MAHAKAMA ya hakimu Mkazi Arusha imepanga kutoa uamuzi kwenye kesi ya uhujumu Uchumi inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake sita Mei 31, mwaka huu.
Aidha, Mshitakiwa wa tatu, Watson Mwahomange ambaye kwenye shauri hilo alikuwa akijitetea mwenyewe ameshindwa kufika mahakamani hapo kutokana na kuugua akiwa mahabusu huku mahakama ikimpa siku moja kusaini hoja za majumuisho zilizowasilishwa kwa maandishi.
Hakimu Mkazi Mwandamizi, Patricia Kisinda anayesikiliza shauri hilo namba 27/2021 alipanga tarehe hiyo leo Machi 31, 2022 baada ya mawakili wa pande zote kuwa wamewasilisha hoja zao za majumuisho kwa maandishi na mshitakiwa, Watson ambaye ametakiwa kuzisaini na kuzirejesha mahakamani kesho.
“Mshitakiwa wa tatu, (Watson Mwahomange) ambaye hajasaini hoja zake za majumuisho nampa siku moja kufanya hivyo kesho (leo) awe amesaini na kuzileta mahakamani, kesi itatajwa April 13 kwa sababu washitakiwa wako mahabusu hukumu Mei 31, 2022,” amesema Hakimu Kisinda akiahirisha shauri hilo.
Awali, askari magereza, Inspekta Ramadhan Misanga ameieleza mahakama hiyo kuwa mshitakiwa wa tatu, Mwahomange anaumwa hajafika mahakamni hapo huku akieleza kuwa wana hoja zake za majumuisho za maandishi ambazo hazijasiniwa hivyo akaomba apewe muda ili ampelekee gerezani akazisaini.
“Mheshimiwa hakimu taarifa za mahabusu namba tatu Watson Mwahomange tunazo sisi maafisa wa magereza kwamba leo hatujaja ane tumemuacha gerezani akiwa anaumwa,” amesema Inspekta Misanga na kuongeza.
…Mimi asubuhi niliitwa na mganga mkuu wa gereza akanipa taarifa za kuumwa kwake amenipa cheti alichoandika yeye daktari ili nije nacho mahakamani ili maneno ninayotoa yabarikiwe ili yawe na uthibitisho wa daktari,”.
Hakimu Kisinda akaomba hicho cheti akakiangalia kisha Inspekta Misanga akaendelea kuieleza mahakama hiyo kuwa ana hoja za majumuisho za maandishi za mshitakiwa huyo ambazo hazijasainiwa.
“ Kwa hiyo tunaiomba mahakama, itupe muda baada ya hapa tukamsainishe ili ziweze kuletwa mahakamani,” alieleza Inspekta Misanga.
Kwa upande wa Jamhuri Wakili wa Serikali Mwandamizi, Felix Kwetukia alieleza mahakamani hapo kuwa waliwasilisha hoja zao za majumuisho jana asubuhi huku wakili wa utetezi Faudhia Mustafa akisema hoja zao waliziwasilisha Machi 30, mwaka huu.
Kwenye shauri hilo linalovuta hisia za wengi Sabaya pamoja na Enock Nkeni, (41) maarufu Dikdik, Watson Mwahomange, (27) maarufu Mamimungu,John Aweyo, maarufu Mike One, Silvester Nyengu, (26) maarufu Kicheche, Jackson Macha, (29) na Nathan Msuya, (31) wanakabiliwa na mashitaka ya kuongoza genge la uhalifu, kujihusisha na vitendo vya rushwa, utakatishaji fedha na matumizi mabaya ya madaraka.
Awali, ilidaiwa mahakama hapo kuwa washitakiwa hao waliyafanya makosa hayo Januari 21, 2021 katika eneo la kwa Mrombo jijini Arusha.
Kwenye shauri hilo, Sabaya peke yake anakabiliwa na makosa matatu ikiwemo matumizi mabaya ya madaraka alipokuwa mkuu wa Wilaya ya Hai huku washtakiwa wengine wote wanakabiliwa na makosa mengine mawili ya kuongoza genge la uhalifu na utakatishaji fedha.
Makosa hayo wanadaiwa waliyafanya Januari 21, 2021 katika eneo la kwa Mrombo jijini Arusha ambapo katika kosa la kwanza linalowakabili washtakiwa wote saba ni kuongoza genge la uhalifu, la pili linalomkabili Sabaya peke yake ni kujihusisha na vitendo vya rushwa na la tatu linalomkabili Sabaya pia ni kujihusisha na vitendo vya rushwa ambapo anadaiwa kuchukua Sh90 milioni.
Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa kosa la nne linalomkabili Sabaya mwenyewe ni matumizi mabaya ya madaraka huku kosa la tano linalowakabili wote saba likiwa ni utakatishaji fedha ambapo wanadaiwa kupata Shilingi 90 milioni huku wakijua kupokea fedha hizo zao la kosa la vitendo vya rushwa.
Katika kesi hiyo inayovuta hisia za wengi upande wa Jamhuri ulileta jumla ya mashahidi 13 na vielelezo 12 ambapo awali waliahidi kuleta mashahidi 20 mahakamani hapo huku upande wa utetezi ukileta mashahidi nane akiwemo mke wa Sabaya, Jesca Nassary na washitakiwa wote saba kila mmoja akijitetea ingawa awali waliahidi kuleta zaidi ya mashahidi 10.
Mashahidi Mashahidi wa Jamhuri ni pamoja na Mkurugenzi msaidizi anayesimamia utawala wizara ya fedha na mipango, Renatus Msangira, (45), Kaimu meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Arusha, Kayobyo Majogolo(41).
Wengine ni mwangalizi wa geti (mlinzi) na mfanyakazi kwa Mrosso,Adanbest Peter Marandu(61), pamoja na Philemon Tilatwa Kazidila,(64), Juma Nuhu, (28) na Mfanyakazi wa Benki ya CRDB, Geofrey Nko.
Mashahidi wengine wa Jamhuri, afisa uchunguzi wa kielektroniki kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini,(TAKUKURU) Johnson Kisaka, Meneja Benki ya CRDB tawi la Kwa Mromboo, Mary Mayoka Kimasa(40) na mmiliki wa Moroso Injector pump, Frances Mrosso.
Wengine ni dalali wa magari kutokea jijini Dar es Salaam, Sabri Abdallah Sharif ,(36), Meneja wa ulinzi na ushirika wa vyombo vya ulinzi na usalama Vodacom PLc,Tegeta DSM James Lisao Wawenje(39) na Afisa uchunguzi wa TAKUKURU, Ramadhani Rajab Juma, (39)

0 Comments:
Post a Comment