WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro anatarajia kuongoza zaidi ya wananchi 300 kupanda mlima Kilimanjaro ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 60 ya uhuru wa Tanzania Bara.
Ameyasema hayo leo Novemba 21,2021 jijini Arusha wakati akieleza namna wizara hiyo kwa kurikiana na kampuni ya uwakala wa utalii ya Zara walivyojipanga kushirikiana na wananchi katika kusherekea siku hiyo.
Amesema tayari wananchi 120 wamethibitisha kupanda mlima huo kuanzia Desemba 5, mwaka kwa kutumia kampuni ya uwakala wa utalii ya Zara ya mjini Moshi.
Amesema kuwa wamejipanga kusherekea siku hiyo kwa njia tofauti kwenye maeneo mbalimbali hapa nchini mojawapo ikiwa ni kwa kupanda mlima Kilimanjaro.
"'Style' ya upandaji mlima itakuwa ya kipekee. Zaidi ya watu 300 watapanda mlima kilimanjaro, mpaka sasa zaidi ya watu 120 wameshathibitisha kupanda na kasi ya kuthibitisha ni kubwa sana hivyo tunaomba wale ambao hawajathibitisha wafanye haraka kusajili kupitia kampuni ya Zara tours, ambao ndiyo wanashirikiana na serikali kuratibu zoezi hilo, " alisema Waziri Ndumbaro na kuongeza
....Unapochelewa kujisajili unaweza kukuta ile namba ya watu 300 imetimia ukakosa hiyo fursa adhimu ya kupanda mlima kusherekea miaka 60 ya uhuru".
Waziri Ndumbaro alisema kuwa gharama za kupanda mlima zimepunguzwa sana ili kutoa fursa kwa watu wengi zaidi kuweza kumudu ambapo itakuwa ni shilingi laki 8 kwa siku tano mpaka saba.
"Kumbukumbu inatuambia siku kama hiyo mwaka 1961 Luteni wa jeshi alipanda mlima ule na kuweka bendera juu ya kilele cha mlima huo mrefu kuliko yote barani Afrika," amesema Dkt Ndumbaro na kuongeza.
....Sisi tunataka miaka 60 tukumbuke zoezi hilo, tuwaombe wananchi wa kawaida, wanamichezo, vyama vya siasa vyote, kuna vyama vinajisifia sana vina vijana basi wawalete vijana wao kwenye zoezi hilo la kizalendo.
...wasanii, wabunge japo wabunge wengi wameshajisajili, vyombo vya ulinzi na usalama na watu maarufu wote tyjitokeze kwa wingi kuhakikisha siku hiyo inakuwa kweli ni kushereke miaka 60 ya uhuru wa Tanzania Bara,".
Hata hivyo Waziri Ndumbaro alisema kuwa licha kuwa wamejipanga kwa watu 300 ila idadi ikizidi wataongeza njia zitakazotumika kupanda mlima huo kwani njia ya Marangu ina uwezo wa kutumia na wapanda mlima 120 kwa wakati mmoja hivyo wanaoongezaka watatumia njia nyingine.
Mlima Kilimanjaro mbali na njia ya Marangu pia zipo njia za Machame, Umbwe, Rongai na Lemosho ambazo zote zinakufikisha kwenye kilele cha Kibo ambacho, kina urefu wa mita 5895 (futi 19340), na ndicho kivutio kikubwa kwa sababu ya kufunikwa na theluji mwaka mzima.
Lakini pia watakaopanda watapata fursa ya kuona kuna vilele vingine kama Shira, upande wa magharibi, kikiwa na urefu wa mita 3962, Mawenzi upande wa mashariki, chenye urefu wa mita 5149.
No comments:
Post a Comment