Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Dokta Vincent Mashinji ni mmoja wa Viongozi wa Umoja wa Vyama vya Kidemokrasia Duniani (IDU) walioalikwa kukutana na Rais wa Ghana, Nana Akufo-Addo nchini humo, Jumatano, Juni 21, mwaka huu, ikiwa ni sehemu ya mkutano wa umoja huo unaofanyika mjini Accra, Ghana.
Mbali ya kukutana na Rais Nana Akufo-Addo, Dokta Mashinji atakutana na Rais Mstaafu wa Ghana John Agyekum Kufuor kwenye mazungumzo yatakayofanyika Juni 20, mwaka huu, baada ya ujumbe huo wa IDU kutembelea Bunge la Ghana.
Viongozi hao mbali ya kubadilishana uzoefu wa mazingira tofauti ya kisiasa, watatumia mkutano huo kujadili masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na namna ambavyo nchi zao zinaweza kusimamia misingi ya kidemokrasia kwa ajili ya maendeleo na ukuaji wa kiuchumi, kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na jinsi ya kunufaika na ongezeko kubwa la vijana.
Mkutano huo wa IDU ulioanza Juni 19, mwaka huu, unawakutanisha viongozi kutoka nchi mbalimbali wakiwemo pia viongozi kutoka Umoja wa Vyama vya Kidemokrasia Afrika (DUA), miongoni mwao akiwa ni; Kiongozi wa Chama cha Forum for Democratic Change (FDC), ambaye pia ni Mwenyekiti wa DUA Dokta Kizza Besigye kutoka Uganda, Katibu Mkuu wa DUA Charles Owiredu na Mwenyekiti wa Heshima wa DUA, Peter Mac Manu.
Katibu Mkuu Dokta Mashinji aliyeondoka Juni 18, kwa ziara hiyo ya kikazi atarejea nchini Juni 22, mwaka huu.
*Imetolewa leo Jumatano, Juni 20, 2017 na;*
*Tumaini Makene*
*Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano*
No comments:
Post a Comment