Mkutano
wa 19 wa wakuu wa nchi za jumuiya ya Afrika Mashariki unafanyika leo Machi 29,
2022 huku ajenda kuu ikiwa ni kuiidhinisha rasmi nchi ya Jamhuri ya
kidemokrasia ya Congo kuwa mwanachama mpya wa jumuiya hiyo kongwe barani Afrika.
Congo iliomba kujiunga na jumuiya hiyo tangu
mwezi Februari mwaka 2021 na mamlaka husika zilikuwa bado zinapitia ombi hilo
kwa kuzingatia mkataba wa kuanzishwa kuwa jumuiya ya Afrika Mashariki.
Awali
katika mkutano wa 18 wa wakuu wa nchi uliofanyika mwaka jana , katibu mkuu wa
jumuiya ya Afrika Mashariki Dr. Peter Mathuki alibainisha kuwa
mwezi Machi mwaka huu hatua zote za Congo kujiunga na jumuiya hiyo, zitakuwa
zimekamilika.
Kikao kilichotangulia cha baraza la
mawaziri wa jumuiya hiyo , kimependekeza kwamba wakuu wa nchi katika
mkutano wao wa leo, wazingatie ripoti ya timu ya uhakiki kuhusu maombi ya
jamhuri ya kidemokrasi ya Congo ya kujiunga na jumuiya hiyo.
Katibu mkuu wa umoja wa mataifa Antonio
Guterres aliwahi kutoa wito kwa nchi duninai kuimarisha ushirikiano wa
kimataifa wa kikanda na hata kiulimwengu, na hivyo jumuiya ya Afrika Mashariki
inachukua wigo wa kupanua uanachama wake kutoka nchi sita hadi kufikia saba.
Pamoja na mambo mengine, mkataba wa
kuanzishwa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki unaeleza kuwa, nchi nyingine
inaweza kujiunga na Jumuiya hiyo iwapo itaungwa mkono na nchi wanachama na
iwapo nchi hiyo inayoomba itakuwa imetimiza masharti yafuatayo ya uongozi bora,
Demokrasia, inaheshimu sheria, inasheshimu haki za binadamu, na kwamba iwe
jirani na mojawapo ya nchi wanachama.
Mpaka sasa jumuiya ya Afrika Mashariki
inaundwa nan chi sita, ambazo ni Kenya, Tanzania, Burundi, Rwanda, Uganda na
Sudan kusini iliyojiunga mwaka 2016.
Maamuzi hayo yanakuja kufuatia
mapendekezo ya kikao cha baraza la mawaziri kilichoketi tarehe 25 Machi kwamba
Congo imekidhi vigezo vya kujiunga na jumuiya hiyo kongwe barani Afrika.
WAKUU
wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, (EAC), wameidhinisha kuingizwa kwa Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo katika umoja huo.
Wamefikia
muafaka huo katika mkutano wao wa kilele uliofanyika leo Machi 29,2022 kwa njia ya mtandao ambapo baada ya Kongo
kujiunga na jumuiya hiyo inakuwa na nchi saba.
"Waheshimiwa
maraisi ninapenda kutumia fursa hii kuwashukuru sana kwa kunikaribisha katika
mkutano huu maalumu ambapo kwa mara ya kwanza ninazungumza kwa niaba ya
wananchi wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo kama mwanachama mpya wa jumuiya ya
Afrika Mashariki,” amesema rais Tshisekedi.
Pamoja
na mambo mengine Tshisekedi amesema anatarajia kwamba kuwa ndani ya jumuiya ya
Afrika Mashariki kutaisaidia nchi yake kuwa na ulinzi na usalama hasa eneo la
Mashariki mwa Congo ambalo linakumbwa na machafuko.
Wachambuzi
wa masuala ya kimataifa wanadai kuwa Kongo imekuwa mwanachama rasmi wa EAC
lakini hakuna mengi yanayoweza kubadilika mara moja.
Taifa la Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo lipo kusini mwa jangwa la
Sahara lina watu wanaofikia milioni 90 na ni taifa la pili kwa
ukubwa barani Afrika baada ya Algeria iliyoko kaskazini mwa Afrika.
Katika
kikao cha leo, wakuu wa nchi kwa pamoja
wameikaribisha Congo na kuonesha matarajio ya kila upande kufaidika, Kama
anavyoeleza Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.
"Tanzania
inasema karibu sana DRC. Ni matumaini yangu kwamba DRC inauharakisha mchakato
wa kukamilisha makubaliano yaliyo katika mkataba wa kujiunga, ili kuwapa
wananchi wake fursa ya kufurahia matunda ya
jumuiya. Maamuzi yenu ya kujiunga na jumuiya yatasaidia kupatikana na amani na
ulinzi, umoja na mshikamano sio tu Congo bali kwa jumuiya nzima kwa ujumla.” Amesema
Samia.
Kwa sasa Jumuiya ya Afrika Mashariki
imepanuka kutoka umoja unaoundwa na nchi sita na kuwa saba hivyo unatarajiwa
kuwa wigo mpana zaidi wa kibiashara kuanzia bahari ya hindi mpaka ya atlantiki.
Katibu Mkuu wa EAC, Peter Mathuki amesema amefurahi
sana huku akitoa wito wa kuondolewa kwa vikwazo vyote vya kibiashara
baina ya nchi wanachama.
"Sisi ni majirani na DRC, lakini
hatufanyi biashara nayo sana kwa sababu tu hakuna mfumo. Bidhaa nyingi
zinazokuja DRC zinatoka nje ya Afrika Mashariki kama vile Zambia na Asia,"
Mathiki amewaeleza waandishi wa habari mara baada ya kikao hicho cha wakuu wa nchi
na kuongeza.
…Kwa hiyo, tunatazamia kuweka utaratibu ambao
utahakikisha biashara kati yetu na DRC inaimarika." Amesema Mathuki
Wabunge wa Kongo bado wanapaswa kuidhinisha sheria na
kanuni za EAC kabla ya kuanza kutumika.
Raia wa Kongo wanaotaka kutembelea nchi
nyingine wanachama - Burundi, Kenya, Rwanda, Sudan Kusini, Tanzania na Uganda -
bila visa wanaweza kuhitaji kusubiri kwa muda mrefu zaidi kwa sababu
ushirikiano kamili katika EAC unaweza kuchukua miezi au hata mwaka.
Sudan Kusini ilichukua muda wa miezi minne kutoka kwa
mkataba wa jumuiya mwezi Aprili 2016 hadi kuwa mwanachama kamili wa EAC mwezi
Agosti mwaka huo.
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ilituma maombi ya
uanachama mwaka wa 2019, ikitumai kuboresha uhusiano wa kibiashara na kisiasa
na majirani zake wa Afrika Mashariki.
Kongo inapakana na wanachama wote wa EAC isipokuwa Kenya,
na inatumai kuvutia wawekezaji zaidi kutoka kanda hiyo hivyo kujiunga na EAC kunaipa nchi hiyo ufikiaji bora wa vifaa kama
vile bandari za Bahari ya Hindi za Dar es Salaam na Mombasa.
Kinadharia, nchi za Afrika Mashariki zinaweza kupata
ufikiaji wa Afrika Magharibi na Bahari ya Atlantiki kupitia DR Congo, lakini
mitandao ya barabara na reli ya nchi hiyo itahitaji kuboreshwa kwa kiwango
kikubwa kwanza.
Njia pekee ya
kuvuka nchi hii kubwa, ambayo ni theluthi mbili ya ukubwa wa Ulaya Magharibi,
kwa sasa ni kwa ndege.
Upanuzi huu unaowezekana wa uhusiano wa
kibiashara kutoka Bahari ya Hindi hadi Atlantiki utasaidia kupanua uwezo wa
kiuchumi wa kanda wakati ambapo bara hili linafanya kazi ya kutekeleza Mkataba
wa Biashara Huria wa Bara la Afrika (AfCFTA)
Kwa sasa Kiingereza na Kiswahili ndizo lugha rasmi za
Jumuiya ya Afrika Mashariki, ingawa kumekuwa na mazungumzo kuhusu kuanzisha
Kifaransa, ambacho kinazungumzwa nchini Rwanda na Burundi.
Lugha rasmi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Kongo ni Kiswahili, Kifaransa, Kilingala, Kituba (Kikongo) na Tshiluba ambapo wataalamu
wanasema asili ya lugha nyingi katika eneo hili inapaswa kuangaliwa kama fursa
na sio kizuizi.
Kumekuwa na msukumo wa kukuza matumizi makubwa ya
Kiswahili, hasa baada ya Umoja wa Afrika kukipitisha kama lugha rasmi ya kazi
mwezi Februari 2022.
Hata hivyo, baadhi ya mikoa kama vile Magharibi mwa
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na sehemu za mataifa mengine ya EAC
haizungumzi kiswahili

No comments:
Post a Comment