Tuesday, January 5, 2021

GIGY AWAPONZA WASAFI TV

 
MAMLAKA  ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imeisitisha utoaji huduma za utangazaji kwa Televisheni ya Wasafi TV  kwa muda wa miezi 6 kuanzia leo hadi Juni 2021 baada ya kukiuka taratibu za utangazaji.


Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo Johannes Kalungula, amesema maamuzi hayo yanatokana na ukiukwaji huo uliofanyika kupitia kipindi cha "Tumewasha Concert," Wasafi Tv.

Kipindi hicho kulirushwa hewani  Januari Mosi, 2021 majira ya saa mbili hadi saa tano usiku iliyorusha maudhui ya picha jongefu yaliyomwonesha msanii wa bongo Fleva Gift Stanford Mwakyusa maarufu kama Gigy Money akicheza katika jukwaa kwa mitindo.


Gigy Money

Msanii huyo alionekana akiwa anaonyesha   utupu wa mwili wake kinyume na kanuni  namba 11 (1) (b) (c) na (d) za kanuni za Mawasiliano ya kielektroniki na Posta (Maudhui ya utangazaji wa Redio na Televisheni,) ya mwaka 2018 inayomtaka mtoa huduma wa maudhui kuhakikisha kuwa hatangazi maudhui yasiyozingatia utu na maadili ya Jamii.


Aidha Wasafi TV wametakiwa kutumia siku ya leo iliyobaki kuahirisha matangazo yote na kutumia muda wote uliobaki siku ya leo kuomba radhi kwa Umma wa watanzania wake kufuatia ukiukaji wa kanuni za utangazaji kupitia kipindi cha "Tumewasha Live Concert." 


Kalungula amesema  wakikaidi au kukataa hatua zaidi za kisheria na udhibiti zitachukuliwa dhidi ya Wasafi TV.

No comments:

Post a Comment