Aidha, kimesema kuwa hakitashirki mkutano wa Kituo cha Demokrasia Tanzania, TCD utakaofanyika Machi 30 na 31 mjini Dodoma.
Mkutano huo wa Dodoma unaoitwa kuwa wa maridhiano ya umoja wa kitaifa unatarajiwa kuhudhuriwa pia na Rais Samia Suluhu na Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi.
''Kwenye hoja zinazowasilishwa hatuoni suala la katiba, tunaona kuna mkakati wa kuua suala la Katiba, sasa sisi hatuwezi kushiriki,"amesisitiza Mbowe.
Mbowe ameeleza kuwa Chadema haijashirikishwa kwenye masuala yaliyopo kwenye ripoti ya TCD ambayo inaamini imeweka kando kipaumbele muhimu cha suala la katiba mpya.
"Nimemwambia mheshimiwa Rais process (mchakato) yoyote ya upatanisho lazima itanguliwe na ukweli", amesema Mbowe na kuongeza.
..Tunakwenda kuridhiana tulikosea wapi? Wahanga wakubwa wa maamuzi hayo ni Chadema, sisi ndio watu ambao tumepitia tabu hizo kuliko wote, viko vyama vya siasa vinasema uchaguzi ulikuwa wa haki, sisi tumetengwa na tumetengwa kwa muda mrefu, nimemwambia mheshimiwa rais kwanza ukweli kisha upatanishi".
Mbowe ameongeza pia maazimio ya TCD yana lengo la kuwaondoa kwenye kipaumbele cha katiba mpya.
WENGI WANASOTA MAGEREZA
Amesema kuwa Pamoja na kazi kubwa inayofanya polisi nchini Tanzania, lakini kuna uovu mkubwa pia unaofanywa na polisi hao.
Amesema kuwa kuna watu wengi ambao wapo kwenye magereza na mahabusu lakini kwa kukosa msaada wa kisheria wanakaa muda mrefu bila kupata haki.
"Mimi kabla ya kwenda gerezani niliwekwa lupango kwa siku tano, kule ndani kulikua na vijana karibu 40, wamekaa kwa wiki tatu, hawana mwanasheria hawana msaada wowote wa kisheria," amesema Mbowe.
Amesema mbali na madhila aliyopitia akiwa gerezani lakini kuna mazuri amejifunza na kuwa hajapoteza muda bure.
''Sikupoteza siku ambazo nilikua gerezani, nimejifunza mengi sana, nimejiimarisha kifikra, kimtazamo na hata moyo wangu umebadilika sana," ameeleza Mbowe.
Kauli hiyo ya Mbowe imekuja siku chache baada ya chama tawala, CCM, kulitaka jeshi la polisi nchini kujitathmini kutokana na mwenendo wa matukio kuhusisha jeshi hilo.
Mbowe amesema kuwa chama chake wamekua wakilaumu jeshi la polisi kwa muda mrefu na anashangaa kwanini kiongozi wa jeshi hilo hajajiuzulu.
''Hii ni kauli sisi tumeihubiri miaka na miaka, nashangaa Sirro, (IGP Simon) bado yupo ofisini, chama tawala kinasema jeshi la polisi hili lijitathmini , wewe IGP bado uko ofisini? Inatakiwa siku ya pili yake ujiuzulu," amesisitiza Mbowe.
Mbowe na wenzake watatu walikuwa wakikabiliwa na kesi ya ugaidi na uhujumu uchumi, ambayo ilisababisha wakae mahabusu kwa zaidi ya miezi saba gerezani ambapo baadae kesi hiyo ilifutwa na mwendesha mashtaka wa serikali, (DPP).
HATUJATEUA WABUNGE 19
Mbowe amesema kuwa Spika wa Bunge ameshaandikiwa barua na anajua wabunge 19 wa viti maalumu sio wabunge walioteuliwa na chama hicho.
Amesema Baraza Kuu litakaa mwezi ujao tarehe 25 na kama kuna rufaa zao basi zitaonekana .
" Chadema haijawahi kuteua Kamati Kuu na ninarudia tena leo Chadema haijawahi kuteua wabunge wa viti maalumu," amesema Mbowe.
Kamati kuu ya CHADEMA ilifikia makubaliano kadhaa ikiwemo kutoshiriki kwenye masuala ya TCD, ambayo ni muungano wa vyama vya siasa vye uwakilishi bungeni, na vyama vingine vinavyoshiriki kama wajumbe washiriki.
0 Comments:
Post a Comment