Sunday, March 20, 2022

MBOWE KUTOA MILIONI 100 KUMALIZIA KANISA, KANISA LATANGAZA SIKU SABA ZA MAOMBI



MWENYEKITI wa Taifa wa CHADEMA, Freeman Mbowe ameweka  nadhiri kutoa shilingi milioni 100 kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa kanisa Usharika wa Nshara, Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kikutheri nchini,  (KKKT),  ikiwa ni sehemu ya kumbukumbu yake ya kukaa gerezani ukonga kwa miezi nane.


Aidha, Mchungaji kiongozi wa usharika huo, Rodrick Mlay ametangaza maombi ya siku saba kwa ajili ya kumshukuru Mungu kuwezesha Mbowe kuachiwa huru.

Wameyasema hayo  hayo leo Jumapili Machi 20, 2022 kwa nyakati tofauti wakati wakizungumza kwenye ibada ya shukurani ambayo  umati mkubwa wa watu walijitokeza kumsindikiza kiongozi huyo pamoja na familia yake.

 

 "Tutafanya maombi ya siku saba kuanzia kesho Jumatatu 12:00 jioni hadi saa 2:00 usiku, kuendelea kumshukuru Mungu kwa matendo yake makuu" amesema Mchungaji Mlay na kuongeza.

...Leo ni siku ya furaha kwa kuwa mwenzetu aliyekuwa kwenye mahangaiko amekuwa huru, tunaungana naye kumshukuru Mungu,".


Ibada hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Chadema , wachungaji, pamoja na Askofu mstaafu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini, Erasto Kweka.

Akiongea kanisani hapo, Mbowe amesema kuwa hakuna mahali watu wanamtaja Mungu kama jela kwani wanaamka saa 10 alfajiri wanaimba na kuabudu, na wengine wanajutia kwa makosa waliyoyafanya.

Hata hivyo amesema yeye hajutii kwa aliyopitia kwani anajua wazi yalikuwa ni makusudi ya Mungu huku akiweka nadhiri ya kujenga kanisa. 

"Binafsi nimeweka nadhiri kwamba, nitakwenda kutafuta kokote kule shilingi milioni 100 na Mungu atanaiongoza kupata, ili zimalizie ujenzi wa Kanisa la KKKT Usharika wa Nshara-Machame, ili iwe kumbukumbu yangu ya kukaa gerezani miezi 8 Ukonga na kisha kutoka," amesema Mbowe  na kuongeza.


...Tukilijenga vizuri hekalu hili la BWANA (Kanisa la KKKT Usharika wa Nshara-Machame), litatoa huduma kwa watu wengi hata wasio na haki, kupitia hekalu la Mungu watasikia neno la Mungu nao hatimaye wataijua haki,".


Mbowe ambaye amekuwa mbunge wa jimbo la Hai kwa mihula mitatu tofauti amesema kuwa kilio chao  kila siku ni kusimama katika haki na kweli, na hayo watayasimamia bila hofu. 

"Kikao changu cha kwanza baada ya kutoka gerezani kilifanyika Ikulu na Rais, niliwambia Rais Samia Suluhu Hassan kuwa hii nchi watu wengi mioyo yao inavuja damu," amesema Mbowe na kuongeza 


... Nilimwambia Rais kuwa, hofu zinazojengwa na wasaidizi wa watawala kwamba wana-CHADEMA katika nchi hii wanapenda vurugu na ni watu wasiopenda amani, ni maneno ya uongo,". 



Mbowe ambaye ni miongoni mwa waasisi wa CHADEMA amesema kuwa hawajawahi kuiombea serikali iliyoko madarakani ishindwe kutekeleza mambo yao ila wanawasimamia ili wafanye kazi zao kwa uadilifu mwisho wa siku watu wote wapate ustawi na ustawi wa Taifa ukipatikana hivyo  maisha bora kwa kila Mtanzania yataonekana.

"Ustawi wa Taifa ukipatikana, wana-CHADEMA au wasio na vyama, sote tutanufaika, na hili ndio jambo ambalo tunalihubiri kila siku," amesema Mbowe na kuongeza 

...Wanachama wa vyama vyote watangulize haki mbele, haki ya raia, haki ya Taifa, kila haki ina wajibu wake lakini ni dhahiri kwamba tukikubaliana sote tukutane kwenye haki, wala hatutagombana.

...Huwa najiuliza, katika suala la katiba hivi tunagombania wapi, na kwanini tugombane. Hawa wanasema wanataka katiba na hawa wanasema wanataka shule, kwani aliyesema anataka shule wapi alisema hataki katiba bora, tukae tuzungumze tofauti zetu ziko wapi,"

Mbowe na wenzake watatu walikuwa wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi na ugaidi ambapo walikuwa waanze kujitetea baada ya mahakama kuwaona wana kesi ya kujibu ndipo Machi 4, mwaka huu Mkurugenzi wa Mashitaka nchini, (DPP) akawasilisha hati ya kutokuwa na nia ya kuendelea na shauri hilo hivyo mahakama ikawaachia huru.










No comments:

Post a Comment