Monday, March 28, 2022

JITIHADA ZA KUFUATA KANUNI ZA KUKABILIANA NA UVIKO 19 NCHINI ZAONGEZA IDADI YA WATALII


SEKTA ya utalii nchini imeanza kuinuka baada ya kukumbwa na athari zitokanazo na ugonjwa wa UVIKO 19 ambapo kwa mwaka 2021 kumekuwa na ongezeko la asilimia 48.6 la watalii wa kimataifa waliotembelea nchini huku mapato yatokanayo na sekta ya utalii yakiongezeka kwa asilimia 76.

  

Hayo yasemwa Machi 28,2022  jijini Arusha na Katibu Mkuu wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt Francis Michael wakati akizindua mafunzo ya upangaji wa madaraja wa  na upimaji ubora wa huduma za malazi na chakula Chuo cha Taifa Cha Utalii, (NCT) kampasi ya Arusha.



Katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Mkurugenzi wa Utalii, Wizara ya Maliasili na Utalii, Philip Chitaunga, Dkt. Francis amesema kuwa baada ya dunia kukumbwa na janga la UVIKO 19 idadi ya watalii wanaofika nchini ilishuka kwa asilimia 59.3 na mapato yalishuka kwa asilimia 72.5.

 

“Lakini janga na UVIKO 19 limeiathiri sekta hii kama ilivyotokea kwenye nchi nyingine duniani kote, lilisababisha watu wasisafiri kwani utalii unahusisha kusafiri sasa watu waliacha kusafiri, ndege zikaacha baadhi ya safari zake kila kitu kilisimama,” amesema Dkt,Francis na kuongeza.

 

…Sisi kama nchi masoko yetu ya utalii nayo yaliathirika  kwani watu walikuwa hawaji Tanzania na biashara zetu zilianguka, hoteli nyingi zilifungwa biashara za utalii ziliathirika idadi ya watalii ilishuka kwa asilimia 59.3 na mapato yalishuka kwa asilimia 72.5. hii ni anguko kubwa sana,”.

 

 

Hata hivyo amesema  Serikali kwa kushirikiana na na sekta binafsi walichukua hatua mbalimbali kuhakikisha wanarejesha sekta ya utalii katika hali yake ya kawaida miongoni mwa mambo yaliyofanyika ni kuandaa muongozo ulioiongoza sekta ya utalii kufanya shughuli zake wakati wa janga la UVIKO 19.

 

“Tuliandaa ‘Standard Oparating Procedure’, tuliandaa mpango wa kurejesha utalii katika hali yake ya kawaida, tuliandaa mafunzo kwa wale ‘front liners’ wote kwenye hii sekta,” amesema Katibu mkuu huyo akieleza namna walivyofanikiwa kuongeza idadi ya watalii nchini na kuongeza

 

…Hii ilitusaidia sana, shirika la kimataifa linalosimamia utalii na usafiri ‘World Tourism and Travel council’ liliipatia Tanzania ‘safe travel stamp’  kueleza kuwa Tanzania ni sehemu salama ambayo watu wanaweza kusafiri.

 


…Hii iliwezesha watalii kujenga imani na sisi hivyo hata wakati wa UVIKO 19 watalii waliendelea kutembelea Tanzania  ambapo mwaka 2021 tumekuwa na ongezeko la asilimia 48.6 la watalii wa kimataifa waliotutembelea nchini,”

 

Dkt Francis amesema hapa nchini kwenye mpango wa utoaji chanjo ya UVIKO 19  sekta ya utalii imekuwa miongoni mwa sekta zilizopewa kipaumbele ndiyo sababu wamepatiwa fedha za kutoa mafunzo hayo yatakayosaidia kuboresha viwango vya huduma za sekta ya utalii hivyo kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi shindani katika kuboresha huduma na hivyo kujenga imani kwa wageni wanaokuja nchini.

 

“ Mpango wa maendeleo na ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya UVIKO 19 tumepata fedha hizi zinazotumika kutoa mafunzo haya yatakayosaidia kuboresha utendaji wa sekta hiyo na kufikia malengo ya kupokea watalii milioni 5 ifikapo mwaka 2025 kama ilani ya chama tawala, (CCM) inavyoeleza,” amesisitiza Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Maliasili na Utalii.

 

Amesema sekta vya utalii ina mchango mkubwa sana katika uchumi wa nchi wa nchi kwani kabla ya janga la Uviko 19 mwaka 2019 sekta hiyo ilikuwa ikichangia asilimia 17 ya pato la Taifa sawa na dola za Marekani bilioni 4.2 kwenye pato la Taifa na  imekuwa ikichangia asilimia 25 ya mauzo yote ya nje yanayohusu huduma.

 

“Lakini pia imekuwa ikitoa ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja milioni 1.6 kama ambavyo mnafahamu sekta ya utalii huwa inachochea maendeleo ya sekta nyingine. Sehemu ambayo utalii umekua na shughuli nyingine za kibiashara zimekua,” amesisitiza Dkt. Francis na kuongeza.

 

Sekta ya utalii imekuwa muhimu katika kukuza uchumi, kutoa ajira na maendeleo mengine kwa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

 

 


Akizungumzia juu ya mafunzo hayo yanayotolewa kwa washiriki 44, Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Maliasili na Utalii amesema kuwa ameambiwa mtaala utakaotumika ni ule uliopitishwa na  Jumuiya ya Afrika Mashariki, (EAC)  hivyo wasahihishaji wa mitihani si lazima wawe wakufunzi waliowafundisha  hapo bali  wanaweza kutoka kwenye nchi yoyote mwanachama.



“Hii siyo semina hii ni shule tunatarajia mnasoma ili mfaulu itakuwa ni aibu sana kwamba umekaa hapa miezi miwili halafu unatoka hapa unarudi nyumbani  umefeli. Si kitu ambacho sisi tunakitarajia,” amesema Chitaunga akisoma hotuba hiyo ya Katibu Mkuu wa wizara ya Maliasili na utalii na kuongeza.



…Tupambane tuhakikishe yale wakufunzi wetu watatupatia tutayaweka vizuri kichwa mwetu tuweze kuhakikisha kwamba sisi wote 44 tulioanza mafunzo haya tumefauli.



…Mafunzo haya pamoja na kulenga katika ukarimu lakini pia yatahusisha maeneo mengine ya utoaji huduma kama vile ubora wa  mazingira , usalama mahali pa kazi, masuala ya ajira, bima, ulinzi na usalama. 

 

…Ninawasihi Chuo Cha Taifa Cha Utalii ambao ndiyo wanatoa mafunzo husika na wadau wengine watakaohusika kutoa mafunzo hayo kuhakikisha wanatoa maelezo muhimu kwa washiriki ili waweze kuelewa umuhimu wa kila jambo katika yale wanayofundishwa.

 


Awali, Mkurugenzi wa NCT, Dkt, Shogo Mlozi ameishukuru EAC, Sekretarieti ya Uzalishaji na Jamii kwa kuwezesha kitengo chake cha usimamizi wa upangaji wa madaraja na upimaji ubora wa malazi na chakula kwa kuweza kuratibu mafunzo hayo kwa kushirikiana na NTC.

 

Amesema NTC inatoa mafunzo ngazi ya cheti na diploma ambapo wana matawi manne nchini likiwemo hilo la Arusha, Mwanza na mawili jijini Dar es Salaam.

 

“NTC kwa sasa imepewa jukumu la kuendesha mafunzo ya aina mbili  kupitia mpango wa maendeleo kwa ustawi wa Taifa na makabiliano ya UVIKO 19 na Wizara yako unayoisimamia,” amesema Dkt Mlozi na kuongeza.

 

 

…Kama chuo tumeshamaliza mafunzo ya awamu ya kwanza tuliyopewa ambayo ilikuwa ni mafunzo ya kuwaongezea ujuzi wadau muhimu katika mnyororo wa Utalii katika mikoa nane Tanzania Bara ambapo jumla ya washiriki 1,200 wamenufaika na mafunzo hayo,”.

 

Mkurugenzi huyo wa NCT amesema washiriki hao walitokea mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma, Njombe, Iringa, Mbeya, Mara na Mwanza ambapo mafunzo hayo yalitolewa kwa watu kati ya 100 na 150 kwa kila mkoa kulingana na ukubwa wa eneo.

 

Dkt Mlozi amesema kuwa mafunzo ya sasa  ni awamu ya pili ambayo ni ya upangaji madaraja na upimaji wa ubora wa huduma za chakula na malazi yanatolewa kwa washiriki 44 kati yao 14 wanatoka kwenye sekta binafsi na 30 kutoka sekta ya umma.

 

“Mafunzo haya yanaenda kutolewa na wataalam wanaotambulika na EAC ambayo kwa hapa nchini ni wachache sana wako mama Salama Kibogoyo, Joseph Ntimba, Franline Mwinyimbegu, Kemirabi Kibogoro na Burhan Hassan,” amesema Dkt Mlozi na kuongeza.

 

“Aidha mafunzo hayo yataambatana na mafunzo ya wakufunzi wa wataalam saba  ambao walishiriki mafunzo ya wataalam wa upangaji wa huduma za malazi katika ubora mwaka 2011 ambapo mafunzo yao yatakiwa ya wiki nne,”.

 

 

Dkt Mlozi amesema taratibu za utoaji huduma za chakula na malazi wakati huu wa janga la UVIKO 19 zimebadilika ambapo mabadiliko haya yanatakiwa kuzingatiwa katika upangaji wa madaraja na upimaji wa ubora wa chakula na malazi hivyo kufanya mafunzo haya kuwa ni ya muhimu sana kutolewa nyakati hizi ambazo kama nchi na dunia tunaendelea kukabiliana na janga hili la UVIKO 19.

 

“Mafunzo haya yamelenga kuandaa wataalam ambao wataenda kutoa weledi kwa watoa huduma juu ya namna mpya ya kuendesha biashara ya utalii na kusaidia kuinua viwango vya ubora katika sekta ya utalii nchini,” amesema Dkt Mlozi na kuongeza.

 

…Hii itasaidia kuonyesha Tanzania imejiandaa vema katika kuhakikisha wageni wa ndani na wa nje wanapata huduma zenye ubora kama inavyotarajiwa na kamba ambavyo Tanzania imewekwa kwenye ramani ya dunia kama sehemu salama ya kutembelea,”.

 

 Kwa upande wake, Katibu Tawala mkoani Arusha, (RAS), Dkt Athuman Kihamia aliyewakilishwa na Afisa elimu mkoani hapa, Abel Ntupwa aliwahimiza washiriki hao mara watakapohitimu wakatekeleze majukumu yao kwa kuzingatia maadili ikiwemo kutunza siri na kuepuka vitendo vya rushwa.

 

 

Naye Afisa anayeshughulikia Masuala ya Utalii kutoka Sekretarieti ya EAC,  Dkt. Simon Kiarie ameipongeza Tanzania kwa kuwa mstari wa mbele katika kutekeleza mapendekezo yaliyotolewa na jumuiya hiyo katika kukabiliana na athari za UVIKO 19 kwenye sekta ya utalii.

 

Akiongea kwenye mkutano huo kwa njia ya mtandao amesema kuwa UVIKO 19 ulisababisha idadi ya watalii wanaotembelea ukanda huu kushuka kwa asilimia 70 kutoka watalii milioni 7 mpaka watalii milioni 2.26 kwa mwaka.

 

Kiarie amesema nchi wanachama wanapaswa kufanya juhudi za pamoja kuhakikisha wanarudi kwenye idadi ya awali ya wastani wa watalii milioni 7 waliokuwa wakitembelea vivutio vilivyo kwenye ukanda huu.

 

Amesem kuwa EAC iliweka mipango kadhaa ya kuinua utalii ikiwemo kuanzisha maonyesho ya utalii ambapo aliipongeza Tanzania kwa kuyafanya jijini Arusha mwaka jana.

 

Kiarie amesema kuwa Tanzania imekuwa nchi ya kwanza kwenye nchi zinazonda EAC  kutoa mafunzo hayo ya usimamizi wa upangaji wa madaraja na upimaji ubora wa malazi na chakula Suala la ubora wa huduma na chakula ni mambo ambayo ni miongoni mwa masuala yaliyoazimiwa na EAC.

 

 








 

No comments:

Post a Comment