020


Wakili: Ulieleza ulivyofika Point Zone ulikuta magari yanaondoka?


Shahidi: Ndiyo nilieleza


Wakili: Na ni ukweli ulieleza 20/1/2021 baada ya kupata gharama za pump ulituma meseji kwa Lengai Ole Sabaya?


Shahidi: Ndiyo nilieleza


Wakili: Na baada ya muda ilisema ulitumiwa fedha hizo na Sylvester?


Shahidi: Ndiyo ni kweli


Wakili: Ni ukweli pia ulieleza baada ya kukufunga pingu Point zone waliondoka bila wewe kuwaelekeza wakafika gereji kwa Mrosso?


Shahidi: Ndiyo nilieleza


Wakili: Utakubaliana na mimi Lengai Ole Sabaya na watu aliokuwa nao walikuwa wanafahamu fika wanapoelekea bila wewe kuwaelekeza?


Shahidi: Ndiyo ni kweli nakubaliana na wewe


Wakili: Ni kweli walifika gereji kwa Mrosso 22/1/2021 bila wewe kuwaelekeza?


Shahidi: Ni kweli


Wakili: Ulieleza gereji ulimuona mtu anaitwa Macha


Shahidi: Ndiyo


Wakili: Ni muda gani?


Shahidi: Ilikuwa majira ya saa nane mchana 


Wakili:Katika ushahidi wako umeeleza Sabaya amekuwa akikutana na watuhumiwa wenzake Magereza wanaweka vikao katika zile tarehe Takukuru walikuwa wanakuja magereza?


Shahidi:Ndiyo ni kweli


Wakili:Na wewe ulikuwa mmoja wapo katika hivyo vikao?


Shahidi: Mimi nilitengwa


Wakili: Uliwasikia washitakiwa wengine wakitoa ushahidi wamesema hawamfahamu Lengai Ole Sabaya


Shahidi: Ndiyo niliwasikia


Wakili: Kwa nini unasema waliosema hawamfahamu ni waongo?


Shahidi: Kwa sababu nilikamatwa na Enock na ameleza mahakamani hamfahamu Sabaya, nilikamatwa na Sylvester na siku ya 22/1/2021 nilimuona Macha na yeye akasema hamfahamu Sabaya


Wakili: Utakubaliana na mimi si rahisi watu ambao hawafahamiani kukaa vikao Magereza na kupanga nini cha kusema mahakamani?


Shahidi: Nakubaliana na wewe


Wakili: Jana na juzi wakati ukiendelea kutoa ushahidi wako umeeleza aliyekuwa wakili wao alikuwa akija magereza na muda mwingi alitumia kuongea na Sabaya?


Shahidi: Ndiyo nilieleza hivyo


Wakili: Pia umeeleza kabla wakili wako hajasema hakuwakilishi ulikuwa ukimpa maswali ya kuuliza mashahidi wa jamhuri lakini alikuwa hayaulizi?


Shahidi: Ni kweli alikuwa hayaulizi


Wakili: Ni kweli umeeleza kwamba kabla wakili hajasema hakuwakilishi tena alikuelekeza nini cha kuja kusema katika utetezi wako?


Shahidi: Ndiyo alieleza


Wakili: Utakubaliana na mimi kuwa wakili alitaka uieleze mahakama yangekuwa ni uongo wa kupotosha mahakama?


Shahidi: Ni kweli kwamba alichokuwa ananiambia nije kusema kilikuwa cha kupotosha mahakama 


Wakili: Ulieleza Sabaya alikuwa akikupiga na ulikuwa mateka wake?


Shahidi: Ndiyo ni kweli nilieleza


Wakili: Utakubaliana na mimi kwa kipindi chote ulichokuwa ukipigwa na Sabaya alikuwa bado ni Mkuu wa wilaya


Shahidi: Ndiyo alikuwa bado ni mkuu wa wilaya


Wakili: Unakubaliana na mimi wakati Sabaya akitoa ushahidi kwa masikitiko alieleza ametumikia Taifa hili kwa uaminifu kwa muda wa miezi 32?


Shahidi: Ni kweli nilisikia akieleza


Wakili: Ni ukweli usiopingika yeye kama Mkuu wa wilaya alikuwa mtumishi wa umma?


Shahidi: Ni kweli alikuwa mtumishi wa umma


Wakili: Na kati ya majukumu yake mengi ni kuwa mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya?


Shahidi: Ni kweli alieleza


Wakili: Utakubaliana na mimi mtumishi huyu muaminifu hata kama ulikosea alipaswa kufuata sheria hakupaswa kukupiga


Shahidi: Ni kweli kabisa


Wakili: Utakubaliana na mimi katika kukupiga alikuwa akikufanyia udhalimu na unyanyasaji na alikuwa akikiuka kiapo chake cha utumishi wa umma?


Shahidi: Ni kweli nakubaliana na wewe


Wakili: Kwenye ushahidi wako ulieleza ulikuwa unampiga picha Lengai Ole Sabaya?


Shahidi: Ni kweli nilieleza hicho


Wakili: Ukaulizwa ulikuwa ukilipwa ukajibu alikuwa anakulipa


Shahidi: Alikuwa akinilipa kwa kazi


Wakili: Na utakubaliana na mimi 22/1/2021, watuhumiwa wote Sabaya akiwemo walieleza walikuwa maeneo tofauti na si gereji Mbauda kama ulivyoeleza?


Shahidi: Ni kweli


Wakili: Sasa kwa nini unaeleza uliwaona gereji wakati wao wanadai hawakuwepo akiwemo Sabaya, Macha na Enock?


Shahidi: Nakumbuka kwa sababu nilipelekwa na gari ya Sabaya na niliwaona pale ndani baada ya kupeleka pump 


Wakili: Ni kweli ulieleza gari VX Masai iliyokutoa Point Zone hadi gereji kwa Mrosso ilikuwa ikiendeshwa na Shukuru?


Shahidi: Ni kweli


Wakili: Ni kweli ulieleza ulitoroka na ukaacha hayo magari pale gereji


Shahidi: Ni kweli nilieleza


Wakili: Ni ukweli usiopingika baada ya kutoroka hufahamu nani aliendesha ile VX Masai?


Shahidi: Ni kweli sifahamu


Wakili: Uliulizwa maswali kuhusiana na mzigo ulioletwa na mtu mwenye benzi ni kweli Sabaya wakati anaongea na wewe hakusema ni mzigo gani?


Shahidi: Ni kweli


Wakili: Lakini ni kweli mzigo uliokufikia ni pump uliyotakiwa kwenda kuitengeneza?


Shahidi: Ndiyo ni pampu


Wakili: Na kweli pampu hii ndiyo uliyopewa 22/1/2021 na watu waliokuwa na Sabaya ukapeleka ofisini kwa Mrosso?


Shahidi: Ni kweli


Wakili: Na jana ulizungumzia kuhusu mtu anaitwa Mashala alikupigia simu


Shahidi: Ni kweli


Wakili: Huyu Mashala ni nani?


Shahidi: Mashala ni mpiga picha


Wakili: Kwa nini  awe na Sabaya akakupigia  simu?


Shahidi: Alinipigia baada ya kuona picha 'status' yangu


Wakili: Ulisema uligundua Sabaya ni mtu hatari 2020 kwa nini ulieleza hivyo?


Shahidi: Alikuwa ananipiga bila sababu na kuniweka 'lock up' bila sababu na kuninyima dhamana na hata ukimshitaki hakuna kinachofanyika


Wakili: Umeeleza alikuwa anakuweka 'lock up', alikuwa anakuweka 'lock up' wapi?


Shahidi: Sakina, Central Arusha, Sekei na wilayani Hai


Wakili: Jana uliulizwa baadhi ya majina ya watu kama wamefika kutoa ushahidi washitakiwa na mmoja  wao ni Shukuru na Saitabau ni kweli ulieleza hivyo?


Shahidi: Ni kweli nilieleza hivyo


Wakili: Utakubaliana na mimi wewe siyo mpelelezi wala unayeleta mashtaka mahakamani?


Shahidi: Ndiyo nakubaliana na wewe


Wakili: Na utakubaliana na mimi huna uelewa wowote kuhusiana na namna watu wanatakiwa washtakiwe au kuletwa kama mashahidi katika kesi?


Shahidi: Ndiyo nakubaliana na wewe


Wakili: Ulieleza uliyosema 16/9/2021 ilikuwa uongo, na unayoeleza sasa ni ukweli, kwa nini ulieleza uongo wakati wa hoja za awali?


Shahidi: Mimi ni mgeni niliambiwa na wakili wangu aliyekuwa ananiwakilisha utakapokubali utafungwa miaka 20, akaniambia kataa jina lako la Watson kubali jina la Henrick ambalo halijulikani ila baadaye ushahidi ulivyokuwa unaendelea nilimwambia wakili mimi nitaeleza ukweli


Wakili: Jana ulieleza shahidi namba mbili wa utetezi Jesca Nasari, kwanini ulisema ni muongo?


Shahidi: Nilisema hivyo kwa sababu wote tulikamatwa sehemu moja 27/5/2021


Baada ya shahidi kumaliza kuulizwa maswali ya dososo, Hakimu Kisinda alimweleza mshitakiwa huyo kuwa mahakama inahitaji ufafanuzi wa baadhi ya masuala aliyozungumzia katika ushahidi wake na wakati akiulizwa maswali ya dodoso.Sehemu ya mahojiano hayo ni ama ifuatavyo;


Hakimu: Umeeleza uhusiano wako na mshitakiwa namba moja haukuwa mzuri?


Shahidi: Ndiyo haukuwa mzuri


Hakimu: Ulikuwaje?


Shahidi: Nilikuwa nafanya anavyotaka, kitu kidogo anakupiga na kukupeleka polisi na anataka uwepo muda wowote ilikuwa huwezi kumkwepa


Hakimu: Huo uhusiano unaweza kuuelezea kwa neno moja tu?


Shahidi: Alikuwa dikteta kwangu


Hakimu: Mlivyokuwa mkifanya kazi pamoja ulikuwa na furaha?


Shahidi: Sikuwa na furaha na yeye kwa sababu alikuwa ananilazimisha nifanye anachotaka


Hakimu: Una chochote ambacho hukusema?


Shahidi: Naiomba mahakama iniachie huru


Hakimu: Je unajiona uko hapa kwa sababu ya mshitakiwa namba moja?


Shahidi: Ndiyo niko hapa kwa ajili ya matendo aliyotenda yeye


Hakimu: Kwa matendo aliyokufanyia au?


Shahidi: Kwa matendo aliyotenda kwa Mrosso


Hakimu: Nitakuwa sahihi ulikuwa na uhasama na mshitakiwa namba moja kwenye uhusiano wako?


Shahidi: Ilifika hatua nilikuwa nimemzoea nilikuwa nafanya anachokitaka


Hakimu: Lakini hamkuwa sawa


Shahidi: Ndiyo hatukuwa sawa 


Baada ya Mwahomange shahidi wa nane, Nathan Msuya ametia ushahidi wake ambapo upande wa utetezi ulifunga ushahidi wake.

Shauri hilo limeahirishwa mpaka Machi 31, mwaka huu litakapokuja kwa ajili ya  mahakama kutangaza tarehe ya kutoa hukumu.

0 Comments:

Post a Comment