Monday, August 21, 2017

UPDATES: " ...Namtaka IGP Sirro ailekeze jeshi lake..." Lema


WAZIRI kivuli wa Mambo ya Ndani, Godbless Lema, amemtaka Inspekta Jenerali wa Jeshi la Polisi nchini, (IGP), Simon Sirro, kuwaelekeza polisi wafanye kazi kwa kuzingatia weledi na si kufuata maelekezo ya wanasiasa kwani inaweza kuhatarisha amani ya nchi.

Aidha ameitaka Serikali kuiga mfano wa kudumisha demokrasia  kwa nchi jirani ya Kenya ambapo Rais, Uhuru Kenyatta, aliwaagiza polisi kuwapa ulinzi waandamanaji waliokuwa wakipinga ushindi wake.

Lema ambaye pia ni mbunge wa Arusha Mjini, (CHADEMA), aliyasema hayo ofisini kwake wakati akilaani kitendo cha Jeshi la Polisi Kanda maalum Tarime na Rorya kumshikilia mbunge wa Bunda, Ester Bulaya, (CHADEMA), na kumuhoji kwa kufanya mkutano nje ya jimbo lake eneo la Nyamongo jimbo la Tarime Vijijini.

"Tunaona polisi wakitekeleza maagizo,  tunajiuliza maagizo haya wanasema ni amri ya Dc (mkuu wa wilaya)  au RC (Mkuu wa Mkoa) namtaka IGP Sirro alielekze jeshi lake lifanye kazi kwa weledi. Siyo kila amri itakuwa na afya katika Taifa hili, siyo kila amri ambayo utaitii itakuwa na  aana katika Taifa hili,maana leo DC akisema Mbunge apigwe risasi,kabla ya saa 12 jioni,tutapigwa risasi?," alihoji Lema.

Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya CHADEMA alisema kuwa analaani vikali kitendo cha kukamatwa kwa mbunge wa Bunda, Bulaya kwa kosa alilodai kuwa halipo kisheria huku mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, (CHADEMA) akidaiwa kuwa mafichoni kwa sababu naye anatafutwa na polisi ahojiwe kwa kushiriki mkutano wa hadhara kwenye jimbo la Tarime Mjini.

"Kosa la Bulaya ni kwenda kuhudhuria mkutano wa hadhara Tarime,kwa kosa ambalo hata katika sheria ya Tanzania hakuna,na hata kama sheria itafanyiwa marekebisho gani huwezi kutunga sheria ya kuzuia mbunge au mtu yoyote kuongea ndani ya mipaka ya Taifa lake ilimradi havunjia sheria," alisema Lema na kuongeza.

"Hiki  kinachofanyika siyo tu kinaua demokrasia na uhuru wa kutoa maoni na haki ya kutembea popote.Hiki kinatengeneza mpasuko mbaya katika Taifa na mbegu hii ikishaota yatakuja machafuko makubwa," alionya Lema.

Aliohoji sababu za ukimya wa idara ya usalama wa Taifa wakati kukiwa na matendo hayo aliyodai ni hatari kwa usalama huku akiuliza endapo taasisi hiyo inayaona kwani watu watakaoshindwa kuvumilia ukiukwaji wa haki za binadamu, udhalilishaji, kamatakamata wabunge isiyozingatia sheria wakihoji nao hukamatwa.

"Leo DC anaweza akaamua akasema weka ndani yule (kushikiliwa kituo cha polisi) na mtu akakamatwa ,tunaendelea kuvumilia mateso lakini nirudie kusema kuna kizazi kinakuja ambacho hakitahubiri kwa "microphone" wala kulalamika kupitia vyombo vya habari,hakitalia kupitia mitandao ya kijamii, kitaamini katika siasa za jino kwa jino kwa jino," alionya Lema na kuongeza.

"Naonya sana kwa sababu napenda nchi yangu,hiki kinachofanyika ni kitu kibaya kinaligawa Taifa na kitaleta ubaguzi mkubwa sana katika Taifa letu.

"Roma (msanii) amewaambia vizuri sana wekeni silaha chini tupambane kwa hoja, Bulaya amekamtwa alienda Tarime vijijini,Heche anatafutwa alienda Tarime Mjini kwa Matiko (Ester). Kitendo hiki kinaleta mpasuko mkubwa kwa jamii,".

AMWAGIA SIFA KENYATTA

Lema alisema kuwa tupaswa kuiga mfano kwa nchi ya Kenya ambayo licha ya kuwa majirani zetu lakini Yuko nayo kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki, (EAC) kwa namna inavyodumisha demokrasia.

"Rais Kenyatta jirani yetu hapa, wapinzani wake waliamua kuandamana na kufanya  mkutano wa hadhara kumpinga,na kumshutumu chama chake kimeiba kura, Uhuru aliagiza Jeshi la  Polisi  litoke hadharani likalinde waandamanaji,hii ndiyo demokrasia iliyokua," alisema mbunge huyo.

VIONGOZI WA DINI WAKEMEE

Lema aliwataka viongozi wa dini kukemea matendo yote maovu ikiwemo ukiukwaji wa katiba ya nchi na haki za binadamu badala ya kujikita kwenye kukemea unywaji wa vileo tu.

"Niombe taasisi za dini, maaskofu, masheikh na  wachungaji, wasijifanye mambo haya hawayaoni, kazi yao isiwe kukeme bia tu na viroba, kazi yao iwe hasa kukeme ukiukwaji wa misingi ya katiba,sheria inayoendela katika Taifa letu, manyanyaso, udhalilishaji uanoendelea dhidi ya wapinzani ilitulikomboe taifa letu na vita vya wenyewe kwa wenyewe,haki ikiendelea kudhalilishwa watu hawa siku moja watashindwa kuvumilia, " alionya Lema.

No comments:

Post a Comment