HABARI: JAJI KESI YA LEMA AAGIZA MAWAKILI WA SERIKALI WASAKWE


JAJI wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Dkt Modester Opiyo, agoma kuahirisha kesi kutokana na mawakili wa Serikali kutokuwepo badala yake akaagiza watafutwe mpaka wapatikane kesi iweze kuendelea.

Jaji huyo aliagiza hayo jana baada ya wakili wa mleta rufaa, mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, (CHADEMA), Sheki Mfinanga kuomba mahakama ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kusikilizwa kwa shauri hilo la rufaa kwani mawakili wa Serikali hawapo.

Aidha, Wakili Mfinanga,  aliomba mahakama impatie hati nyingine  ya kuwaita mawakili hao wa Serikali mahakamani hapo ili awapelekee tena ingawa wenye jukumu hilo ni Mahakama.

Jaji Dk Opiyo alisema kuwa hapendi kuona shauri hilo la rufaa ya jinai namba 48/2017 iliyowasilishwa Lema linavyokaa bila kuendelea kwani lilifika mbele yake kwa mara ya kwanza mwezi machi mwaka huu.

"Mimi hainisaidii chochote kesi hii kuendelea kukaa hapa, naomba namba ya simu ya wakili Njau au Nuda  (wakili wa Lema, Sheki akajibu hana ila akadai amewaona mahakamani hapo wakamwambia wana kesi nyingine mahakama ya hakimu mkazi Arusha) nenda kawaite," aliagiza Jaji huyo.

Baada ya kuwasili mawakili hao, Innocent Njau na Khaliki Nuda  walidai kuwa ofisi yao haijapata wito wa Mahakama kwa ajili ya shauri hilo jambo ambalo Jaji Dk Opiyo aliwahoji kama hawakuwa na wito ilikuwaje wakili wa Serikali, Penina Joachim alikuwa mahakamani hapo wakati shauri hilo lilipotajwa Mei 10, mwaka huu.

Wakili Njau aliomba kwa jana shauri hilo liendelee kusikilizwa kama ilivyokuwa imepangwa ila wao wataenda kufuatilia kwenye masjala ya ofisi yao kuona kama kuna hati hiyo ya wito wa mahakama.

Julai 12, mwaka huu shauri hilo lilishindwa kuendelea mahakamani hapo baada ya Mawakili wa Serikali kushindwa kutokea mahakamani hapo.

SHAURI HILO KUSIKILIZWA KWA NJIA YA MAANDISHI

Jaji Dk Opiyo alimwagiza wakili wa Lema kuwasilisha mahakamani hapo hoja zake za rufaa kwa njia ya maandishi Agosti 30, mwaka huu ambapo upande wa Jamhuri watatakiwa kuwasilisha hoja za majibu Septemba 13, huu.

Alisema kuwa mawakili wa Lema watawasilisha hoja za ziada Septemba 20, mwaka huu kabla ya kukutana Mahakamani hapo Septemba 27, mwaka huu kwa ajili ya kupanga tarehe ya kutoa uamuzi.

RUFAA

Uamuzi mdogo uliokatiwa rufaa ulitolewa februari 8, mwaka huu na Hakimu Mkazi,Bernad Nganga,  wa mahakama ya hakimu Mkazi Arusha,  kwenye shauri la jinai namba 352/2016 ambaye alitupa pingamizi lililowasilishwa na mawakili wa Lema wakitaka  shauri hilo likasikilizwe na majaji watatu kutokana na hati ya mashitaka kujumuisha masuala ya  kikatiba.

Akisoma uamuzi huo mdogo, Hakimu Mkazi, Nganga alisema kuwa mara baada ya kupitia hoja za pande zote mbili ameamua shauri hilo liendelee kwenye mahakama hiyo huku akidai kuwa endapo kuna masuala ya kikatiba yatakosa majibu basi itawanufaisha upande wa utetezi.

"Ushahidi wa Jamhuri kushindwa kutolewa  hautakuwa na madhara kwa mshitakiwa bali utamfaidisha na hoja ya shauri kuwa na masuala ya kikatiba, hoja hiyo huwezi kuitambua kwa kuangalia vifungu alivyoshitakiwa navyo mshitakiwa na kama ni hivyo hoja hiyo iletwe wakati wa utetezi kama kesi itafika hatua ya utetezi.

"Pingamizi zinatupiliwa mbali na mahakama hii haijaona haina uwezo wa kusikiliza hivyo tutaendelea na kesi ya msingi," alisema hakimu Nganga akihitimisha uamuzi wake.

Alisema, alipitia hati ya mashitaka inayoeleza kuwa Lema anashitakiwa kwa kosa la kushawishi kutenda kosa kinyume na kifungu cha 390 na cha 35 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jianai  ambapo anadaiwa kuhamasisha watu kufanya kusanyiko na maandamano isivyo halali.

"Baada ya kupitia hati hiyo na kwa mujibu wa kifungu cha 390 kinaelezea mtu akihusika na kushawishi kosa,hata kama halina madhara huyo mtu ni mkosaji.Kifungu cha 35 kinaelezea iwapo mtu akikutwa na hatiani kwa kosa hilo adhabu yake ni kifungo cha miaka miwili au faini au vyote viwili kwa pamoja," alisisitiza hakimu huyo

Baada ya uamuzi huo wakili wa Lema, Sheki Mfinanga aliwasilisha kusudio la kukata rufaa kwa njia ya mdomo kwa kile alichoeleza kuwa hawajaridhika na uamuzi huo na kuomba kuwasilisha notisi hiyo ambayo ina nguvu sawa na rufaa huku akiomba kupatiwa mwenendo wa kesi hiyo pamoja na uamuzi huo mdogo  ili waweze kuandaa rufaa hiyo na kuwasilisha Mahakama Kuu.

"Tunaupinga uamuzi huu ulioutoa na tunaomba kuwasilisha notisi ya kukata rufaa ambayo ina nguvu sawa na rufaa na tunaomba shauri lisiendelee kwanza mpaka Mahakama Kuu ikasikilize rufaa yetu dhidi ya uamuzi huu," alisema Mfinanga.

0 Comments:

Post a Comment