Gari iliyowabeba watuhumiwa ikitoka mahakamani
ASKARI watatu wanaotuhumiwa kushawishi na kupokea rushwa kutoka kwa mmiliki wa kampuni ya Germs and Rocks Venture, Sam Mollel wamefikishwa mahakamani kisha kurejeshwa rumande kituo cha polisi bila kufikishwa mbele ya hakimu.
Watuhumiwa hao, Heavenlight Mushi, Gasper Paul na Bryton Murumbe walifikishwa mahakama ya hakimu mkazi Arusha jana (januari 11, mwaka huu) majira ya saa mbili asubuhi ambapo walikaa kwenye mahabusu ya mahakama hiyo pamoja na mahabusu wengine.
Ilipofika majira ya saa sita mchana watuhumiwa hao walitolewa kwenye chumba cha mahabusu cha mahakama hiyo huku wakiwa wamefunika sura zao kwa shuka za kimasai walipakizwa kwenye gari ya polisi aina ya land Rover na kuondoka wakiwa chini ya ulinzi mkali wa askari polisi wenye silaha za moto.
Kamanda wa polisi mkoani hapa, Salim Hamduni akiongea na mwandishi wa habari kwa njia ya simu alisema kuwa watuhumiwa hao wamerejeshwa rumande kwenye kituo cha polisi kutokana na hati yao ya mashitaka kutokuwa tayari.
"Sisi tulikamilisha upelelezi tukawaachia wenzetu ofisi ya mwendesha mashitaka waendelee kuandaa hati ya mashitaka. Kuna taratibu hazijakamilika ndiyo maana wanarudishwa polisi. Ofisi ya mwendesha mashitaka inajitegemea hivyo ukiwasiliana nao unaweza kujua kwa undani," alisema RPC huyo na kuongeza.
Sisi tunasubiri maelekezo kutoka ofisi ya mwendesha mashitaka. Kama jalada la polisi lina ushahidi au halina na nini sisi tunasubiri maelekezo ya kisheria kutoka kwao,".
Mwendesha mashitaka mfawidhi mkoani hapa, Abdallah Chavula alipotafutwa na waandishi wa habari kwa njia ya simu alisema yuko likizo.
Awali desemba 24, mwaka jana watuhumiwa hao wakiwa ni askari namba G. 5134 DC Heavenlight Mushi aliyekuwa Askari kitengo Cha Intelijensia Mkoa wa Kipolisi Kinondoni jijini Dar es Salaam, H.125 PC Gasper Paul kitengo Cha Intelijensia Makao Makuu Dodoma na H.1021 PC Bryton Murumbe aliyekuwa Askari wa kawaida Mkoani Dodoma inadaiwa walikamatwa wakipokea rushwa ya shilingi milioni 10 kutoka mfanyabiashara wa madini Mollel.
Januari 7, mwaka huu RPC, Hamduni aliwaeleza waandishi wa habari kuwa askari hao walishitakiwa kijeshi nankupatika na hatia hivyo walipewa adhabu ya kufukuzwa kazi kwa fedheha.
Askari walidaiwa kushirikiana na raia sita katika kupanga njama za kuomba rushwa ya shilingi milioni 30 wakiwemo mfanyabiashara na mkazi wa Makole Dodoma ,Shabani Benson, (40), Leonia Joseph, (40) mkazi wa Ilboru mfanyakazi wa kampuni ya Gem and Rock Venture, Joseph Chacha, (43) mkazi wa llboru, Omary Mario,(43).
Wengine ni pamoja na mfanyabiashara na mkazi wa Olorien Jijini Arusha ,Nelson Lyimo, (58) mfanyabiashara na mkazi wa Kimandolu Jijini Arusha na mfanyabiashara maarufu wa madini ya Tanzanite Jijini Arusha Lucas Mdeme, (46) ambaye na pia ni meneja wa kampuni ya kuuza na kununuwa madini nje ya nchi ya Crown Lapidary ya Arusha.




No comments:
Post a Comment