UPDATES: THRDC Waguswa wasikitishwa na tukio la shambulio la ofisi za mawakili wa IMMMA , Walinzi wakutwa Kawe hawajitambui ..


 Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu umesikitshwa sana na tukio la kuvamiwa ofisi ya mawakili ya IMMA usiku wa kuamkia leo tarehe 26/08/2017. Tunatambua kuwa wanasheria ni kundi kubwa katika makundi ya watetezi wa haki za binadamu hapa nchini na duniani kote. Wanasheria husaidia wananchi kupata haki zao kwa njia za amani katika mahakama zetu , wanasheria pia hutetea haki za wananchi mahakamani pale zinapovunjwa , wanasheria pia ni watetezi wakubwa wa katiba na utawala wa sheria. Hivyo kitendo chochote kinachokwenda kuzua hofu katika kundi hili madhara yake ni makubwa kwa taifa na katika mfumo wa utoaji haki.

Tutambue kuwa mawakili au wanasheria ni sehemu ya mahakama , na  mahakama haiwezi kukamilika au kuendesha kazi zake bila wanasheria kwani kwa mujibu wa Sheria Mawakili ni Maafisa wa Mahakama na wao ndio wanaoisaidia Mahakama katika kutenda haki. Sisi kama Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu tunalaani tukio hili na kutoa pole kwa mawakili na wafanyakazi wote wa Kampuni ya Mawakili ya IMMA. Tutapenda kuona wahusika wote wa tukio wakifikishwa mbele ya vyombo vya sheria kujibu tuhuma zinazowakabili na huu uwe ndio muda sasa wa kutumia mashtaka binafsi dhidi ya matukio kama haya. Mietolewa na Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) Onesmo Olengurumwa. Leo tarehe 26/08/2017


Vilivile habari za hivi punde zimeeleza kuwa Walinzi wawili ambao walikuwa wanalinda ofisi za wanasheria za IMMMA zilizoshambuliwa wamekutwa maeneo ya Kawe jijini Dar Es Salaam,wakiwa hawajitambui mithili ya watu walioleweshwa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Uwakili ya IMMMA, Sadoc Magai ameelezea, kuwa chanzo cha tukio hilo hakijajulikana lakini alikuta mapipa ya Petrol, pia vioo vimepasuka na mlango mkubwa wa kuingilia ofisini humo umebolewa kwa kitu kinachoonekana ni mlipuko.

”Hakuna majeruhi na hakuna kilichoibiwa zaidi ya athari za jengo, ambapo jengo hili lina ofisi za mawakili 25.” amesema mkurugenzi mtendaji wa IMMMA, Sadoc Magai alipozungumza na wahabari.

0 Comments:

Post a Comment